Breaking News

TPSC YATAKIWA KUTOA MAFUNZO YATAKAYOWAWEZESHA WATUMISHI WA UMMA KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI.


 


NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi alipowatembelea  ofisini kwao Makao Makuu ya TPSC Jijini Dar es Salaam  jana Januari 13, 2019. Kulia ni Mkuu wa Chuo hicho Dk. Henry Mambo. (Picha zote na James Mwanamyoto-UTUMISHI). 

Na James Mwanamyoto

WATUMISHI wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wametakiwa kutoa mafunzo bora yenye kuzingatia weledi, yatakayowajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa umma wanaopata fursa ya kujiendeleza katika chuo hicho ili waweze kutoa huduma bora na kwa wakati kwa jamiii.

Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, wakati akizungumza na watumishi wa TPSC Makao Makuu na Kampasi ya Dar es Salaam.

MKUU wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dk. Henry Mambo, akieleza  majukumu ya TPSC kwa Naibu Waziri Dk. Mary, wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa TPSC cha kuhimiza uwajibikaji.


Dk. Mary, alizungumza na watumishi hao jana Januari 13, 2019 ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara zake za kikazi zenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu majukumu na kujiridhisha na utendaji kazi wa taasisi zilizoko chini ya wizara yake ambapo jana alipembelea chuo hicho.

Naibu Waziri Mary, aliwahimiza watumishi wa TPSC kuwa wabunifu kwa kuboresha mitaala itakayowaandaa vema watumishi wa umma, sekta binafsi na wananchi wanaohitimu katika chuo hicho ili waweze kuwa na mchango katika maendeleo ya taifa.

 DK. Mary, akikagua daftari la mmoja wa wanafunzi wa  Chuo cha Utumishi  alipowatembelea  wanafunzi  hao  katika moja ya madarasa  ya Kampasi ya Dar es Salaam ambapo aliwaasa wasome kwa bidii ili wawe watumishi bora  wa umma hapo baadae.

Alisema kuwa, katika ulimwengu wa sasa  jamii inabadilika, uchumi unabadilika na siasa  zinabadilika pia, hivyo amewataka  watumishi wa TPSC wabadilike ili utendaji wao uwe wenye kujali matokeo  na wenye tija. 

Aidha, Dk. Mary, alipata fursa ya kutembelea madarasa ya Kampasi ya Dar es Salaam ili kujionea vitendea kazi na kuzungumza na wanachuo ambao walimueleza kuwa, wanaridhika na elimu inayotolewa, hivyo watatumia elimu na ujuzi watakayoipata  katika kulitumikia taifa.


NAIBU Waziri Dk. Mary, akijaribu kutumia mashine ya kupiga chapa (typewriter) inayotumiwa kutolea mafunzo kwa wanafunzi wa TPSC alipotembelea moja ya darasa katika Kampasi ya Dar es Salaam ya  Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania  Jijini Dar es Salaam.


Naye, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dk. Henry Mambo, alisema, TPSC ilianzishwa ili kusaidia kujenga uwezo wa watumishi wa umma uwe wenye kujali matokeo katika kutoa huduma bora kwa umma.

Alisema, kwa sasa chuo kina matawi sita yaliyopo Dar es Salaam, Mtwara, Singida Tabora,Tanga na Mbeya.

Dk. Mambo alifafanua kuwa, madhumuni makubwa ya kuanzisha chuo ilikuwa ni kuziba pengo lililokuwepo la kukosekana kwa chuo rasmi kinachoshughulikia mafunzo ya watumishi wa umma ili waendane na mabadiliko yaliyoletwa na maboresho katika utumishi wa umma.

Alisema, lengo lingine lilikuwa ni kusaidia, kukuza na kuboresha stadi za wafanyakazi, kubadili mtazamo juu ya utendaji wa watumishi wa umma katika suala zima la utoaji huduma bora kwa umma unaolenga kukuza uchumi na kuondoa umaskini kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu.
DK. Mary, akizungumza na  wanachuo  wa TPSC waliopo Maktaba ambapo aliwataka kutumia vema maktaba hiyo ya chuo kujisomea ili kuongeza  uelewa wa masomo wanayosoma.


Kwa mujibu wa Dk. Mambo, tangu chuo kianzishwe mwaka 2000 kimeweza kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 61,221 katika nyanja ya uongozi, menejimenti na utawala.

Aidha, alisema chuo kimeruhusiwa kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa sekta nyingine ikiwemo sekta binafsi iwapo wana mahitaji ya kupata mafunzo ya kuwawezesha kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku.

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ni Wakala wa Serikali iliyoanzishwa mwaka 2000 chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali ya mwaka 1997.

Kuanzishwa kwa Chuo cha Utumishi kunafuatia muungano wa Chuo cha Watumishi wa Serikali, Dar es Salaam (Civil Service Training Centre) na kilichokuwa Chuo cha Uhazili Tabora (Tabora Secretarial College). Chuo cha Utumishi wa Umma kipo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala.

No comments