Breaking News

ZIDISHENI MAPAMBANO KUPINDA VITENDO VYA UDHALILISHAJI-BALOZI IDDI.   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif  Ali Iddi (kulia), akizungumza na Mabingwa wa Soka wa Ligi Kuu ya Zanzibar, kwa Mwaka 2018/2019 Timu za JKU na Zimamoto walipofika Ofisini kwake Vuga kukabidhiwa zawadi zao zilizotolewa na Mdau wa Michezo Mohamed Raza Hassanaali. (Picha zote na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar).
                         Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Balozi. Seif Ali Iddi,  amewakumbusha wanamichezo nchini kutumia nafasi yao kwa kuongeza mapambano dhidi ya  kupinga vitendo vya udhalilishaji vinavyoleta  sura mbaya  katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Alisema Sekta ya Michezo kwa vile ina ushawishi mkubwa  miongoni mwa jamii, inaweza kutumika vyema katika mapambano hayo na kuleta mafanikio makubwa katika jitihada za kukabiliana na kadhia hiyo.
 BALOZI Iddi, akizungumza na mabingwa hao jana Januari 6, 2019.

Balozi Iddi, aliyasema hayo jana Januari 6, 2019  wakati akikabidhi zawadi kwa Timu ya Soka ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar,  kwa mwaka 2018/2019 na mshindi wa pili Timu ya Kikosi cha Zimamoto na Uokozi hafla iliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Vifaa hivyo vilivyoambatana na sh. Milioni 2  kwa JKU na Milioni 1 kwa Zimamoto vilivyotolewa na mdau wa michezo Mohamed  Raza Hassanaali ni pamoja na seti za jezi, viatu, mipira, , pea  40 za viatu kwa timu ya wanawake ya mpira wa Pete ya JKU pamoja na seti ya jezi kwa timu zote za Vikosi vya SMZ.
 

 BAADHI ya Vionmgozi wa Timu ya JKU wakifuatilia Hotuba ya Balozi Seif hayupo pichani wakati wa hafla maalum iliyoandaliwa ya kukabidhiwa zawadi zao.

Balozi Iddi, alisema, suala la udhalilishaji wa kijinsia linalowakumba zaidi watoto na akina mama linaleta athari pia katika nyanja ya michezo vitendo ambavyo vinapaswa kulaaniwa na wadau wote. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  alihimiza uendelezwaji wa nidhamu michezoni ambayo kwa kiasi kikubwa huleta Heshima kwa mchezaji mwenyewe pamoja na Taifa kwa ujumla.

alisema ni vyema timu hasa zile za vikosi zikaonekana kuzingatia zaidi nidhamu kwa kuheshimu maamuzi yanayotolewa na muamuzi wa mchezo ambayo yanakuwa hayana mjadala kwa Wachezaji.

 MDAU wa Sekta ya Michezo Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamed Rza Hassanaali, akisisitiza lengo lake la kuendelea kuunga mkono Sekta ya Michezo.

Amempongeza mdau wa michezo nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini,  Mohamed Raza Hassanaali,  kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya Sekta ya Michezo kwa kipindi kirefu sasa.

Balozi Seif alisema,  Mohamedraza ambae ameshafikia hatua ya kuteuliwa kuwa Mshauri  wa Rais katika masuala ya Michezo kipindi kilichopita kutokana na mchango wake mkubwa anastahiki kuitwa Gurudumu la Michezo.

Alisema katika kuunga mkono jitihada hizo Zanzibar kupitia Serikali yake ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaamua kuimarisha Sekta ya Michezo ili irejee katika hadhi yake ya kutambulika kuwa kituo cha michezo Kimataifa.


 BALOZI Iddi (kushoto), akimkabidhi zawadi mbali mbali Kamishna wa Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Abdullah Ali Malimus, kwa ajili ya  Timu yake ikishikilia nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Zanzibar Msimu wa Mwaka 2018/2019.

Alikumbusha kwamba Zanzibar imeshawahi kubwa bingwa wa michezo mbali mbali Kimataifa akatolea mfano mchezo wa vinyoya, soka, mpira wa Pete pamoja na ule wa Meza.

Mapema  mdau wa michezo, Raza, alisema washirika wa michezo nchini wana wajibu wa kuunga mkono michezo mbali mbali ili kuwapa ari washiriki wa michezo hiyo hasa wanapokuwa kwenye  mashindano.

Raza, alisema uzoefu unaonyesha wazi kwamba timu nyingi nchini humalizia mashindano yao katika mazingira magumu hata zile zinazochukuwa ubingwa.

Alisema alilazimika kutekeleza Ahadi yake aliyoitoa kwa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ya kuwapatia zawadi washindi wa kwanza na wa pili wa Ligi Kuu ya Zanzibar ikiwa kama motisha ya wachezaji ya kuwaongezea nguvu na ari ya kuendelea kushiriki tena kwenye Mashindano yajayo.


 KAMANDA wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar JKU Ali Mtumweni, akitoa shukrani kwa niaba ya wanamichezo wenzake baada ya kupokea zawadi mbali mbali kufuatia timu yake kuibuka na Ushindi wa Ligi Kuu ya Zanzibar.

Wakitoa  shukrani kwa niaba ya wanamichezo wenzao Kamanda wa JKU  Kanali Ali Mtumweni na Kamishna wa Zimamoto  na Uokozi Abdullah Ali Malimus, wameupongeza Uongozi wa  Kampuni  ya  ZAT  kwa uzalendo wake wa kusaidia Sekta ya Michezo Nchini.

Makamanda hao walisema kwa pamoja msaada waliopewa na mdau huyo umekuja wakati muwafaka wakijiandaa kuelekea katika mashindano tofauti na kuongeza ari kwa wanamichezo mbali mbali.

No comments