Breaking News

KALEMANI ATAKA KITUO CHA UMEME KURASINI KIKAMILIKE HARAKA.
WAZIRI wa Nishati, Medard Kalemani ameagiza watendaji 
wa TANESCO wanaosimamia ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Kurasini kuhakikisha kuwa Kituo hicho kinakamilika ifikapo tarehe 10 mwezi Machi mwaka huu.

Kalemani ameyasema hayo leo baada ya kutembelea kituo hicho na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo ambao kukamilika kwake kutawezesha wananchi wa Kigamboni kupata umeme wa uhakika.

“ Kama mnakumbuka, huu mradi umeanza mwaka 2009, na sasa nimeshakagua zaidi ya mara tano na nilipokuja mwezi Novemba mwaka jana tulikubaliana kuwa mradi ukamilike mwezi Februari mwaka huu, lakini sasa mnasema mtamaliza mwishoni mwa mwezi Machi, jambo ambalo silikubali, haiwezekani mradi wa miaka mitatu utekelezwe kwa miaka Kumi,” Amesema Kalemani.

Kalemani pia ameagiza kuwepo kwa vibarua kuanzia kesho katika maeneo yote ambapo mradi unatekelezwa na wafanye kazi usiku na mchana ili kuweza kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa na kuwaondolea changamoto ya upatikanaji umeme wananchi wa Kigamboni, Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha wananchi 9000 kuhudumiwa na Kituo hicho kwa wakati mmoja hivyo inaonesha ni jinsi gani Kituo hicho kilivyo muhimu katika kuwaondolea wananchi changamoto ya kutopata umeme wa uhakika.

Wakati, huohuo, Kalemani amewaagiza Mameneja wa TANESCO katika maeneo mbalimbali jijini Dar es` Salaam kufanya ukaguzi katika maeneo yao ili kufahamu sababu za ukatikaji wa umeme unaotokea wakati nchi ikiwa na nishati ya umeme ya kutosha na ziada.

Kwa upande wake, Meneja Miradi kutoka TANESCO, Mhandisi Stephen Manda, amesema kuwa watatekeleza maagizo ya Waziri wa Nishati na kuyakamilisha kabla ya tarehe 10 mwezi Machi mwaka huu ili kuhakikisha kuwa wanatatua kero za umeme kwa wananchi wa Kigamboni.


Amesema kuwa, moja ya sababu zilizochelewesha mradi huo ni mwananchi mmoja kukataa kupisha eneo linalopitiwa na mradi kwa kudai fidia ambayo ni asilimia 47 ya bajeti yote iliyotengwa kwa ajili ya fidia kwa wananchi wote wanaopisha mradi, hata hivyo, kwa maagizo ya Waziri wa Nishati, walifanya mazungumzo na mwananchi huyo na kwa sasa mradi unaendelea kutekelezwa.No comments