Breaking News

WAPEWA SIKU 7 KWA WATUMISHI KUHAMIA KARIBU NA KAZI


NAIBU WAZIRI, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Zena Said kuhakikisha watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga wanaoishi nje ya vituo vya kazi kuhamia wilayani Mkinga ndani ya siku saba ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati.

Agizo hilo amelitoa wilayani Mkinga wakati wa kikao kazi na watumishi wa halmashauri hiyo, alipowatembelea kuhimiza uwajibikaji kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini  wilayani humo kwa  lengo la kukagua na kujiridhisha kuhusu utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.

Mwanjelwa amesema, watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga wanaoishi nje ya vituo vya kazi na kutumia rasilimali za serikali, ni dhahiri kuwa wanatumia vibaya rasilimali za umma hivyo wanafanya kosa kwa mujibu wa Kanuni, Sheria na Taratibu za Utumishi wa Umma.

Amesisitiza kuwa, ni marufuku kwa mtumishi wa umma yeyote nchini kuishi nje ya kituo cha kazi, kwani kitendo hicho kinawanyima haki ya msingi wananchi wanaohitaji huduma katika Taasisi za Umma kutokana na watumishi wengi kuchelewa kufika kazini kwasababu ya kuishi nje ya vituo vyao vya kazi.

Amehoji uwepo wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga na wakuu wake wa Idara kushindwa kushughulikia tatizo hilo la watumishi kuishi nje ya vituo vya kazi, na kumtaka Mkurugenzi huyo kuhakikisha anashirikiana na menejimenti yake kushughulikia suala hilo kwa wakati na kuongeza kuwa, iwapo tatizo hilo litaendelea kuwepo wilayani humo, itakuwa ni ishara tosha kwamba, wamedhihirisha kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao.

Amewataka watumishi wa umma wilayani humo kuzingatia nidhamu ya kazi na kutochezea fursa waliyonayo ya kuutumikia umma na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwa na utumishi wa umma wenye viwango na unaomjali mwananchi pindi anapofuata huduma katika taasisi za umma.

Aidha, Mwanjelwa  amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Tanga na Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kushughulikia ubadhirifu wa fedha uliopo katika Kituo cha Afya cha Kiwegu na kutaka apatiwe mrejesho mapema iwezekanavyo.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Zena Said amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga na Maafisa Utumishi kuhakikisha ifikapo Februari 21 mwaka huu, watumishi wote wanaoishi nje ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga wawe wameshahamia wilayani Mkinga.

Zena amemshukuru Mwanjelwa kwa kuwahimiza watumishi wilayani Mkinga kuvaa mavazi yenye staha na kumtaka kila mtumishi wa umma wilayani humo kuzingatia Waraka wa Mavazi Na. 3 wa Mwaka 2007.

Kuhusiana na ubadhirifu wa fedha katika Kituo cha Afya cha Kiwegu, Zena amemuahidi Mwanjelwa kutekeleza maelekezo aliyoyatoa kwa wakati  kwa kufanya ufuatiliaji ili kutatua tatizo hilo.

Mwanjelwa anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Tanga yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi kwa umma,  ikiwa ni pamoja na kukagua na kujiridhisha na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na TASAF mkoani humo. Mpaka sasa ameshatembelea Halmashauri ya Mji wa Tanga, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga.
No comments