Breaking News

ONGEZEKO LA BAJETI LAIPAISHA TANZANIA KATIKA VIWANGO VYA AFYA.


WAZIRI MKUU wa Jamuhuri ya Muunano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema ripoti ya kamati maalumu kuhusu masuala ya afya barani Afrika, inaonesha Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri barani humo.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Februari 11, 2019) wakati akitoa muhtasari wa yaliyojiri kwenye Mkutano wa 32 wa Wakuu wa nchi za Afrika (AU) unaofanyika Addis Ababa, Ethiopa. 

Amesema Tanzania imefanya vizuri katika kusimamia na kudhibiti malaria, mapambano dhidi ya ukimwi pamoja na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi mpaka vijijini.

“Imetupa faraja kwa sababu ukaguzi uliofanywa na kamati maalumu ya maendeleo ya afya, iliyotembelea nchi za Afrika kuona mwenendo wa utoaji wa huduma za afya imeonesha kwamba Tanzania tupo kwenye kiwango kizuri.”

amesema mafanikio hayo yamekuja baada ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kuongeza bajeti ya wizara afya  kutoka sh. bilioni 37 hadi kufikia sh. bilioni 269.

Katika mkutano huo, viongozi wa AU wamekutana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu biashara, wakimbizi na usalama, pia wamemchagua  Rais wa Misri, Abdul Fatta Al Sisi kuwa Mwenyekiti mpya wa umoja huo.
Al Sisi anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame kumaliza muda wake baada ya kushika wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema licha ya changamoto zote zinazolikabili bara la Afrika, bara hilo limeacha milango yake wazi kwa wakimbizi, hivyo ameyataka nchi za Ulaya ambazo zimefunga milango yake kwa wakimbizi zijifunze kutoka kwa Afrika.

No comments