Breaking News

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA BARRICK GOLD CORPORATION IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John  Magufuli akiwa na Waziri wa Sheria na Katiba Palamagamba Kabudi na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Florens Luoga katika picha ya pamoja  na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ( kwa Afrika na Mashariki ya Kati) Willem Jacobs na ujumbe wake baada ya kukutana na kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaa leo Februari 20, 2019.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli leo tarehe 20 Februari, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold anayeshughulikia Afrika na Mashariki ya Kati Willem Jacobs, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Willem Jacobs aliyeongozana na washauri wa Barrick Gold Corporation ambao ni Rich Haddock, Duncan Bullivant na Wicus du Preez amesema wamekutana na Mhe. Rais Magufuli ili kumhakikishia kuwa makubaliano yaliyofikiwa tarehe 19 Oktoba, 2017watayatekeleza kikamilifu hasa baada ya kampuni kubwa ya uchimbaji dhahabu ya Rand Gold ya Afrika Kusini kuungana na Barrick Gold Corporation katika umiliki, uwekezaji na menejimenti.

Willem Jacobs amebainisha kuwa hakuna kitakachokuwa tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali ambayo yaliongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick Gold Corporation John Thornton ikiwemo Barrick Gold Corporation kuilipa Serikali ya Tanzania kifuta machozi cha Dola za Marekani Milioni 300 (sawa na shilingi Bilioni 682.5), kuendelea na uwekezaji kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold na mgawanyo wa mapato ya kiuchumi kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold.

Willem Jacobs amempongeza Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia maslahi ya Watanzania katika rasilimali za nchi yao na amesema pamoja na ukweli kwamba Rais Magufuli yupo katika njia sahihi, yeye akiwa Mwafrika anaunga mkono juhudi hizo kwa kuwa ndio mwelekeo sahihi ambao nchi za Afrika zinapaswa kuufuata.

“Mimi ni Mwafrika na sisi sote ni Waafrika, anachokifanya Mhe. Rais Magufuli ni sahihi kabisa, anahakikisha utajiri wa rasilimali uliopo unabainishwa na unawanufaisha Watanzania, na ndio maana tupo hapa kwa sababu tunakubaliana na Rais.

Na hivi ndivyo sisi Waafrika tunapaswa kufanya kwa rasilimali zetu, na sisi tunahakikisha tunafanya kazi vizuri na Serikali na jamii kulinda rasilimali hizi, kumbuka rasilimali hizi ni za wananchi, jukumu langu kama mwekezaji ni kubadili hayo madini kuwa kodi na ajira kwa Tanzania na pia kampuni yangu kupata faida yake halali” amesema Dkt. Willem Jacobs.

Amebainisha kuwa baada ya muungano huo wa Rand Gold na Barrick Gold, sasa Kampuni mpya ya Barrick Gold imekuwa kampuni kubwa inayoongoza kwa umiliki wa rasilimali za dhahabu duniani ikimiliki rasilimali 5 kati ya 10, na kwamba kutokana na uwezo huo Barrick Gold Corporation sasa imeweza kujiimarisha zaidi kiuwekezaji na utaalamu na ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha rasilimali ya dhahabu iliyopo inaleta manufaa kwa pande zote mbili yaani Watanzania na mwekezaji.

Waziri wa Katiba na Sheria Palamagamba Kabudi ambaye ameongoza timu ya majadiliano kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold amesema nyaraka za makubaliano hayo zimekamilika na kwamba sasa kinachosubiriwa ni utekelezaji wa makubaliano hayo unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwezi Machi 2019.

“Baada ya muungano wao (Rand Gold na Barrick Gold Corporation) hii sasa ni timu mpya na tumewaona ni watu ambao sasa wapo tayari kutekeleza yale yote yaliyokubaliwa, na sasa ni kwa kila upande kwenda kwenye vyombo vyake vinavyohusika kufanya maamuzi ya mwisho ili utekelezaji ufanyike” amesema Kabudi.

No comments