Breaking News

VIJANA NCHINI WATAKIWA KUANZISHA VIJIWE VYA UCHUMI.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuanzisha vijiwe vya kiuchumi.

Ametoa wito huo leo February 26, wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo na miradi ya vijana iliyopo katika Kituo cha Maendeleo ya Vijana, Sasanda kilichopo Kata ya Nyimbili, Mkoani Songwe.

Akiwa katika ziara hiyo Jenista alieleza kuwa, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imeendelea kutimiza azima yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, hivyo vijana watumie fursa hiyo kujifunza mambo muhimu na kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vitawafanya wabadilishe vijiwe wanavyokaa kuwa vya kiuchumi.

“Tunataka kuona vijana watakapo jifunza kilimo bora, ufugaji wa ng’ombe au nyuki wataweza kuboresha thamani mazao na bidhaa kwa kuanzisha viwanda vidogo ndani ya Mkoa wa Songwe, mkakati wetu katika kituo hiki ni kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana kuongeza thamani ya mazao na bidhaa watakazozalisha ambazo zitakuwa ni kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo yao” alisema Jenista.

Aliongeza kuwa, Takribani vijana 500 kwenye kituo hicho wamejifunza stadi za maisha, ufundi na elimu mbalimbali zinazotolewa kwenye kituo ambazo zitawawezesha kujipatia kipato.

Sambamba na hilo, Jenista aliwahimiza Viongozi wa Mkoa kushirikiana na Ofisi yake ili waweze kuwasaidia vijana ambao wamekwisha anzisha viwanda vidogo vidogo ndani ya mkoa huo kwa kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwatafutia soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Aidha, Waziri Jenista alitoa rai kwa vijana kujiunga kwenye vikundi ambavyo ni endelevu na vyenye muelekeo  wa kuanzisha viwanda  vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wenzao na pelekea kufikia uchumi wa kati kama mpango wa maendeleo wa taifa unavyoelekeza. 


No comments