Breaking News

TRA SONGWE KUKAMATA MAGARI YA IT YANAYORUDI NCHINI KINYEMELA.


MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) mkoani Songwe, imeanza doria ya kila siku ya kuyakamata magari ya IT yanayovuka mpaka kisha kurudi nchini kinyemela bila kulipiwa ushuru.

Akizungumza ofisini kwake leo Meneja wa TRA mkoani Songwe, Paul Walalaze, alisema doria hiyo imeanzishwa ili kukabiliana na changamoto iliyoanza kuota mizizi ya magari yenye namba za IT kuvuka mpaka wa Tunduma kisha kurudi nchini kinyemela bila kulipia ushuru.

Akifafanua uingizaji huo, meneja huyo alisema kuna watu wanaingiza magari bandarini Dar es salaam kisha wanakuwa na nyaraka zinazoonesha kwamba gari linakwenda katika nchi jirani zinazopakana na Tanzania na kuwa na namba za Kimataifa (IT) lakini baadae zinarudi tena nchini kinyume cha sheria.

Walalaze alisema gari hizo zinapovuka mpaka wa Tanzania kwa upande wa Zambia, zinabadilishwa namba na kuwekwa namba za Tanzania na kurudi nchini tena bila kufuata taratibu za kulipiwa ushuru.

"Ili kukabiliana na changamoto hii, tumeanzisha doria ya kila siku, na tunamshukuru Kamishina Mkuu ametupatia gari la kutuwezesha tuwe barabarani kila siku na muda wowote," alisema Walalaze.

Meneja huyo alisema uchunguzi walioubaini ni kwamba vitendo hivyo vya uingizaji magari kinyume cha sheria umekuwa ukifanywa na baadhi ya askari wa mji wa Kibaha na Dar es salaam.

Alisema uingizaji huo umekuwa ukifanywa baada ya magari yao ya awali kuharibika au kupata ajali na wao huagiza gari la aina ile ile ili iwe rahisi kubadilisha namba za gari.

"Magari mengi yanayopitishwa kwa aina hiyo tumegundua ni ya askari wa Kibaha na Dar es salaam, magari yao yanapopata ajali hununua mengine na kutumia mbinu hiyo ya magari ya IT," alisema Walalaze.

Alitaja na kuonesha baadhi ya magari yaliyokamatwa kwa mbinu hizo kuwa pamoja na gari aina ya Coaster lililopita likiwa na namba ya  IT katika mpaka wa Tunduma Februari 28 na kurudi likiwa na namba T 159 DMX.

Gari hilo alisema ni la mwanajeshi mmoja wa Dar es salaam, lilikamatwa Machi 3 mwaka huu na askari polisi katika eneo la Kijiji cha Muyovizi kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi kwenye barabara ya Mbeya Tunduma. Gari hilo mmiliki wake endapo atalikomboa atalazimika kulipa kiasi cha shingili milioni 28.

Katika hatua nyingine TRA imeweza kukamata mafuta aina ya Diesel kiasi cha lita 6,400 ambayo yalikuwa na vibali kwamba yanatoka Zambia kwenda Kigali, Rwanda lakini baadae yakaingizwa nchini kinyemela na kinyume cha sheria.

Meneja wa TRA mkoani Songwe Paul Walalaze, alisema licha ya kukamata mafuta hayo ya Diesel, pia wamekamata mafuta ya kula aina ya Kimbo kiasi cha madumu 15 ambayo yalipita katika mpaka wa Tunduma kwamba yanakwenda DR Congo lakini yakawa yamehifadhiwa kwenye moja ya maduka hapo mpakani.

Meneja huyo alisema mbali na kuanzisha doria hizo aliwataka wananchi hasa raia wema kutoa ushirikiano kwa TRA pindi wanapoona matukio kama hayo ili waweze kukamatwa.


No comments