Breaking News

UTOAJI TAARIFA NI KIKWAZO KWA KASI YA MAENDELEO NCHINI.


IMEELEZWA kuwa upatikanaji wa taarifa kuanzia ngazi ya Halmashauri, Mikoa bado ni changamoto kubwa hali ambayo inasababisha kurudisha nyuma kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini.
Hayo yamebainishwa leo na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dorothy Gwajima kwenye kikao kazi cha Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage Jijini Dodoma.
Dorothy amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa  na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wote nchini kuhakikisha kila idara   inawasilisha  taarifa sahihi na kwa wakati  ili, kuweza kuimarisha tathmini ya kasi ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali na kubaini mafanikio na changamoto na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.
“Taarifa ya mpango wa malipo kwa ufanisi (RBF) umechukua miezi 3 na cha kushangaza, mara baada ya kutoa notisi ya saa 72 kuwa, Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri wakabidhi majukumu ya uongozi iwapo watashindwa kuwasilisha na warudi kwenye kazi zao za kitaaluma, wote waliwasilisha kabla hata ya muda huo, kitu kinachodhihirisha kuwa, kuna uzembe katika uwajibikaji." amesema Dorothy
Amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanawasimamia wataalamu walio chini yao kuwajibika kikamilifu na kwa wakati.
Kuhusu utoaji wa taarifa za ujenzi waHospitali mpya  (67) za Halmashauri za Wilaya amesema kuwa, Waganga Wakuu wa Mikoa waliagizwa kuwasilisha taarifa hizo wiki mbili zilizopita lakini, mpaka sasa ni mikoa sita tu ndiyo imetoa taarifa.
Aidha, mikoa mingine iliyowasilisha, taarifa hizo hazijakamilika hivyo, amewaagiza Waganga Wakuu Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanawajibika kuwasaidia kikamilifu viongozi wao.
“kuwe na mpango wa ujenzi wa vituo unaoonesha nini kinafanyika kila wiki na taarifa ya utekelezaji iwasilishwe kila wiki Wizarani” amesema Dorothy


Aidha, Dorothy amesema, kila Katibu Tawala wa Mkoa husika na Mkurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ahakikishe  vituo vya afya vyote  vilivyokamilika vinawezeshwa kuanza kutoa huduma kwa kutumia rasilimali za ndani ya halmashauri badala ya kusubiri kila kitu toka Serikali kuu.
 Amesema, inawezekana kuanza kutoa baadhi ya huduma kwa kutumia rasilimali toka halmashauri husika kama ilivyofanyika kwenye halmashauri zingine. Aidha, wale wanaoendelea na ujenzi au ukarabati wasimamie wakamilishe.
Dorothy amesisitiza kuwa kila Halmashauri ihakikishe inatumia mifumo ya kielektoniki katika ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vyote vya afya ili kuepusha mianya ya upotevu wa fedha za Serikali.
Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watoa huduma kutafuta visingizio vya kutotumia mifumo hii hivyo wajue kuwa, matumizi ya mifumo hii ni lazima na haikwepeki
Kuhusu fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi za maendeleo Dorothy amesema, zitumike kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo na kinyume na hapo, hatua kali zitachukuliwa.
Pia amewataka Makatibu Tawala na Wakurugenzi kuwasimamia wataalamu wa afya kuwa wabunifu katika  kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa kuimarisha utoaji wa huduma za tiba kwa mkoba kwa kualika wataalamu ambao, wanakosekana katika maeneo husika ili, kuongeza kasi ya kusogeza huduma kwa wananchi na kuwapunguzia adha ya kusafiri mbali kufuata huduma hizo.
“Unaposogeza huduma za Afya karibu na wananchi kwa njia ya mkoba, hata uwezo wa wananchi kuchangia unakuwa mkubwa maana, unawapunguzia gharama ya nauli na gharama za maisha mbali na makazi yao” Anasema Dorothy.
Aidha ametoa wito kwa viongozi hao kutochukua  hatua za kinidhamu kwa watumishi bila kufuata taratibu za kiutumishi kwa maana, unapochukua hatua kinyume na taratibu ukumbuke kuwa, hilo ni kosa kwa mujibu wa miongozo na taratibu za utumishi wa umma .

No comments