Breaking News

BILION5.7, WATUMISHI 119 KUIMARISHA HUDUMA YA AFYA NJOMBE.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameeleza kuwa wizara yake imeandaa watumishi 119 watakaotoa huduma katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe na kwamba katika awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo, Serikali imetenga shilingi Bilioni 5.7 kwa ajili ya kuendeleza miundombinu yake.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo mkoani Njombe mara baada ya Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli kufungua hospitali hiyo ikiwa ni moja kati ya mambo mengi yaliyofanywa na Dkt. Magufuli akiwa katika Ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Ameongeza kuwa Wizara ya Afyaimejipanga kuhakikisha Hospitali ya Mkoa wa Njombe pamoja na hospitali zote za rufaa nchini zinakuwa na Madaktari Bingwa wa kada muhimu za kipaumbele na inatumia shilingi Bilioni 2.5 kila mwaka kusomesha Madaktari Bingwa ambao wana mkataba wa kufanya kazi katika hospitali za Serikali kwa miaka mitatu baada ya masomo yao.

Kuhusu Hospitali hiyo, Dkt. Magufuli ameagiza ianze kutumika ndani ya miezi miwili na amewapongeza wananchi Njombe kwa kupata hospitali hiyo.

Kesho tarehe 11 Aprili, 2019 Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli,  atamaliza ziara yake  Mkoani Njombe kwa kufungua barabara ya Mafinga – Igawa na kuzungumza na wananchi katika mji wa Makambako.

Hospitali ya Mkoa wa Njombe imejengwa katika eneo la Wikichi Mjini Njombe na awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo yaliyohusisha jengo la huduma za wagonjwa (OPD) imegharimu shilingi Bilioni 3 na Milioni 629 fedha zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

No comments