Breaking News

DAWASA YAANDIKA HISTORIA MPYA BONYOKWA


Na Tunu Nassor

KWA MARA YA KWANZA wakazi wa kata ya Bonyokwa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam leo wameanza kupata huduma ya Maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi wa kupeleka maji katani hapo.

Akizungumza katika ufunguzi wa mradi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam  (Dawasa) Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema zaidi ya wateja 1,500 wameunganishiwa huduma hiyo.

Alisema mradi huo umetekelezwa kwa kulaza mabomba kilomita tatu na kusambazwa na wananchi.

"Mradi utawahudumia wakazi 30,00 wa kata hii ambapo tayari mabomba ya inchi 8,4,3, na 2 yamelazwa," amesema Luhemeja.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa maeneo hayo hao wameshangilia kupata huduma hiyo kutokana na kutokuwa na maji kwa miaka mingi.

Mmoja wa wakazi hao, Saumu Ally amesema kupatikana kwa huduma hiyo kutawasaidia kufanya shughuli zingine za maendeleo baada ya kuwa wanatumia muda mwingi kutafuta maji. 

"Tunashukuru sana sasa hata tukioga tutapendeza maana tumekuwa tukinywa maji ya visima ambayo tuliyanunua kwa bei kubwa," amesema Saumu.

Naye Athanas  Masaka amesema ni historia  kwa Bonyokwa kushuhudia maji ya Bomba yakitoka katika eneo hilo.

"Hii ni historia imeandikwa maana tangu tumeanza kuishi katika eneo hili  hatujawahi kuona maji yanatoka bombani...tunamshukuru Rais John Magufuli," amesema Masaka.


No comments