Breaking News

MAGUFULI AANZA ZIARA YA SIKU 6 RUVUMA.


Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo tarehe 04 Aprili, 2019 ameanza ziara ya kikazi ya siku 6 katika Mkoa wa Ruvuma akitokea Mkoani Mtwara.

Akiwa njiani kutoka Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara kwenda Tunduru Mkoani Ruvuma, Magufuli amesalimiana na wananchi wa Vijiji vya Michiga, Nakapanya na Namiungo ambako amewahakikishia kuwa Serikali itanunua korosho zote za wakulima, zikiwemo zilizokusanywa kwa mtindo wa Kangomba baada ya waliofanya makosa hayo kukiri na kuomba radhi.

Katika Kijiji cha Nakapanya, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Ramo Makani ametoa maelezo juu ya tatizo la maji linalokikabili kijiji hicho na vijiji vingine vya Wilaya ya Tunduru na Magufuli ametoa maagizo kwa wataalamu na viongozi kuangalia namna ya kuvuna maji ya mvua kwa kutumia mabwawa makubwa badala ya kuendelea kutegemea kupata maji kutoka mbali.

Magufuli amelazimika kutembelea jengo la soko la Kijiji cha Nakapanya baada ya wananchi kulalamikia kuwa Mahakama imewazuia kutumia jengo hilo kutokana na kujengwa jirani na jengo la Mahakama ya Mwanzo na baada ya kujionea hali halisi ameagiza jengo hilo la soko lianze kutumika kuanzia kesho tarehe 05 Aprili, 2019 na ameagiza viongozi wa Wilaya ya Tunduru wahakikishe mazingira ya jengo hilo yanaboreshwa.

Kuhusu jengo la Mahakama ya Mwanzo lililopo jirani na soko hilo na ambalo ni chakavu, Magufuli ametoa shilingi Milioni 10 kisha kuendesha harambee iliyofanikisha kupatikana jumla ya shilingi Milioni 22 za kujengea jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo ya Nakapanya na ameelekeza kuwa jengo hilo lijengwe mahali pengine.

Dkt. Magufuli pia amezungumza na wananchi wa Kijiji cha Namiungo ambapo Diwani wa Kata ya Namiungo Salima Limbalambala ameomba Serikali iwasaidie wananchi hao kupata Kituo cha Afya, na Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Suleimani Jafo kutenga shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Namiungo.

Kesho Dkt. Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Ruvuma ambapo atafungua barabara ya Tunduru – Matemanga – Kilimasera – Namtumbo na atazindua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Wilayani Namtumbo.
No comments