Breaking News

MAGUFULI APIGILIA MSUMARI MSIMAMO WAKE KUHUSU WAFUNGWA


Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli amelitaka Jeshi la Magereza kuwahamisha wafungwa waliopo katika magereza yasiyokuwa na shughuli za uzalishaji na kuwapeleka katika magereza yenye shughuli za uzalishaji mali likiwemo gereza la Kitai ambalo lina wafungwa 233 ikilinganishwa na uwezo wake wa kuchukua wafungwa 370 ilihali baadhi ya Mikoa hapa nchini ina idadi kubwa ya wafungwa kupita uwezo wake na hawafanyi kazi zozote za uzalishaji mali.

Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo tarehe 08 Aprili, 2019 katika ziara yake Mkoani Ruvuma wakati alipotembelea shamba la Gereza la Kitai lililopo Wilayani Mbinga.

Akizungumza na Askari, Maafisa wa Magereza na wananchi wa Kitai, Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuitikia wito wake wa kuhakikisha linawatumia wafungwa ipasavyo katika uzalishaji na ametoa matrekta 2 kwa Gereza la Kitai ili yasaidie kupanua mashamba ya mazao katika eneo la ekari zaidi ya 7,000 zilizopo katika gereza hilo.

“Nimeambiwa katika Magereza yetu wapo wafungwa kama 18,000 na Mahabusu 19,000 nataka wafungwa hawa watumike kuzalisha mali badala ya kukaa Magerezani halafu Serikali iwe inatoa fedha kwa ajili ya kuwalisha, Magereza mengine yaige mfano wa Gereza la Kitai.” Amesema  Dkt. magufuli na kuongeza kuwa

“Nataka wafungwa watumike kwelikweli na kama kuna suala la kisheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ipeleke mapendekezo ya mabadiliko ya sheria Bungeni” amesema Dkt. Magufuli.

Dkt. Magufuli amelielekeza Jeshi la Magereza liwatumie wafungwa kujenga makazi ya askari pamoja na miundombinu ya huduma za kijamii katika maeneo hayo.

Aidha Dkt. Magufuli ametembelea shamba la mahindi lenye ukubwa wa ekari 650 linalolimwa kwa kutumia wafungwa wa gereza hilo na ambalo linatarajiwa kuzalisha tani 780 za mahindi katika msimu huu.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza Faustine Kasike amemueleza Dkt. Magufuli kuwa mahindi yatakayovunwa katika shamba hilo yatatumika kulisha Magereza ya Mikoa 3 (Ruvuma, Lindi na Mtwara) yenye wafungwa 2,000.

Pia ameeleza kuwa kupitia mkakati wake wa uzalishaji wa mazao katika Magereza 10 Jeshi hilo linatarajia kuvuna tani 15,135.75 za mahindi, mpunga na maharage msimu huu baada ya kupanua mashamba yanayolimwa kutoka ekari 1,950 hadi kufikia ekari 5,395.

Dkt. Magufuli aliyeongozana na Mkewe  Mama Janeth Magufuli kesho tarehe 09 Aprili, 2019 atamaliza ziara yake Mkoani Ruvuma kwa kuzindua Kituo cha Afya cha Madaba Wilayani Songea na ataanza ziara yake ya siku 3 katika Mkoa wa Njombe kwa kufungua kiwanda cha chai cha Unilever kilichopo Lwangu, Mjini Njombe.No comments