Breaking News

MAGUFULI KUIMULIKA RUVUMA


RAIS wa Tanzania, Dkt. John Magufuli Jana tarehe 06 Aprili, 2019 amezindua mradi wa njia ya umeme ya msongo wa KV 220 kutoka Makambako hadi Songea na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha mabasi na barabara za lami katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.

Sherehe za uzinduzi wa mradi wa njia ya umeme zimefanyika katika kituo cha kupoza na kusambaza umeme kilichopo Unangwa Mjini Songea na zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjöberg, Mawaziri, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa huo Godfrey Zambi.

Mradi huo umehusisha ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 245, upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Makambako, ujenzi wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme vya Madaba na Songea na usambazaji wa umeme wa msongo wa kilovoti 33 zenye urefu wa kilometa 900 zilizounganishwa kwa wateja 22,700 katika Wilaya za Njombe, Ludewa, Mji wa Makambako, Songea Vijijini, Songea Mjini, Namtumbo na Mbinga.

Ujenzi wa mradi huo umegharimu shilingi Bilioni 216 na Milioni 941, fedha ambazo zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Sweden na Serikali ya Tanzania, na baada ya kukamilika kwake Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezima mitambo ya kuzalisha umeme kwa mafuta katika vituo 5 na hivyo kuokoa shilingi Bilioni 9.8 kwa mwaka.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amemshukuru Dkt. Magufuli kwa kutilia mkazo wa kuhakikisha mradi huo unaanza kutekelezwa mara alipoingia madarakani na kwamba hivi sasa Mkoa wa Ruvuma wenye mahitaji ya megawati 12 za umeme unapata megawati 48 zitakazowezesha uanzishaji wa viwanda na vijiji vyote kupatiwa umeme ifikapo mwaka 2012.

Kalemani amebainisha kuwa tangu Rais Magufuli aingie madarakani idadi ya vijiji vilivyopatiwa umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijiji (REA) imeongezeka kutoka 2,018 hadi kufikia 6,464 (sawa na ongezeko la asilimia 214).

Balozi wa Sweden hapa nchini Andrers Sjöberg ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa uhusiano na ushirikiano mzuri na Sweden ambao umesaidia kutekelezwa kwa miradi mingi ya maji tangu miaka ya 90 na baadaye kufuatiwa na miradi ya kupeleka umeme vijijini ambako wananchi wengi wamenufaika hususani wanawake.

Kwa upande wake, Dkt. Magufuli ameishukuru nchi ya Sweden kupitia SIDA kwa ufadhili wake katika mradi huo na ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo pamoja na mradi mkubwa ambao Tanzania inaujenga hivi sasa wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji utasaidia kuinua uchumi kupitia viwanda na pia utasaidia kuokoa mazingira kwa kuwa wananchi watatumia umeme badala ya kuni na mkaa ambao unapatikana kwa kukata miti.

“Takwimu zinaonesha ekari 400,000 za miti huvunwa kila mwaka kwa lengo kupata kuni na mkaa wa kupikia, hii yote inasababishwa na umeme kidogo na wa gharama kubwa tulionao, tunapotekeleza miradi hii tutaokoa uharibifu huu wa mazingira, kwa hiyo nakuomba Balozi ukawaeleze Mabalozi wenzako kuwa Tanzania tunapotekeleza miradi hii tunataka kuimarisha uchumi wetu na pia kuokoa misitu yetu” amesema Magufuli.

Ametoa wito kwa Sweden na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa nishati ya umeme kupitia vyanzo mbalimbali vikiwemo gesi, makaa ya mawe, urani, upepo na joto ardhi, na pia amewataka Watanzania waongeze juhudi katika utunzaji wa mazingira.


No comments