Breaking News

MGOGORO MWINGINE MKUBWA WA ARDHI WAMALIZWA DODOMA.


Na Furaha John,  Dodoma

UONGOZI wa jiji la Dodoma kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa huo wamefanikiwa kutatua mgogoro wa ardhi ambao umedumu takribani miaka 14 huku wakiwataka wananchi waliochukua viwanja mara mbili kurejesha

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Dodoma Binilith Mahenge  kwenye mkutano wa hadhara uliolenga kumaliza changamoto ya ardhi iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa eneo hilo.

Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa wa  Dodoma Dk. Binilith Mahenge amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi kuanza kuanza ugawaji wa viwanja vilivyotengwa kama mbadala kwa wananchi wa eneo la mji mtaa wa mtakuja mwema ambao wamekosa viwanja haraka iwezekanavyo.

Dk. Mahenge amesema, kwa sasa changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu imekwisha pata ufumbuzi na anaamini uongozi wa jiji umekwishaandaa viwanja mbadala kwa ajili ya kuwapatia viwanja wananchi ambao walikosa katika eneo hilo la Mjimwema.

Amefafanua kuwa, wakati walipounda kamati kwa iliyokuwa Mamlaka ya ustawishaji wa mji Mkuu Dodoma (CDA),iligundua baadhi ya wananchi waliopewa maeneo sehemu nyingine baada ya kuondolewa katika eneo la makaburi walilokuwa wamevamia wamerudi  kwenye eneo hilo la awali na kuchukuwa tena viwanja vingine vilivyogawiwa kwa wananchi wa eneo hilo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema watakabidhi kwa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) orodha ya wananchi wote ambao wananchi wamechukua viwanja mara mbili ili wachukuliwe hatua za kisheria kwani huo ni udanganyifu na utapeli.

"Majina haya ya waliochukua viwanja mara mbili tutayabandika kwenye ofisi ya serikali ya mtaa na tutayapeleka TAKUKURU ili wachukuliwe hatua za kisheria kwasababu kuchukua viwanja mara mbili na ukiwa umeshapewa ni udanganyifu ,"amesema.

Pia amewataka wananchi ambao wamechukua barua za viwanja kukamilisha taratibu zote ikiwemo malipo ili waweze kupatiwa hati miliki na kwa upande wa wananchi ambao hawajachukua barua wafike ofisi ya serikali ya kijiji kuchukua.

Naye Mkurugenzi  Kunambi amesema tayari wananchi wote ambao hawajapata viwanja wameshatengewa viwanja mbadala katika eneo la Kikombo lililopo jijini hapa, akisisitiza kwamba ni eneo rafiki kwa watu wote.

Kunambi amesema, yeye pamoja na watendaji wake kazi yao ni kupokea  maelekezo na kuyaweka katika utekelezaji na tayari wameshatenga viwanja hivyo katika eneo la hilo hivyo wananchi walipokee kwa mikono miwili wasione kama wameonewa.

“Wananchi wanaweza wakahisi ni eneo baya,  ra hasha!, Kikombo kuna watu wanaishi  na ni watanzania na eneo hilo litakuwa eneo jipya na kutakuwa mji uliopangwa kuliko miji yote kwasababu upimaji umeshafanyika na kutapelekwa miundombinu ya maji,barabara na umeme,”amesisitiza.


No comments