Breaking News

MWALIMU AILILIA SERIKALI UHABA WA MADAWATI.

Na EZEKIEL MTONYOLE, CHAMWINO.

SERIKALI imeombwa kutatua kati changamoto zinazoikabili shule ya msingi Igamba, iliyopo kata ya Dabalo wilaya ya Chamwino, Mkoani Dodoma ambapo zaidi ya wanafunzi mia moja wanasoma wakiwa wamekaa chini kwa kukosa madawati.

Wakati wanafunzi wa darasa la awali na darasa la pili wakiwa wanasomea nje kwa kukosa vyumba vya madarasa, huku shule hiyo ikiwa na wanafunzi mia saba hamsini na sita(756) na ikiwa na vyumba vya madarasa sita(6) na madawati tisini na tatu(93) tu.

Hayo yamebainishwa  na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Maselino Mtwale,  wakati wa ziara ya kamati ya utekelezaji ya jumuiya ya umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi UVCCM, Mkoa wa Dodoma wakati walipotembelea kata hiyo wakiambatana na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Dodoma anayewakilisha vijana Mariam Ditopile.

Mtwale amesema kutokana na changamoto zinazoikabili shule hiyo wanafunzi mia moja ishirini na tisa wanasoma wakiwa wamekaa chini kutokana na uhaba wa madawati, huku wanafunzi wa darasa la awali na la pili wakilazimika kusomea nje ya madarasa kwa kukosa vyumba vya madarasa.

“Shule hii ina changamoto nyingi sana kubwa kabisa ni uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati shule yetu ina wanafunzi mia saba hamsini na sita wakati tuna vyumba vya madarasa sita(6) tu, na madawati yakiwa tisini na tatu(93) kwa hiyo darasa la awali na la pili wanasomea nje ya madarasa, wakati la tano na sita wanasoma wakiwa wamekaa chini ”, amesema Mtwale.

Aidha amebainisha kuwa kutokana na changamoto hizo madarasa ya awali, la pili, tano na sita wanakose madawati, kutokana na hilo darasa la kwanza kwa sababu wanajifunza kuandika, darasa la nne na la saba wanafanya mitihani hiyo ndio waliopewa kipaombele kukaa kwenye madawati kwa sababu wanamitihani  ili wasome wakiwa wametulia.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Dabalo Elisha Matewa amesema kutokana na changamoto zilizopo katika shule hiyo yeye pamoja na wananchi waliamua kujenga darasa moja ambalo tayari linatumika, na sasa wako kwenye harakati za ujenzi wa vyumba vingine viwili.

Mbali na hilo diwani pia amemuomba mbunge na mwenyekiti wa Uvccm mkoa wa Dodoma Billy Chidabwa, kufikisha kero ya changamoto ya afya ambapo kuna haja ya kupandisha hadhi kuwa kituo cha afya kwa sababu zahanati hiyo inahudumia watu wengi na kukosa uwezo hivyo lazima kipandishwe hadhi kuwa kituo cha afya ili kiweze kukidhi mahitaji.

Kutokana na changamoto hizo Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Dodoma anayewakilisha vijana Mariam Ditopile, ameahidi kufikisha changamoto hizo bungeni, na akaunga mkono juhudi za wananchi kwa kuwachangia mifuko ishirini ya saruji kwa ajiri ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Nae mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi Uvccm, mkoa wa Dodoma Billy Chidabwa, amesema ili kuhakikisha wanafunzi wanaondokana na changamoto hizo aliahidi, umoja wa vijana wilaya na mkoa wataweka kambi katika eneo hilo na kujenga chumba cha darasa kwa nguvu zao wenyewe.

Amesema yeye kama mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa atahakikisha anafikisha kero hizo katika ngazi za juu za chama ili ziweze kutatuliwa kwa haraka, pia alimpongeza diwani wa kata hiyo na wananchi, kwa kazi kubwa wanayofanya katika kata hiyo na kuahidi kuwa nao bega kwa bega.

Katika ziara hiyo kamati ya utekelezaji ya umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi Uvccm mkoa walitembelea shule ya msingi Igamba, mradi wa maji katika kijiji cha Dabalo, ujenzi wa kituo cha polisi na shule ya sekondari Dabalo.


No comments