Breaking News

NEC YAANZA MAANDALIZI YA UCHAGUZI 2020.


Na Furaha John,Dodoma

SERIKALI imesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na uhakiki wa vtuo vya uandikishwaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akiwasilisha Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019,2020.

Amesema, serikali itahakikisha uwepo wa usalama na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi na kwamba hadi sasa kanuni za uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura zimeandaliwa na kutangazwa kwenye gazeti la serikali namba 792 na 793 ya Desemba 28 mwaka jana.

Majaliwa amesema kuwa vituo vya kuandikisha wapiga kura nao umekamilika ambao kwa upande wa Tanzania Bara vituo vimeongezeka kutoka 36,549 vilivyokuwepo mwaka 2015 hadi kufikia vituo 37, 407 mwaka jana, sawa na ongezeko la vituo 858.

Kwa upande wa Zanzibar amebainisha vituo viomeongezeka kutoka 380 vya mwaka 2015 hadi kufikia vituo 407 kwa mwaka jana ambapo alitoa wito kwa wananchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha mara zoezi litakapoanza.

Katika hatuna nyingine serikali imekamilisha maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zitakazotumika kusimamia uchaguzi huo ambao sasa utafanyika Oktoba mwaka huu.

Uchaguzi huo wa sita kufanyika nchini tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, katika Halmashauri zote 185 serikali imeshahakiki maeneo ya utawala ambayo yatashiriki kwenye uchaguzi huo, Serikali imeshakamilisha uhakiki wa maeneo ya utawala ambayo yatashiriki kwenye uchaguzi huo kwenye Halmashauri zote 185.

Amesema lengo la uhakikihuo ni kujiridhisha na usahihi wa maeneo hayo kwa idadi na majina ili kufanikisha maandalizi ya bajeti na mahitaji mengine muhimu ya uchaguzi huo," amefafanua.

Waziri mkuu ametoa wito kwa wadau na wananchi kujiandikisha na kujitokeza kwa wingi kwenye upigaji kura ili waweze kutumia haki yao kidemokrasia ya kuchagua au kuchaguliwa.

Waziri mkuu ameeleza kuwa hali ya kisiasa na demokrasia imeendelea kuimarika nchini kwani katika mwaka 2018/19 zilifanyika chaguzi ndogo za wabunge katika majimbo 10 na madiwani katika kata 231 kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Ameyataja majimbo yaliyoshiriki chaguzi hizo ni Buyungu, Korogwe, Monduli, Ukonga, Liwale, Serengeti, Serengeti, Simanjiro, Ukerewe, Babati Mjini na Temeke.

"Katika chaguzi hizo, wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walishinda majimbo yote na kata 230 huku Chadema wakishinda kata moja. Navipongeza vyama vyote vilivyoshiriki chaguzi hizo na kipekee, naipongeza CCM kwa ushindi mkubwa uliopata katika chaguzi hizo," Waziri mkuu, amesema.

Kuhusu Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Majaliwa amesema ofisi hiyo imeendelea kusimamia na kukuza mfumo wa demokrasia wa vyama vingi vya siasa ili kudumisha amani, utulivu na mshikamano uliopo nchini.

Amesema katika kutekeleza jukumu hilo, Sheria ya Vyama Vya Siasa namba tano ya mwaka 1992 Sura ya 58 imefanyiwa marekebisho kuondoa mapungufu yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji.

Kuhusu mapambano dhidi ya madawa ya kulevya ameeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye mapambano hayo na kusema kuwa serikali imeendelea kubaini mtandao wa wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

Amefafanua kuwa hadi Januari mwaka huu, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola imefanikiwa kukamata watuhumiwa 11,617 wakiwa na dawa hizo aina mbalimbali kama Heroine, Cocaine, bangi na mirugi.

Vilevile, ekari zaidi ya 59 za mashamba ya bangi ziliteetezwa nchini katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza na Dodoma huku watumiaji wapatao 6,500 wakiendelea kupatiwa huduma za tiba ya methadone katika vituo mbalimbali vilivyopo nchini.


No comments