Breaking News

SIMBA, YANGA ZACHONGANISHWA NA SEVILLA..


Na Furaha john, Dodoma.

KAMPUNI ya SportPesa itaileta  Tanzania timu ya Sevilla ya Nchini Hispania kucheza dhidi ya mmoja kati ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari bungeni jijini Dodoma jana, Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya SportPesa, Abbas Tarimba, amesema kampuni yao kwa kushirikiana na uongozi wa La Liga, wamekubalina kuileta timu hiyo nchini.

Amesema kuwa awali walipanga kuwe na mechi kati ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga ili mshindi wa mechi hiyo ndiyo acheze dhidi ya Sevilla, lakini imeshindikana kutokana na kile alichoeleza kuwa ugumu wa ratiba unaozikabili timu hizo kwa sasa.

Tarimba amesema mechi kati ya Sevilla na timu ya Tanzania watakayoichagua, itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Mei 23, mwaka huu.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangalla, ameipongeza SportPesa kwa kuamua kuwaleta Sevilla Tanzania.

Amesema wizara yake itautumia ujio wa timu hiyo kama fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini na kwamba timu hiyo itakapowasili nchini, wataipeleka kwenye hifadhi moja au mbili kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii nchini.

"Tunaamini kwa kufanya hivi tutaongeza idadi ya watalii. Tutaangalia pia uwezekano wa kuwapeleka Zanzibar kutembelea fukwe," amesema.

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ameipongeza SportPesa kwa kufanikisha ujio wa timu hiyo na kueleza kuwa kampuni ni mdau mkubwa wa michezo nchini.

Amesema ujio wa Sevilla nchini utaitangaza Tanzania duniani na hivyo kusaidia kuwatangaza hata wachezaji wa Tanzania watakaocheza dhidi ya timu hiyo Mei 23.

"Hivi sasa, Tanzania imeanza kuonesha mafanikio makubwa katika mchezo wa soka na michezo mbalimbali na kutia imani kwa wananchi kwamba pale tunapotaka kufika, itawekana," alisema.

Naye,Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF)Wilfred Kidau amesema ujio wa Sevilla utasaidia kukuza Soka nchini pamoja na kuwatangaza wachezaji wa Tanzania.

Sevilla kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) ikiwa na pointi 52 baada ya mechi 32.


No comments