Breaking News

WAAJIRI WA UMMA WATAKIWA KUWAJENGEA UWEZO WATUMISHI WAO.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amewataka Waajiri katika Taasisi za Umma nchini kuwawezesha Watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika Chuo cha Utumishi wa Umma ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Mkuchika amesema leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Amesema watumishi wengi hawajui taratibu za kiutumishi hivyo kukosa uwezo wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Amesisitiza kuwa, pamoja na majukumu mengine, Chuo cha Utumishi wa Umma kina jukumu la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo, hivyo ni vema watumishi hao wakapata mafunzo katika chuo hicho.

Ameongeza kuwa, kuanzia sasa atafanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha waajiri wote wanawapeleka watumishi wa umma wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza katika Chuo hicho kupata mafunzo stahiki.

Mkuchika ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya kiasi cha shilingi 683, 529,221,617 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Taasisi zilizo chini yake.No comments