Breaking News

WAHITIMU WA MAFUNZO YA UONGOZI WATAKIWA KUTUMIA UJUZI WALIOUPATA KUONGEZA UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI

NAIBU WAZIRI, Ofisi ya Rais, Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka wahitimu wa mafunzo ya Stashahada ya Juu ya Masuala ya Uongozi kutumia vizuri ujuzi walioupata ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na hatimaye kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Dkt. Mary amesema hayo, alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wahitimu wa Stashahada ya Juu ya Masuala ya Uongozi iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mary amesema anatarajia wahitimu hao kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii kwa kusimamia vema masuala ya utawala bora, haki za binadamu, utawala wa sheria huku wakionyesha uzalendo na ufanisi wa hali ya juu  katika shughuli zao za kila siku.

“Nina imani kuwa mafunzo haya yamewabadilisha kifikra na kimtazamo katika masuala yote yanayohusu uongozi na mmekuwa na uelewa mpana utakaobadili utendaji kazi wenu kutokana na programu hii iliyofundishwa na wataalamu wabobezi wa hapa nchini na nje ya nchi,” Dkt. Mary amesisitiza.

Dkt. Mary ameongeza kuwa, serikali inategemea kuona kwa vitendo kile walichojifunza darasani kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia uzalendo na uadilifu mkubwa na kuwa na uongozi wa kimkakati kwa kusimamia vizuri rasilimaliwatu na rasilimali fedha.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Neema Mwakalyelye ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Dkt. Mary na kusema kuwa watakuwa viongozi bora wanaopenda mabadiliko chanya ili kutimiza dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu watumishi kuhudhuria mafunzo hayo na Serikali ya Finland kwa kudhamini na hatimaye kufanikisha uwepo wa mafunzo hayo nchini Tanzania.

Jumla ya wahitimu 33 wakimemo baadhi ya viongozi wastaafu wa serikali na viongozi waandamizi serikalini walitunukiwa vyeti vya Stashada ya Juu ya Masuala ya Uongozi yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Chuo cha AALTO cha nchini Finland.

No comments