Breaking News

WANANCHI BAHI WAOMBA KUBORESHEWA BARABARA.

Tafadhali picha haihusiani na eneo la tukio.

Na EZEKIEL NASHON, BAHI.

WAKAZI wa kijiji cha Kigwe kata ya Kigwe, Wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma, wameiomba serikali kuwakarabatia barabara inayoingia katika kata hiyo kwa sababu imekuwa kero kwa watumiaji hasa kwa akina mama wanaokwenda hospitali.

Wameyabainisha hayo wakati wa ziara ya kamati ya utekelezaji ya jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi Uvccm, Mkoa wa Dodoma walipotembelea katika kata hiyo wakiongozana na Mbunge wa viti maalumu Mariam Ditopile.

Ikiwa ni sehemu ya kuangalia utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwa wananchi, sambamba na kuangalia ushiriki wa vijana katika shughuri za maendeleo katika kata hiyo.

Wananchi  hao wamesema kwa mda sasa wamekuwa wakiteseka kutokana na ubovu wa barabara licha ya kata hiyo kuingiza mapato mengi kupitia mnada lakini barabara hiyo haitengenezwi.

“Kero kubwa inayotusumbua katika kata hii ni ubovu wa barabara barabara imekuwa mbovu sana kata yetu hii kupitia mnada ule tunaingiza mapato mengi lakini barabara hazitengenezwi kwa kweli ni kero kubwa sana serikali itusaidie” amesema Magidarena.

Vilevile wamebainisha kuwa hawapati huduma ya maji safi na salama wakati kuna mradi wa kisima kirefu chenye uwezo na maji mengi lakini imekuwa kinyume na matarajio kwa wananchi hao.

“Niombe serikali yetu itusaidie kwenye kero ya maji kwani tunateseka sana hatuna huduma ya maji safi na salama, katika kata hii tuna shule ya kidato cha tano na sita wanaoishi katika mabweni kuna kipindi  hadi walipata gonjwa la kipindu pindu, kero ya maji imekuwa kubwa sana” amesema Laurance.

Aidha wameshangazwa na kutokana na katika kijiji hicho kuna mradi wa kisima chenye maji mengi lakini wananchi hawapati huduma ya maji safi na salama, maji ambayo yangefika hadi katika makazi ya watu.

Akijibu kero hizo kwa wananchi afisa mtendaji wa kata hiyo Mwasiti Magilla, amekili kuwepo kwa changamoto hizo,  amesema amepata uteuzi hivi karibuni hivyo hajapokea ripoti ya mtangulizi wake, hivyo atayafanyia kazi kujua changamoto ni nini.

“Changamoto kweli ipo lakini mimi nimeteuliwa hivi karibuni bado sijafuatilia tatizo ni nini, kwa sababu kesho tuna kikao na watendaji tutajaribu kupata ripoti na sababu zinazosababisha, nikuahidi mwenyekiti nitafuatilia ili nijue changamoto ni nini” alisema Mwasiti.

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu anayewakilisha   kundi la vijana, aliyeambatana na msafara wa kamati ya Uvccm, Mariam Ditopile amemtaka afisa mtendaji wa kata kufuatilia kwa ukaribu kero hizo na kumpa mrejesho ili alifikishe katika ngazi husika.

Pia katika kata hiyo, Mbunge wa viti maalumu Mariam Ditopile,   amesema wamekuja ili kuangalia namna ilani ya chama inavyotekelezwa, na kama mikakati wanayoipanga katika mgazi za juu je utekelezaji  unafika hadi ngazi za chini? Mbunge katika kuunga  mkono juhudi za wananchi.

Ametoa laki moja(100,000) kwa ajili ya kikundi cha akina mama wa UWT kwa ajili ya kununulia vifaa vya ujasiliamali ili waweze kujikwamua kiuchumi, pia ametoa jezi seti moja kwa ajili ya vijana kushiliki katika michezo na ameahidi kuanzisha ligi kubwa katika kata ya Bahi na kutoa zawadi nono kwa mshindi.

 Vilevile amechangia mifuko kumi(10) ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyoo ili kuunga mkono ujenzi wa shule ya msingi Lioni ambayo wananchi wameijenga kwa nguvu zao wenyewe ikiwa na madarasa mawili na ofisi moja.

Nae mkuu wa msafara Wenslaus Mazanda, aliyekuwa akimuwakilisha mwenyekiti Uvccm Mkoa Billy Chidabwa, amesisitiza watu kulima kwa wingi kwani soko la mazao yao linakwenda kuwa kubwa kutokana na serikali kuhamia makao Dodoma hivyo kutakuwa na soko kubwa kutokana na wageni wengi kuhamia Dodoma.

Pia amegawa bendera sita (6) kwa kila kata alizozipitia, zilizotolewa na mwenyekiti wa Uvccm Mkoa, Billy Chidabwa,  kwa wenyeviti wa mashina ili wakazipeperushe katika  matawi yao, pia alipokea wanachama 6 ktika kata ya Bahi waliojiunga na ccm wakitokea vyama vya upinzani walioamua kurudi ccm.

Vilevile  amesisitiza katika uchaguzi ujao watu wajitikeze kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama serikali kwani nafasi zipo kwa kila anayejiweza, ametaka pia wachague viongozi wanaotokana na ccm ili Rais akija kusiwe na wapinga maendeleo katika mkoa wa Dodoma.

Katika ziara hiyo kamati ya utekelezaji ya Uvccm imetembelea ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Bahi, ambayo imetengewa bilioni 1.5, na vikundi mbalimbali vya ujasiliamali ambavyo vinanufanika na mikopo ya halmashauri.

No comments