Breaking News

WAWEKEZAJI WALIOBINAFSISHIWA VIWANDA KUKOPEA MABILIONI KUKIONA CHA MOTO.


Na.Alex Mathias,Dodoma

WIZARA ya Viwanda na Biashara imewasilisha bungeni hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 huku ikitangaza kuwachukulia hatua kali za kisheri wawekezaji waliobinafsishiwa viwanda kisha kuvichukulia mikopo mikubwa na kushindwa kulipa.

Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Joseph Kakunda,amesema kuwa Serikali haitaongeza muda ambao walipaswa kuleta maelezo yenye kueleweka serikalini kuhusu viwanda hivyo .

Akizungumzia hali ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa, alibainisha kuwa viwanda 88 vinafanyakazi huku viwanda 68 vikiwa havifanyikazi.

Waziri Kakunda amesema kuwa kati ya viwanda 88 vnavyofanyakazi, viwanda 42 vinafanyakazi vizuri, 46 vinafanyakazi kwa kiasi cha kuridhisha na viwanda 20 vimefutwa kwa sababu ubinafsishwaji wake ulifanywa kwa kuuza mali moja moja na vingine kuruhusiwa kubadili matumizi.

"Viwanda vingine 48 wamiliki wameshindwa kuviendesha kwa mujibu wa mkataba wa mauziano na hivi sasa, tayari viwanda 16 vimerejeshwa serikalini na vingine 32 wamepewa notisi ya kuwasilisha mipango ya kuviendeleza kabla ya Mei 31 mwaka huu," amesisitiza

Pia ameelezea kuwa viwanda 13 havikubinafsishwa kutokana na sababu mbalimbali na hivyo kuendelea kuwa mali ya umma, chini ya msajili wa hazina.

Kakunda amesema kuwa  baadhi ya viwanda hivyo vinafanyakazi kwa kusuasua na vingine havifanyikazi.
"Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) kunatafuta wawekezaji wapya wenye nia ya kuwekeza kwa maslahi mapana ya maendeleo ya nchi yetu.

Katika hotuba yake, ameelezea  kuwa Serikali ina miliki kiwanda cha viuadudu cha Kibaha kwa asilimia 100 kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).

Waziri amesema kuwa kiwanda hicho kina umuhimu katika kupambana na ugonjwa wa maralia, kwani kinazalisha na kusambaza dawa za kuua viluilui na wadudu wakiwemo mbu.

"Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeagiza lita 200,000 zenye thamani ya sh. bilioni 2.64 na tayari imelipa lita 60,000. Aidha, TAMISEMI kupitia Halmashauri mbalimbali nchini imetenga sh.bilioni 8.9 kununua viuadudu kutoa kiwandani," amebainisha

Kakunda amesema kuwa  hadi kufikia Desemba mwaka jana, Tume ya Ushindani ilifanikiwa kufanya kaguzi 153 katika Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu zilizopo Dar es Salaam ili kubaini, kukamata na kuteketeza bidhaa bandia kabla hazijaingia sokoni.

Hata hivyo amesema kuwa katika kaguzi hizo, makasha 1,536 yamekaguliwa ambapo katika makasha hayo makasha 82 yamekamatwa kwa kukiuka Sheria ya Alama za Bidhaa ya Mwaka 1963 na marekebisho yake.

Kakunda amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2018/19, tume ya ushindani imefanya kaguzi za kushtukiza 18 zilizofanyika Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na katika mikoa ya Shinyanga na Tabora ambapo bidhaa bandia ikiwemo viatu, pombe kali na wino wa vitakirishi zilikamatwa.

Aidha Kakunda amebainisha kuwa, kwa mujibu wa kanuni ya 55 ya Kanuni za Alama za Bidhaa ya Mwaka 2008 na marekebisho yake inayompa mamlaka Mkaguzi Mkuu kuharibu au kugawa bidhaa zilizokamatwa, tume imegawa pampu za maji nne na vifaa vya muziki kwa Chuo Cha Polisi Tanzania.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kanali Mstaafu Masoud Ali Khamis, amesema kuwa kuimarika kwa mazingira ya kufanyabiashara nchini ni chachu ya kukua sekta ya viwanda na biashara.

Pia amesema kuwa kwenye sekta ya sukari kumegubikwa na malalamiko juu ya viwango vya sukari inayoingia nchini kulinganisha na mahitaji halisi ya nchi.

"Kamati inaishauri serikali kuweka umakini mkubwa wakati wa kutoa vibali vya kuingiza sukari nchini na kwamba vibali hivyo vitolewe baada ya serikali kufanya tathimini kubaini upungufu wa sukari uliopo," amesisitiza

Kanali Masoud amesema kuwa mahitaji ya bidhaa ya mafuta ya kula nchini ni tani 700,000 na uzalishaji wa bidhaa nchini ni tani 210,000.

Hata hivyo amesema kuwa katika takwimu hizo zinadhihirisha kuwa ili kukidhi mahitaji ya soko ni lazima tofauti iliyopo iruhusiwe kuingia kutoka nje ya nchi.

Aidha amesema kuwa kamati yake inaishauri serikali kuzisimamia kwa ukaribu mamlaka hizo kuhakikisha wanatekeleza majukumu kwa maslahi mapana ya nchini.

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Msemaji wa kambi hiyo kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara, Cesil Mwambe, amesema kuwa bado wafanyabiashara wanakumbana na kadhia kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mhe.Mwambe amesema kuwa kwa kipindi kirefu, TRA imeshindwa kubuni mkakati wa makusanyo ya kodi na badala yake wanatumia vibaya mamlaka katika kutekeleza majukumu na kusababisha malalamiko ya kuwepo vitendo vya rushwa.

No comments