Breaking News

SERIKALI YA RAIS MAGUFULI YAONYESHA MWELEKEO MZURI KUIPELEK A TANZANIA KUWA NCHI YA UCHUMI NA VIWANDA


Na John Mapepele 

Serikali ya awamu ya tano imetimiza  muda wa kutosha kujivunia ikiwa madarakani kwa mafanikio makubwa  katika  dhamira yake kuu ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa viwanda  ifikapo 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, John Magufuli amefanya  mabadiliko makubwa  kwenye  Sekta kuu za uzalishaji ili ziweze kuwa na uzalishaji wenye tija utakaosaidia kuchangia malighafi zinazohitajika katika viwanda hapa nchini.

 Miongoni mwa mabadiliko hayo ni pamoja na kubadili iliyokuwa  Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi na kuunda  Wizara mbili tofauti; Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inayoongozwa na Mh. Luhaga J. Mpina na Naibu wake Abdalah Ulega.

Sekta za Mifugo  na Uvuvi ni miongoni mwa mihimili mikuu katika kujenga nchi ya viwanda kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo 2025 kwa kuwa ni miongoni mwa sekta ambazo zinatoa malighafi  kwa ajili ya  viwanda.

Taarifa zinaonyesha  Tanzania ni nchi ya tisa duniani na ya tatu kwenye nchi za Afrika kwa kuwa na mifugo mingi lakini haichangii kiasi kinachostahili katika uchumi na pato la taifa  ukilinganisha na nchi nyingi duniani ambazo hazina kiasi kikubwa cha mifugo kama nchi yetu.
 
Katika kuhakikisha  kwamba sekta hii inachangia kwa kiasi kinachotakiwa tayari Waziri mwenye  dhamana  ya Sekta hiyo, Mh. Luhaga Mpina amefanya mapinduzi makubwa  kuhakisha  sekta inatoa mchango unao stahili.

Waziri Mpina anasema katika kipindi cha takribani miezi miwili sasa toka kuundwa kwa Wizara mpya ya kusimamia sekta hizo, Serikali imeratibu na kutekeleza mikakati kadhaa inayoweka usimamizi madhubuti ya mapinduzi wa sekta husika.

Ametaja baadhi ya mikakati iliyoanza kutekelezwa katika ngazi ya nchi nzima kuwa ni pamoja na  operesheni  maalumu ya “Ondoa Mifugo na tokomeza Uvuvi haramu” iliyofanyika katika mikoa yote ya mipaka  ya nchi yetu. Operesheni hiyo inalenga kuzuia mifugo yote kuingia na kutoka nje ya nchi bila kufuata taratibu za kisheria.

Mh.Mpina anaongeza kuwa operesheni hiyo pia inalengo la kuondoa kabisa uvuvi wa haramu  wa  kutumia mabomu na nyavu  za kukokota zinazoharibu mazingira  na kuvua samaki wadogo ambao hawajafika katika kiwango  kinachotakiwa katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Novemba mwaka huu.

Hadi sasa tayari maelfu ya mifugo yamekamatwa yaliyoingia nchini bila kufuata utaratibu kutoka katika nchi jirani katika zoezi ambalo limeongozwa na Mh. Mpina mwenyewe ndani ya mwezi mmoja sasa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo anasema ripoti zinaonyesha kwamba asilimia 30 ya malisho ya mifugo nchini inatumiwa na mifugo kutoka nje ya nchi hali inayosababisha  kuleta migogoro mikubwa baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ikiwa ni pamoja na  wakulima.

“Oparesheni hii itasaidia sana kulinda mifugo/wanyama kutopata magonjwa ambayo kama wataugua  serikali italazimika kutibu mifugo kwa gharama kubwa. Wizara itahakikisha kuwa hakuna  mfugo hata mmoja  kutoka  nchi  nyingine utakaoingia  bila kufuata utaratibu na kwamba watendaji watatumia sheria ya magonjwa ya  wanyama na 17 ya mwaka  2003 kifungu cha 62( 1)a,(2) kwa  kuwatoza faini wahusika na kurejesha mifugo ilikotoka  au kuitaifisha mifugo yote” alisisitiza Dkt.Mashingo

Alisema Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inahakikisha  uzalishaji wa malisho ya mifugo unaboreshwa ili kupatikana katika kipindi chote cha mwaka mzima.

Mh. Mpina amezitaka Halimashauri za Wilaya zote nchini kushirikiana na Mamlaka  husika kuhakikisha kuwa maeneo ya  mifugo  yanatengwa  ili wafugaji waweze kuwa na sehemu za kuchungia mifugo yao.

Katika hatua nyingine, Mh. Waziri Mpina ameagiza hadi ifikapo mwisho wa mwezi Desemba mifugo katika yote nchini iwe imepigwa chapa ili kuboresha usimamizi wa sekta hiyo hatimaye kuwa na mazao bora ya mifugo katika masoko ya kimataifa.

“Hatuwezi kukubali sisi kama  nchi kutokuwa wa kwanza  katika masoko ya mazao ya mifugo kimataifa wakati nchi yetu ni miongoni mwa nchi inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo duniani” alisisitiza Mh. Mpina.

Hata hivyo amesisitiza kwamba ni muhimu kwa watendaji wote kwenye Halimashauri zote kuzingatia  namna  bora ya upigaji wa chapa ili kutoharibu thamani ya ngozi katika mifugo inayopigwa chapa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo amesisitiza kwamba Wizara ilishatoa muongozo wa jinsi ya kupiga  chapa mifugo ili kuepuka kuharibu thamani ya ngozi za  mifugo hususan kwenye masoko ya kidunia.

“Ngozi inathamani kubwa kuliko hata nyama, kwa kuzingatia hilo Wizara ilishatoa miongozo ya namna bora ya kupiga chapa mifugo kote nchini na bado hadi sasa inaendelea kufuatilia na kuhakikisha kwamba  zoezi linakamilika kwa usahihi” amesisitiza Dkt. Mashingo.

Ametaja sehemu ambayoinatakiwa kupigwa chapa kwa Ng’ombe ni juu kidogo ya goti katika  mguu wa nyuma wa kulia wa Ng,ombe na kuongeza kwamba  sehemu hiyo pia inafanya ilama kuonekana  vizuri.

Katika hatua nyingine ya mageuzi makubwa ya sekta hiyo, Waziri  Mpina ameagiza Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za  Mifugo za Taifa(NARCO Limited), Profesa, Philemoni Wambura kuvunja  mikataba ya wawekezaji wa vitalu vyenye jumla ya hekta 68,238 kwenye ranchi ya Mkata na Dakawa ndani ya mwezi  mmoja baada kushindwa kuviendeleza na kuvilipia vitalu hivyo kwa muda mrefu.

Ameyataja mambo ambayo Serikali imezingatia katika kufikia hatua hiyo ya kuvunjwa mikataba kuwa ni pamoja na wawekezaji hao kukaa muda mrefu wa kipindi cha kuanzia miaka kumi hadi kumi na nane bila kutekeleza wala kuendeleza vitalu hivyo.

Aidha ,amesema mikataba hiyo haina maslahi kwa taifa kwa kuwa Serikali imekuwa ikiambulia asilimia 30 tu ya hisa zote na wawekezaji kuwa na hisa ya asilimia 70 wakati Serikali ndiye mmiliki  mkuu wa ardhi na miundombinu yote katika mashamba  hayo.

“Hili ni jambo lisiloingia akilini na lisilokubalika  hata kidogo.Serikali haiwezi ikawa inaambulia  kiasi kidogo cha hisa kama hicho wakati ndiyo mmliki wa kila kitu?” amehoji Mpina

Pia amesema jambo jingine ambalo linasikitisha sana katika mikataba hiyo ni tozo la kodi ya ardhi ya shilingi mia tano na shilingi mia tano inayopelekwa NARCO, kwa hekta moja kwa mwaka amesisitiza kuwa hailingani kabisa na bei ya soko ya sasa.
 
Naye Diwani wa Kata ya Parakuyo katika Wilaya ya Kilosa, bwana Ibrahim Kalaita amesema kwambwa ukodishaji wa eneo la hekta moja la shamba la mahindi ni shilingi elfu hamsini wakati ukodishaji wa hekta moja kwa ajili ya kulima mpunga unaanzia shilingi laki moja kwa mwaka.

Aliiomba Serikali kuwanyang’anya wawekezaji wote katika maeneo hayo na badala yake wapewe wafugaji ambao watayaendeleza na kuyalipia  na hivyo serikali kupata faida.

Ameyataja baadhi ya vitalu vya mashamba ambavyo vinaleta  migogoro isiyoisha  katika  katika Wilaya ya Kilosa baina ya wawekezaji,wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi  katika kijiji cha Ngaite Luhoza  kuwa ni  vitalu namba  419 420,421,422na 423.

Hata hivyo, Mh. Mpina ameagiza Mkuu wa Wilaya kupitia kwa Katibu Tawala wa Wilaya Kilosa, bwana Yohana Kasitile kuhakikisha kuwa wanakaa pamoja na  serikali ya Kijiji cha Ngaite  Luhoza kuondoa kesi zote zilizopo mahakamani na kuwa na meza ya pamoja na kujadili namna bora ya kumaliza migogoro iliyopo mara moja.

Mpina amesema kama  vyombo  vya Serikali vingetumika vizuri kuanzia ngazi ya kijiji kungepunguza  migogoro ya wakulima na wafugaji  katika wilaya  hiyo. Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa Wilaya zinaongoza kwa  kuwa na migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

“Naelekeza kwamba kaeni pamoja  mmalize migogoro hii isiyo na tija. Suala la kukimbilia mahakamani wakati ninyi nyote ni vyombo vya Serikali haisaidi kabisa nataka kusikia ndani ya muda mfupi kila kitu kiwe kimemalizika”. Alisisitiza Mpina

Mh. Mpina amezitaja kampuni za wawekezaji ambazo zilizomilikishwa  vitalu zinatakiwa kuvunja mkataba kwa kushindwa kuendeleza na kulipia kwa upande wa Ranchi ya Mkata katika Wilaya ya Kilosa kuwa ni pamoja na Kadolo Farm Company Ltd  kitalu namba 418 yenye hekta 4005,Bagamoyo Farm kitalu namba 419 yenye hekta 3672.96, A to Z Animal Feeds Company Ltd kitalu namba 420 yenye hekta 3692.97 na Ereto Livestock Keepers kitalu namba 422 yenye hekta 4020.54.

Katika Wilaya ya Mvomero kampuni zilizoshindwa  kuendeleza vitalu ni pamoja na kampuni ya  Overland kitalu namba 415 yenye hekta19446.28, Katenda yenye hekta 2500, Mollel yenye  hekta 2500 na Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa (Mtibwa Sugar) chenye hekta 20000 walizomilikishwa toka mwaka 1999 na kushindwa  kukiendeleza na kukilipia kwa miaka 18.

Waziri pia amezitaka Halimashauri zote nchini kutotunga sheria kandamizi  dhidi ya wafugaji. Akitolea mfano, wa sheria ndogo ya Halimashauri ya Mvomero ya kutoza faini ya shilingi 25, 000/=kwa kila mfugo kuingia  katika Wilaya hiyo bila kufuata taratibu  badala ya shilingi elfu kumi iliyoelekezwa katika Sheria ya Magonjwa ya  Wanyama namba 17 ya Mwaka 2003.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT)  Magembe Makoye amesema upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wafugaji utasaidia kuondoa migogoro  baina ya pande hizo na kuendelezwa kwa ranchi hizo za taifa  kutawasaidia wafugaji kupata shamba darasa litakalo wasaidia kufuga kwa kisasa  na kupata mbegu bora  za mifugo.

Katika hatua nyingine, Mh.Mpina ameagiza machinjio ya kisasa ya Ruvu yaliyotelekezwa kwa muda mrefu kujengwa na  kukamillika  ifikapo Desemba, 2018. Majengo ya machinjio hayo yalianza kujengwa mwaka 2010 lakini hadi sasa hayajakamilika  wakati mitambo ya machinjio hayo ikiwa imewasili toka muda mrefu sasa.

Mpina amesema ni muhimu machinjio hayo ya kisasa yakamilike ili Tanzania ianze kuuza mazao yatokanayo na mifugo katika masoko ya kimataifa.

Alielekeza watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kumpelekea mara moja mpango kazi unaoainisha  namna ya kukamilisha ujenzi wa machinjio hiyo ya kisasa ambayo  baada ya kukamilika itakuwa machinjio kubwa kuliko zote nchini.

Aidha, Waziri Mpina  amesema  kukamilika kwa machinjio hiyo kutasaidia kupunguza  usumbufu kwa wafanyabiashara wa mifugo nawapeleka mifugo yao Dar es Salaam   hali ambayo inaongeza uharibifu wa mazingira  kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Waziri Mpina amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Ranchi  za taifa kuhakikisha kuwa  kunatafutwa fedha kwa ajili ya kuzalisha  mbegu bora za mifugo na kuongeza idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa eneo la ranchi ya Ruvu lenye ukubwa wa hekta 44,000 ambapo hivi sasa eneo hilo la ranchi ya Ruvu lina mifugo ipatayo 1530 wakati uwezo wa ni kuwa na mifugo kuanzia 12000 hadi 22000.

Alisisitiza kwamba maboresho hayo lazima yafanyike ifikapo Desemba , 2018  ambapo ifikapo Juni 2018 tathimini ya awali itafanyika kuona ni kwa namna gani agizo hilo limetekelezwa.

“Tunataka wananchi wapate sehemu ya kujifunza,ranchi ya Ruvu iwe sehemu ya kupata mbegu bora. Siwezi kuwa Waziri wa Mifugo wakati shamba langu halina mifugo bora” alisisitiza  Mpina.

Waziri alielekeza kuwa na mfumo wa kisasa wa kufuga  mifugo kitaalamu  badala ya mfumo wa sasa ambapo mifugo  inafugwa  katika mfumo wa asili kwa muda mrefu.

Mh. Mpina amesema  kwa sasa sekta ya mifugo inakadiriwa kuchangia zaidi ya 7% katika  pato la taifa huku sekta ya Uvuvi pia ikitoa ajira kwa watu zaidi ya laki nne wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za uvuvi.

Ameyataja  baadhi ya mafanikio  katika sekta ya mifugo kuwa ni pamoja na  kuzuia  magonjwa ya milipuko ya mifugo,pia kuimarisha ukaguzi  wa  mazao ya mifugo(ngozi, maziwa na nyama) kwenye vituo vyote vya mipakani.
Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi  Mh. Waziri anasema  

Wizara imeweza kudhibiti ubora na usalama wa mazao ambao umeimarisha ushindani wa soko la ndani na nje. Aidha amesema serikali imeweza kujenga maabara ya Uvuvi  yenye viwango vya kimataifa iliyopata ithibati.

Anasema serikali inashaunda Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu  ambayo  kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania inasaidia kusimamia Uvuvi wa Bahari kuu na kuliingizia taifa mapato ambayo yalikuwa yakipotea.

Pia amesema Serikali imejenga mialo 19 katika ziwa Victoria na nane katika   bahari  ya Hindi ili kusaidia  usimamizi wa raslimali za uvuvi. 

Hata  hivyo amesema  wizara kwa kushirikiana na wadau inaimarisha uzalishaji wa viumbe kwenye maji kwa kuchimba  mabwawa. Hadi sasa zaidi ya mabwawa 22,000 ya kufugia samaki yamechimbwa.
 Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye Kofia) akiwa kwenye picha pamoja  na Viongozi wa Wilaya ya Mvomero na Viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania  alipotembelea ranchi ya Dakawa.
 Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye Kofia) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya  ya Mvomero, Muhamed Utaly  kulia  akitoa maelezo ya kuhusu eneo la hekta 20000 zilizoshindwa kuendelezwa na mwekezaji Mtibwa Sugar kwa lengo  la ufugaji. Kushoto ni Meneja Mkuu  wa Kampuni hiyo bwana Stan Rau hapo.

 Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye Kofia na Miwani) akikagua banda  la Mbuzi  linalokadiriwa kuchukua mbuzi 800 kwa wakati mmoja katika ranchi ya Mkata hivi karibuni.

Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (aliyejishika kiuno)  akiangalia kundi la Mbuzi wapatao 100 walioletwa katika ranchi ya Mkata hivi karibuni.

No comments