Breaking News

GWIJI LA MUZIKI ALIYETOWEKA GAFLA ;KASALOO KYANGA

KASALOO KYANGA ‘NYOTA’ ILIYOTOWEKA GHAFLA

NA MWANDISHI WETU

KYANGA Songa ndiyo yalikuwa majina yake aliyezaliwa pamoja na pacha wake  Kasaloo Kyanga amabo wote walikuwa wanamuziki wakitunga na kuimba nyimbo za muziki wa dansi.

Mapacha hao haikuwa rahisi kwa mtu ambaye hakuwa amewazoea kuwatofautisha.Kasaloo kyanga 

Walikuwa wanafanana wajihi, kimo, tambo ndogo, mtindo wao wa kufunga nywele hata sauti zao.

Wengi hawakuwahi kubaini tofauti yao, lakini mmoja kati yao alikuwa na mwanya kinywani.

Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa aliingia humu nchini akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mapacha hao walifanikiwa kuchukuliwa kwenda kupiga muziki katika bendi nyingi hapa za hapa nchini kufuatia umahiri wao wa kutunga na kuimba.

Baadhi ya bendi walizowahi kupigia ni pamoja na Maquis du Zaire, iliyokuwa ikiongozwa na Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Orchestra Super Matimila iliyoongozwa na Ramadhani Mtoro Ongala ‘Dk. Remy’, Orchestra Makassy chini ya uongozi wa Mzee Makassy na Orchestra Sambulumaa iliyoasisiwa na mwanamuziki Chimbwiza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye hivi sasa yumo gerezani akitumikia kifungo cha maisha.

Pacha wake Kyanga Songa alijiunga katika bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS), ambako naye aliwakuta magwiji wa kutunga na kuimba akina Kalala Mbwebwe, Kabeya Badu, Tshibanda Soni, Mobali Jumbe, Dingituka Mollay na wengine wengi.

Mapacha hao mara nyingi walikuwa kila wahamapo bendi, walikuwa wakifuatana kwenda bendi nyingine wakiwa pamoja.

Bendi zingine walizopiga muzuki ni za Ngorongoro Heroes, Tancut Alimasi iliyokuwa imejikita katika mji wa Iringa, Sandton Sound, bendi ya Orchestra Kalunde ya jijini Dar es Salaam inayoongozwa na mwanamuziki Deo Mwanambilimbi na zingine kadhaa.

Kasaloo mara baada kuingia nchini mwaka 1980 akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alijiunga katika bendi ya Maquis du Zaire.

Bendi hiyo ilikuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa White House, Ubungo jijini Dar es Salaam. Huko alikutana na kikosi cha waimbaji mahiri waliompa changamoto ili aweze kung’aa.

Walikuwepo watunzi na waimbaji akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’,  Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clyton’, Mbombo wa Mbomboka, Tshimanga Kalala Assosa, Kiniki Kieto, na Masiya Radi ‘Dikuba Kuba’. Safu hiyo ilikamilishwa kwa waimbaji Issa Nundu na Tabia Mwanjelwa.

Kwa wale waliokuwa wakihudhuria burudani za bendi hiyo ya Maquis du Zaire, watakumbuka usiku mmoja mwaka 1982, ambapo Kasalo Kyanga ilishindwa kufika ukumbini kwa kuwa alikuwa mgonjwa.

Pacha wake Kyanga Songa aliyekuwa akipiga muziki katika bendi ya Orchestra Safari Sound, alifika ukimbini White House akiwa na sare za Maquis.

Akaimba nyimbo zote za nduguye Kasaloo pasipo kubainika na wanamuziki wa Maquis kuwa aliyekuwa akiimba hakuwa Kasalo Kyanga.

Bendi ya Maquis du Zaire ilijipatia sifa nyingi kufuatia wimbo wa Karubandika.

Wimbo huo ulikuja kuwa maarufu katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, Kasaloo aliuimba akiwa katika bendi hiyo kwa umahiri mkubwa.

Kwa ridhaa yako naomba nikudokolee sehemu ndogo ya maeneno machache aliyoyatumbukiza kwenye kiitikio cha wimbo huo. “…Nilitaka kujitumbukiza ndani ya moto miyee, Kumbe bwana yule hana kitanda wala shuka, Pakulala hana,  Analala kwenye stendi ya basi, Pakulala hana Anakesha kwenye kituo cha UDA Karubandika  yoyo acha vituko eeh babaa…”

“ …Akiingia kwenye baa kazi yake kuomba bia, akiingia kuomba bia hana hata aibu sigara pia anaomba mitaani na kwenye mastoo  hujitangazia kuwa yeye ni mkurugenzi wa Kampuni fulani, kumbe sivyo hivyoo…”

Kasaloo na Kyanga  waliziacha bendi zao na kwenda  kujiunga katika bendi ya Tancut Alimasi ya mjini Iringa.

Wakiwa hako walionesha umahiri wao wa kutunga na kuimba vibao vingi walivyovipakuwa vikiwamo vya Butinini, Masafa marefu, Ndoa si utumwa, Nimemkaribisha Nyoka na Alimasi.

Wimbo wa Butinini, Kasaloo alimuimba msichana mmoja wakati huo, aliyekuwa mchezaji wa mpira wa Netiboli mkoani humo aliyekuwa akijulikana kwa majina ya Jane Butinini.

Baadhi ya wanamuziki maarufu waliounda bendi hiyo walikuwa ni waimbaji maarufu Kalala Mbwebwe,John Kitime na wengine wengi.

Magitaa yaikamatwa na Kawelee Mutimanwa, Alli Makunguru na kwa upande wa Saxophone walikuwapo Mafumu Bilali na Suleiman Akulyake, King Maluu na wengine wengi.

Bendi ya Orchestra Makassy ilimchukuwa Kyanga ambako aliimba katika bendi hiyo akipishana sauti na Issa Nundu.

Aidha Kayanga alishirikiana vyema na Massiya Radi ‘Dikuba Kuba’ kuimba wimbo wa ‘Tunagombana bure’. Massiya Radi alifariki kwa ajali ya kugongwa na gari maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mapacha hao walikuwa na soko katika muziki kwa kuwa baadaye alikwenda kujiunga katika bendi ya  Sandston Sound, baada ya kutoka  bendi ya Orchestra Kalunde.

Kwa mapenzi yake Mungu mapacha hao hatunao tena hapa duniani. Kyanga Songa alifariki akiwa nchini Kenya wakati  Kasalo Kyanga aliaga dunia akiwa katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Setemba 9, 2011 alikokuwa amelazwa kwa matatizo ya mapafu yake kujaa maji.

Miaka  michache ya mwisho kabla ya kifo chake, Kasalo kyanga alibadili dini na kuwa muislamu, akapewa majina ya Selemani Kasaloo.

Ili kuondoa utata aliodhani kuwa ungelitokea wakati wa mazishi yake, Kasalo aliacha wosia kwamba Mungu akimchukua, azikwe kwa sheria na taratibu zote za dini yake ya Kiislam.

Wosia huo iliwabana hata wale waliwaka fikra za kumzika kwa taratibu za dini yake ya zamani.

Alipofariki walifuata maelekezo hayo ambapo mwili wake ulitayarishwa kwa taratibu zote za dini hiyo ya Kiislam kabla ya kuuweka katika nyumba yake ya milele, kwenye makaburi ya Sinza jijini Dar es Salaam.

Selemani Kasaloo aliacha wake wawili na watoto 6.

Selemani Kasaloo na Kyanga Songa wataendelea kukumbukwa kwa yote waliyotuachia ikiwa ni pamoja na utanashati wao.

 Mungu azipumzishwe roho zao pahala pema peponi, Amina.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba 0653900150

No comments