Breaking News

MJUE ALMAR'HUUM "AZIZ ALI" ALI DOSSA KIDONYO


NA MWANDISHI WETU

Ni katika Waafrika wa mwanzo matajiri katika jiji la Dar es Salaam.

Wema wake ulisambaa na kumpatia jina la "Aziz"

Mwezi wa Ramadhani milango ya nyumba zake ilikuwa wazi kuwahudumikia kwa FUTARI mamia ya watu

Temeke imehifazi jina lake kwa eneo moja la Mtoni kuitwa "Mtoni kwa Aziz Ali"Al Haj Aziz Ali akiwa na wanae kulia Hamza Aziz, Dossa Aziz 
na Ramadhani Aziz

Leo tutamuelezea kwa ufupi katika kipengele hichi cha "MWANAUKUMBI WA WIKI" ambacho tunatarajia kuwepo kila wiki kikimuelezea mmoja wa Watu tutakao watambulisha InshaAllah 

JINA LA MTONI KWA AZIZ ALI  LIMETOKEA WAPI!?*

Wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam, kuna eneo linaitwa Mtoni. Mtoni yenyewe nayo ina mitaa mingi ikiwamo Mtoni Kijichi, Mtoni Mtongani, Mtoni kwa Chaurembo, Mtoni kwa Mwenye Kuuchimba na Mtoni kwa Aziz Ali.

Kwa wakazi wa Dar es Salaam haswa wenye kuishi maeneo ya Mtoni, barabara ya Kilwa mpaka Mbagala jina ili la Mtoni kwa Aziz Ali, si jina geni.

Hapo Mtoni kwa Aziz Ali, siku nyingi nyuma alipata kuishi bwana mmoja aliyekuwa mmoja wa Waafrika matajiri sana kupata kutokea wakati huo wa ukoloni nchini Tanganyika. Aliitwa Ali Dossa Kidonyo na kwa hiyo kutokana na umaarufu wake, mahala hapo pakaitwa Mtoni Kwa Aziz Ali.

Aziz Ali, alikuwa Mdigo aliyetokea sehemu za Tanga na kuja kuweka kambi mjini Mzizima (sasa Dar es salaam), mwanzo wa Vita Kuu ya Kwanza (1914-1918) akiwa askari katika jeshi la Wajerumani na baada ya vita aliajiriwa na Goa mmoja.

Mwajiri wake alipoondoka nchini alimwachia Aziz Ali gari mbili na hizi ndizo alizoanzia kufanyia biashara hapo mwanzo na kufungua kampuni ya ujenzi na kuajiri mafundi kadhaa.

Aziz Ali alijitengenezea umaarufu kutokana na kwamba aliweza kumiliki majumba mengi na magari ya biashara (yaani malori ya mchanga) pamoja na ya kutembelea, na vitu vingine kadhaa, kutokana na kazi yake ya kuwa mtaalamu wa kujenga nyumba (building contractor).

Hili jina la Aziz alipewa na watu wa Dar es Salaam kwa hisani na wema wake.

Huyu Aziz Ali alikuwa mwamba katika miamba ya Dar es Salaam. Alikuwa tajiri ,contractor,' wa kujenga, majumba, Mwafrika wa kwanza kununua magari na kujenga nyumba ya vigae na vioo Mtoni.

Yeye alikuwa akitoa fursa kwa watu kumpa pesa kidogo kidogo kama malipo ya nyumba alizokuwa anawajengea na alikuwa mtu akishindwa kulipa akimpa muda hadi atakapoweza.

Nyumbani kwake mwezi Mtukufu wa Ramadhani alikuwa akitandika nje majamvi na kufuturisha hadi watu 100 asiowajua wakija wanafuturu na kuondoka.

Nyumba hii hadi leo ipo na sehemu hiyo kandokando ya barabara ya Kilwa na ndipo hapo pakaja kuitwa Mtoni kwa Aziz Ali.

                   Aziz Ali

Lakini katika sifa hizi sifa yake kubwa sana Aziz Ali ilikuwa ujenzi wa misikiti na kuihudumia misikiti. Hii ilikuwa miaka ya 1930 na hapakuwa na umeme Kariakoo.

Misikiti ilikuwa ikitumia karabai kuonea. Aziz Ali yeye alinunua karabai kwa kila msikiti na ikifika Maghrib mwanae Hamza alikuwa akizitia mafuta na kuziwasha kisha akizipeleka kila msikiti tayari kwa sala ya Maghrib.

Inapomalizika sala ya Isha alikuwa anapita tena katika ile misikiti kukusanya karabai zake na kurudi nazo nyumbani kwao Mtaa wa Mbaruku na Kongo.

Mzee Aziz Ali alikuwa na nyumba nyingi sana Dar es Salaam na ndiyo zilikuwa moja ya utajiri wake.

 Katika nyumba hizi nyumba ambayo imaecha historia ya pekee ni hii nyumba ya Mtaa wa Mbaruku na Congo.

Nyumba hii ilikuwa moja ya sehemu ambazo harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika zilianzia hapo. Nyumba nyingine ilikuwa Mtaa wa Kipata kwa Ally Sykes, hapo zamani lilipokuwa duka la baba yake na barza ya wazee.

Nyumba nyingine ilikuwa Stanley Street kwa Abdul Sykes. Nyumba hii ilikuwa pia ya Kleist na kulikuwa na duka la vifaa vya ujenzi katika uhai wake.

Mzee Azizi Ali alitoa mchango mkubwa sana katika harakati za uhuru wa nchi hii kwa kujitolea mali zake na nguvu zake mfanyabiashara na aliyemiliki kampuni ya ujenzi  wa nyumba, yetu yeye ndie alikua mjenzi miaka hiyo na nyumba nyingi tu mjini mitaa ya Kariakoo .

Yeye alikua amezijenga tena kwa kumlipa kidogo na baadae kummalizia malipo yake kwa makubaliano maalum na wala hajawahi kumshtaki mtu kumcheleweshea malipo yake.

Ndipo kutokana na ukarimu wake mkubwa wakamwita "Aziz" yaani "Kipenzi." Ikawa wakimtaja jina wanatanguliza "Aziz," yaani "Kipenzi chetu Ali." Kiasi ikapelekea jina lake la Kidonyo likafa kabisa. Kwa hakika Aziz Ali alikuwa mcha Mungu sana.

Mzee Aziz Ali alipokufa mwaka wa 1951 miaka miwili baada ya kifo cha rafiki yake Kleist gazeti la Tanganyika Standard liliandika kifo chake kwa maneno haya: 'Aziz Ali the Builder of Mosques is Dead,' yaani, Aziz Ali Mjenzi wa Misikiti Amekufa.'

Alipofariki Mzee Aziz Ali, biashara zake ziliendelezwa na Mmoja wa watoto zake, Dossa Aziz Ali, na hata zile harakati za uhuru alijihusisha nazo tena kwa undani zaidi.

Hii ilikuwa mwanzoni mwa mwaka wa 1950. Mambo yalipamba moto sana kuanzia mwaka huo pale vijana wazalendo walipoanza kufanya mipango ya kuunda chama cha siasa halisi kupambana na ukoloni wa Muingereza.

Nyumba zlizokuwa anamiliki Mzee Aziz Ali ndizo zikawa nyumba ambazo Nyerere alikuwa akifikia kuanzia mwaka wa 1952 kila anapokuja mjini kutokea Pugu alipokuwa akifundisha.

Dossa Aziz Ali (Mtoo wa Aziz Ali), alikuwamo katika kuasisi vyombo vyote vya mwanzo vinavyonasibishwa na harakati za kumng’oa Mkoloni, kama vile TAA na TANU akiwa Afisa na Mjumbe mwanadamizi aliye na sauti - hili  sawa; hili fanya; hili wacha na mambo yakawa hivyo asemavyo.

Dossa, kwa kushirikiana na mwanachama mwengine Alexander Tobias, walichaguliwa na wenzao wakati fulani wawe makatibu wa pamoja wa muhtasari.

Harakati ziliposuasua alikuwa hachoki kuwapitia wenzake na kuwakumbusha majukumu waliyopeana akienda kwa mmoja mmoja nyumbani kwake kwa kutumia gari lake na kutaka kujua kulikoni mambo hayendi ipasavyo.

Katika siku za mwanzo za harakati, chama cha TAA na baadaye TANU havikuwa na uwezo wa kifedha wa kujiendeshea mambo yake hata kidogo.

Tegemeo lao kubwa lilikuwa ni kwa watu kama akina Dossa Azizi, aliyekuwa mkurugenzi na msimamizi mkuu wa biashara na mali za babake.

Wengine ni Mzee John Rupia na wale akina Sykes watatu (Abdul, Ally na Abbas), ambao baba zao walikuwa na uwezo wa fedha, ‘wawapige jeki’ (wachangie pakubwa).  

Habari zinasema, ilikuwa ni Dossa Aziz aliyemwomba Nyerere kuacha tena kuvaa kaptura mbele ya wazee, kwani sasa ameshakuwa kiongozi ambaye atakuwa akikutana na watu wazima na hivyo si vizuri kuonekana na kaptura na stockings (zile soksi ndefu mpaka magotini).

Mzee Dossa alifanikiwa katika  hilo kwani alimnunulia pia Nyerere suti kadhaa maridadi katika safari yake ya kule UNO -Umoja wa Mataifa (wakati ule), ili kupeleka kilio cha Watanganyika kudai nchi yao.

HIYO ndiyo historia fupi ya AZIZ ALI

No comments