Breaking News

SHEIKH SULEIMAN TAKADIR "Makarios" Miiko ya TANU ilivyomuondoa kwenye siasaNA MUSSA YUSUPH

SIASA za TANU zilikuwa zimejikita kwenye miiko ambayo laiti kama ingekuwepo hadi leo, basi wengi wangejikuta wakitupwa nje ya ulingo wa kisiasa hasa kutokana na idadi kubwa wanasiasa wa sasa kuwa na hila za kusaka uongozi kwa mbinu yeyote.

Lakini, wazee walioanzisha chama hicho waliamini kuishi bila miiko ni sawa na fisi kumkabidhi bucha, kwani mwanadamu ni mtu mwenye matamanio na anaposhika hatamu, wengi hujiangalia wao badala ya kundi analoliongoza.

Kutoka kushoto: Sheikh Suleiman Takadir, Mbutta Milando, John Rupia na Julius Nyerere. Hao Waliowazunguka na silaha za jadi ni Bantu Group kundi la vijana wa TANU lililokuwa linatoa ulinzi kwa viongozi wa TANU. Picha Hii Ilipigwa Mwaka wa 1955.

Kwa sababu ya misingi waliojiwekea wazee wa TANU, wengi wao wamefariki wakiwa mafukara na hata majina au historia zao kusahaulika.

Kusahaulika kwao kulitokana na wengi walijikita katika kuhakikisha Tanganyika inapata uhuru na si wao kuwa maarufu au kujilimbikizia mali.

Miongoni mwa wapigania uhuru wa Tanganyika waliosahahulika ni Sheikh Suleiman Takadir, ambaye alikuwa mwanaharakati mzalendo na mwanazuoni wa Kiislamu.

Vilevile alikuwa mmoja kati ya watu wa awali walioshirikiana na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, katika harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika. 

Jina la mwanazuoni huyu limesahaulika kabisa na hata kupata baadhi ya kumbukumbu zake muhimu ni vigumu.
Sheikh Takadir jina lake husikika kwenye harakati za kidini pekee kwani alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa mwanzo wa kiislamu Tanganyika.
Historia muhimu ya kisiasa kwa kiongozi huyo inaanzia mwaka 1954 alipokuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU.
Alishiriki vilivyo ndani ya baraza hilo katika kutayarisha safari ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwenda Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1955. 

Kipindi hicho Sheikh Takadir alikuwa akisifika kwa jina la "Makarios," wakimfananisha na Askofu Makarios wa wa Ugiriki, aliyekuwa akipambana na ukoloni wa Waingereza nchini humo, wakati Sheikh Takadir akiwa anapambana na Waingereza katika ardhi ya Tanganyika. 

Kwa kuwa Takadir alikuwa sheikh na mpambanaji ndipo walimpa jina la "Makarios" na yeye akalipenda.

Mikutano ya mwanzo ya TANU ilikuwa ikifanyika Mnazi Mmoja na baadaye kwenye uwanja uliojengwa jengo la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kipindi hicho eneo hilo lilikuwa mali ya Mzee John Rupia.

Mzee Rupia ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa TANU, alikipa TANU uwanja huo utumike katika shughuli za chama na serikali.
Mikutano ya kwanza ya TANU kabla Nyerere hajapanda kwenye jukwaa kuzungumza na wananchi, alikuwa akitangulia Sheikh Takadir, kuweka mambo sawa.
Kama alivyokuwa Nyerere, Sheikh Takadiri alikuwa na kipaji cha kuongea na kabla Nyerere hajazungumza alikuwa akisoma dua maalumu. 

Baada ya hapo ndipo atapanda Nyerere kuanza kuhutubia. 
Sheikh Takadir alimpenda sana Nyerere kiasi kwamba mwaka 1957 katika hotuba aliyoitoa kwenye tafrija moja ya taarab Mtaa wa Mvita, alimwita Nyerere, "Mtume wa Afrika," aliyetumwa na Mungu kuwaokoa Waafrika. 

Mara kwa mara Nyerere alikuwa akipenda kumtembelea Sheikh Takadir nyumbani kwake Mtaa wa Swahili, Kariakoo. 
Kitendo hicho kilimkera sana Baba mwenye nyumba aliyokuwa akiishi Sheikh Takadir ambapo alilazimika kumfukuza Sheikh Takadir ili asije kumponza kwani Nyerere alijulikana kama adui mkubwa wa Waingereza.

Siasa kwa mwanazuoni huyo zilifika tamati mwaka 1958 baada ya kuvunja miiko ya TANU kwa kosa la kuchanganya dini na siasa.

Wakati huo TANU ikiongozwa na Mufti Sheikh Hassan Bin Amir, ilipitisha azimio la kupiga vita hisia zozote na chembechembe za udini ndani ya TANU.

Inadaiwa kuwa chanzo cha mtafaruku huo ni Uchaguzi wa Kura Tatu wa mwaka 1958. Waingereza waliweka masharti ambayo kwa hakika yalikuwa ya kibaguzi na yalifanya wananchi wengi wasiweze kukidhi sifa zilizowekwa za kupiga au kupigiwa kura. 

Kulikuwa na sifa ya elimu, kipato, kazi ya kukubalika na kupiga kura kwa tabaka za rangi. 
Mpiga kura Mwafrika alitakiwa ampigie kura Mzungu, Muasia na Mwafrika. Masharti hayo yalikuwa kisiki kigumu kwa uongozi wa TANU na wanachama wake kutimiza. 
TANU na viongozi wake wengi hawakuwa na elimu iliyokuwa ikitakiwa wala kipato cha maana. 
Ili mtu asimame kama mgombea kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria awe angalau na sifa hizo zilizotolewa na mkoloni.
Wapiga Kura na wagombea walitakiwa wawe na elimu ya darasa la 10 au kipato cha pauni 400 kwa mwaka na kuwa na kazi ya maana. 

Waafrika waliokuwa na sifa hizo hawakuwa wengi katika TANU. Wengi katika TANU walikuwa makabwela.

Ikawa ili TANU iweze kuweka wagombea ilibidi iwatafute watu nje ya uongozi wa TANU. Hapo ndipo lilipokuwa tatizo.

Jambo hilo lilimkera Sheikh Takadir na wanachama wengi wa TANU, kwani hawakutaka kushiriki uchaguzi huo kwa masharti waliyoyaona ya kibaguzi. 

Ililazimika hatma ya kushiriki kwa TANU katika Uchaguzi wa Kura Tatu ijadiliwe kwenye Mkutano Mkuu wa TANU wa mwaka 1958, uliopangwa kufanyika Tabora.

Inadaiwa kuwa mpinzani mkubwa wa Kura Tatu alikuwa Zuberi Mtemvu ambaye alikuwa Katibu Mwenezi wa TANU kwa wakati huo.

Ukweli ni kuwa Kura Tatu ilitishia uhai wa TANU na zilikuwapo dalili za chama kumeguka pande mbili. 

Kulikuwa na uwezekano mkubwa sana kuwa Zuberi Mtemvu na Sheikh Takadir wangelikuwa upande mmoja na wangeweza kuja na chama kingine ingawa ajenda zao zilikuwa tofauti.

Mtemvu alisimama kwenye Afrika kwa Waafrika na Sheikh Takadir kwenye Uislam. 

Sheikh Takadir na baadhi ya wazee katika Baraza la Wazee wa TANU walikuwa wajumbe katika mkutano wa Tabora. 

TANU ilipiga kura kukubali kuingia kwenye Uchaguzi wa Kura Tatu, hivyo TANU iliingia katika Uchaguzi huo na ikapata ushindi mkubwa.

Mara baada ya mkutano huo malumbano makubwa yaliibuka kwa wanachama kumshutumu Sheikh Takadir kuingiza misimamo ya kidini ndani ya TANU.

Akiwa Dar es Salaam mara baada ya kuvuliwa uanachama wa TANU kwa kosa hilo, kundi kubwa la wanachama na wakazi wa mkoa huo waliandamana hadi kwenye makazi yake kumshutumu anataka kukigawa TANU kwa misingi ya dini.

Kutokana na tuhuma hizo ndiko ikawa mwisho kwa mwanzuoni huyo kushiriki kwenye harakati za kisiasa hadi Tanganyika inapata uhuru kutoka kwa Waingereza.

No comments