Breaking News

TASAF ;NAMTUMBO NA MKAKATI WA KUTOKOMEZA UMASIKINI

TASAF Namtumbo, mkakati wa kukuza ujasiriamali na kutokomeza umaskini

NA  DUSTAN  NDUNGURU,

UMASKINI ni hali ya maisha isiyoridhisha ikiwemo kuwa na kipato duni, kuishi katika mazingira duni, ambayo mara nyingi huambatana na  magonjwa na ujinga.

Jitihada mbalimbali zinaendelea kufanywa na serikali kupitia taasisi mbalimbali kukabiliana na hali hiyo.

Serikali kwa kushirikiana na wananchi imekuwa ikibuni mbinu na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kupambana na maadui hao.
Hata hivyo umaskini bado upo kwa  kiwango kikubwa kulingana na idadi ya Watanzania wasio na uwezo wa kupata mahitaji ya msingi ikiwemo chakula, malazi, mavazi, elimu na matibabu.

Nchini umaskini ni miongoni mwa maadui hao watatu ambao vita dhidi yake imekuwa ikitangazwa, kutokana na ukweli kwamba ni kikwazo cha maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Katika jamii zipo kaya zenye hali mbaya kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha na hivyo kujikuta zikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kupeleka watoto shule na kutomudu gharama za matibabu.

Mpango wa kunusuru kaya maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), umekuwa msaada mkubwa kwa kaya maskini tangu kuanzishwa mwaka 2012.Kaya hizo zimekuwa zikinufaika kwa kupata fedha ambazo huzisaidia  kumudu gharama muhimu, tofauti na awali.

Wilaya ya Namtumbo, Mkoani Ruvuma ni moja kati ya wilaya zianazopokea fedha zinazotolewa na serikali, kupitia mfuko huo kwa ajili ya kaya maskini, ambapo tangu Julai mwaka 2015, kaya 5,556 zilianza kunufaika kwa awamu.

Ofisa Ufuatiliaji wa TASAF wilayani humo, Masejo Songo, anasema licha ya kupewa fedha, wanufaika hao hupatiwa elimu ya ujasiriamali ili kuanzisha miradi ya ufugaji na kilimo.
Jambo hilo limekuwa likitekelezwa kwa walengwa hao, hivyo kuwapa manufaa makubwa.

“Tumekuwa tukiwahamasisha kuanzisha vikundi vya ujasiriamali kwani fedha wanazopata kiasi wamekuwa wakichangiana na kujiwekea akiba, hukopeshana wao kwa wao hivyo kuwasaidia kukabili changamoto mbalimbali.

Anasema kuwa vikundi vingi ambavyo vinaanzishwa katika jamii na uzoefu unaonyesha ni za wenye kipato bora, huku kaya maskini zikishindwa kumudu kujiunga na kutokana na kukosa uwezo.

Hivyo wao wameamua kuhamasisha walengwa kujiunga pamoja na kuanzisha vikundi jambo ambalo limekuwa na mwitikio mkubwa.

Songo anasema kupitia vikundi hivyo wanufaika ambao ni kaya masikini watakuwa na uwezo wa kuanzisha miradi ya pamoja, licha ya kukopeshana pia pindi vitakapojiimarisha vitapata fursa ya kukopa kwenye taasisi za fedha.

Hadi sasa anasema vipo jumla ya vikundi 26 vilivyoanzishwa na wanufaika wa mpango huo, ambapo wamedhamiria kuongeza zaidi ili  wengi zaidi wanufaike kupitia mikopo watakayokuwa wakiipata.

Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika kijiji cha Mandepwende, kata ya Lwinga wameanzisha kikundi chao kiitwacho ‘TASAF Maendeleo’  wanaiomba serikali kuona uwezekano wa kuwapatia elimu ya ujasiriamali.

Wanasema hatua hiyo itawawezesha kupata ujuzi wa kutengeneza sabuni na kusindika mazao wanayozalisha, hivyo kujikwamua kichumi na kuondokana na umasikini.

Katibu wa kikundi cha TASAF Maendeleo Stella Millinga, anasema kuwa kikundi hicho kina jumla ya wanachama 10, kilianza mwaka 2016,  huku kila mwanachama akipaswa kuingia kwa sh. 20,000, awe na hisa za sh. 5,000 na kwamba wanachama wa kikundi ni wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini.

Stella anasema kuwa waliamua kuanzisha kikundi hicho baada ya kuhamasishwa na maofisa maendeleo ya jamii na hivi sasa kinaendelea vizuri.

“Tunaona upo umuhimu kwa serikali kuwapa mafunzo ambayo yatawawezesha kujiendesha wenyewe badala ya kuendelea kutegemea fedha zinazotolewa na mpango huo peke.

Unajua sio kaya masikini zote zimefikiwa na mpango huo wa TASAF, hivyo sisi ambao tumebahatika ni vyema tukajiunga kwenye vikundi na serikali ihakikishe inatoa mafunzo, kutoa mikopo ili kufanikisha uanzishwaji wa miradi ambayo itachochea maendeleo hivyo kuondokana na misaada kama ilivyo sasa,” anasema Stella.

Daima Adam, ni mwanachama wa kikundi hicho anasema tangu kuanzishwa kwa kikundi hicho amefanikiwa kukarabati nyumba yake ambayo ilibomoka kutokana na mvua miaka miwili iliyopita.

Pia anamudu kuwapatia mahitaji muhimu watoto wake wawili  wanaosoma katika shule ya msingi Mandepwende.
Mwanakikundi na mnufaika Latiffa Kassim anawaasa wenzake kuhakikisha wanatumia vizuri fedha wanazokopeshana na kuzirejesha kwa wakati ili na wengine wapate fursa ya kukopa.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Lwinga, Dafrosa Malisa, anasema vikundi vingine vya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini ambao wamehamasishwa kuanzisha ni ‘Muungano TASAF’ kilichopo katika kijiji cha Rwinga na ‘Upendo TASAF’ katika kijiji cha Minazini.


Dafrosa anawaasa wanachama wa vikundi hivyo kuhakikisha wanatumia vema fedha wanazokopa kwa kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo ufugaji na kilimo, pia  kuwapatia watoto wao mahitaji muhimu ili kuwawezesha kufanya  vizuri katika masomo.

Wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika  kijiji cha Mtonya, kata ya Likuyuseka,  wameamua kujiunga pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ambavyo vinawawezesha kukopeshana na hivyo kukabiliana na umaskini.

Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii, Kata ya Namtumbo, Melania Nchimbi, anasema katika kijiji hicho vipo vikundi viwili vilivyoazishwa na wanufaika hao baada ya kuhamasishwa, kujengewa uwezo na kufuatiliwa kwa karibu, ambapo wanalenga kuvisajili ili vitambulike kisheria.

Melania anavitaja vikundi hivyo kuwa ni Mkombozi na Upendo TASAF, ambapo     kwa kikundi cha Mkombozi kinao wanachama 20 na hisa zenye thamani ya shilingi 69,000 na kikundi cha Upendo kina jumuisha wanachama 13 na kina hisa zenye thamani ya sh 230,000.

Zaina Ali ni mwanachama wa kikundi cha Mkombozi, anasema kupitia kikundi hicho amewapatia mahitaji muhimu wajukuu zake wanaosoma, pia amefanikiwa kuanzisha mradi wa ufugaji kuku unaomwingizia kipato,  hivyo kuepukana na adha ya kuomba iliyokuwa ikimkabili awali.

Fatuma Luambano na Amina Mtoyomba wa kikundi cha Mkombozi wanasema mpango wa kunusuru kaya masikini umewafungua kimaisha kwa kuwapatia mwanga mkubwa wa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali.

Wanasema kabla ya kuanzishawa kwa  mpango huo hawakuawa na shughuli ya kufanya kutokana na kukosa mtaji, lakini hivi sasa wanatumia vizuri elimu wanayoipata kutoka kwa maofisa maendeleo ya jamii kuhusu matumizi makini ya fedha tunazozipata, ikiwemo kujiunga na bima ya afya ili kunufaika na matibabu bure.

Awetu Issa wa kikundi cha Upendo anasema tangu aanze kupata fedha za TASAF huzitumia vizuri, ameanzisha mradi wa ufugaji kuku ambapo unaomsaidia kumudu gharama za maisha.

Anaishukuru serikali kwa hatua ya  kuzikumbuka kaya masikini ambazo nazo zinastahili kupata huduma muhimu kama wanazopata walio na uwezo.

Mratibu wa TASAF Wilayani Namtumbo Raphael Mponda,  anasema wananchi wanaopokea fedha za kunusuru kaya masikini zinazotolewa wanapaswa kuwekeza ili kuwa na mitaji mikubwa itakayowafanya kuondokana na umasikini.

Anabainisha kwamba wanufaika wa kaya masikini ambao tayari wameitikia kuanzisha vikundi vya kijasiriamali, wamejikita kikamilifu katika jitihada za kutokomeza umaskini, hivyo ambao hawajajiunga kwenye vikundi hivyo wajiunge.

Anasema kuwa licha ya serikali kutoa fedha hizo zinazoonekana kidogo kwa walengwa lakini wanapaswa kuzitumia vyema kwa kuwekeza kibiashara na kufanikiwa badala ya kuzitumia zote bila kufanya mambo ya maendeleo.

Mratibu huyo anasema lengo la serikali ni kuona wananchi wanakuwa na mitaji ya kufanyia shughuli za  maendeleo, hivyo wanapaswa kuwa wajasiriamali.

Katika wilaya ya Namtumbo anayoiratibu anaahidi kuhakikisha wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini wanajikita pia katika shughuli za kijasiriamali kupitia vikundi au mtu mmoja mmoja kujikita katika ufugaji.

“Wananchi ambao wapo kwenye kaya masikini wameanza kuonyesha mafanikio kwa kuwa wamesaidia kuanzishwa miradi midogo inayowawezesha kuendeleza maisha, lakini tuna matumaini makubwa baada ya kuimarika kwa vikundi vya kijasiriamali vya walengwa maisha yao yatabadilika, kwani dhamira ya serikali ya kuzikomboa kaya masikini itakuwa imetimia,” anasema.

Anataja changamoto za mpango huo kuwa ni ugumu wa mawasiliano ya kuwafikia walengwa hususan vipindi vya mvua na kuongezeka kwa uhitaji kutoka katika kaya zenye sifa ambazo hazikuweza kuingia katika mpango. 

Mponda anasema kuanzia Julai 2015,  walipoanza kupokea fedha kwa ajili ya kaya masikini hadi mwaka jana, tayari sh. bilioni 3 zimetolewa kwa walengwa wilayani Namtumbo na kwamba kwa vikundi 26 vya walengwa vilivyopo wilayani humo vina akiba ya takriban sh. milioni 5, pia sh. milioni 3.5 zimekwishatolewa kwa wanavikundi 93 ambao ni wanachama.

Uhamasishaji wa walengwa na wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini ili wajiunge kwenye vikundi unaofanywa na TASAF wilayani Namtumbo, unapaswa kuigwa na wilaya zingine kote nchini ili kutoa msaada kwa kaya maskini.

 Pia asilimia 10 ya fedha zinazotengwa kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake na vijana, zielekezwe kwa vikundi hivyo vya kaya masikini jambo litakalowawezesha kuendeleza shughuli za ujasiriamali

No comments