Breaking News

TRUMP; SYRIA IJIANDAE KWA KOMBORA

NA MWANDISHI WETU
Rais wa Marekani Donald Trump amechapisha ujumbe wa Twitter kwamba Urusi inafaa 'kujiandaa' kwa kombora litakalorushwa nchini Syria akijibu madai ya shambulio la kemikali wikendi.
Maafisa wakuu wa Urusi walitishia kujibu shambulio lolote la Marekani. Bwana Trump aliahidi kujibu vikali madai hayo ya shambulio la kemikali.
Serikali ya Bashar al-Assad ambayo hupokea usaidizi wa kijeshi kutoka Urusi imekana kuhusika na shambulio hilo la kemikali.
Katika chapisho lake la Twitter, bwana Trump alimuita rais Assad 'mnyama anayetumia gesi kuua watu'.
Siku ya Jumamosi, wanaharakati wa Syria, waokoaji na maafisa wa matibabu walisema kuwa mji huo wa Douma unaodhibitiwa na waasi katika jimbo la mashariki la Ghouta ulishambuliwa na vikosi vya serikali kwa kutumia mabomu yalio na sumu.
Shirika la matibabu linaloshirikisha mataifa ya Syria na Marekani limesema kuwa watu 500 walipatikana na dalili za kushambuliwa na kemikali
Siku ya Jumatano, shirika la afya duniani WHO lilitaka kuingia katika eneo hilo ili kuthibitisha ripoti kutoka kwa washirika wake kwamba watu 70 walifariki, ikiwemo 43 waliokuwa na ishara za kushambuliwa na kemikali za sumu.
Marekani na washirika wake Ufaransa na Uingereza wamekubali kufanya kazi pamoja na wanaaminika kujiandaa kutekeleza shambulio la kijeshi.

Serikali ya Urusi imetaja ripoti za shambulio la kemikali kama uchokozi unaolenga kuthibitisha haki ya Ulaya kumuingilia mshirika wake, Syria.
Maafisa kadhaa wa Urusi wameonya kuhusu jibu la Urusi iwapo Marekani itashambulia huku Alexander Zasypkin , ambaye ni balozi wa Urusi nchini Lebanon akiregelea onyo la kiongozi wa jeshi kwamba makombora yatatunguliwa huku maeneo yanayotoka yakilengwa.
Bwana Trump alikuwa akijibu tishio hili
Pia siku ya Jumatano, msemaji wa waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Maria Zakharova aliuliza iwapo lengo la mashambulio hayo ya magharibi ni kuondoa dalili za uchokozi huo ili wachunguzi wa kimataifa wakose ushahidi.
Rais wa Marekani Donald Trump alifutilia mbali ziara yake Marekani ya kusini ili aangazie Syria. Hatua hiyo inaonyesha kwamba jibu la Marekani litashirikisha operesheni kubwa ya kijeshi , kulingana na mwandishi wa BBC Barbara Plett Usher mjini Washington.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kuwa shambulio lolote litalenga vifaa vya kemikali vya serikali ya Syria.

Lakini gazeti la The Times limeripoti kwamba waziri mkuu wa Uingereza Theresa May amemtaka Trump kutoa ushahidi zaidi kuhusu shambulio hilo la kemikali.
Balozi wa Moscow katika shirika la Umoja wa Mataifa , Vasily Nebenzia ameionya Washington kwamba itawajibika kwa shambulio lolote la kijeshi itakalotekeleza.

No comments