Breaking News

UMILIKI WA RASILIMALI ARDHI KWA WANAWAKE USIGUBIKWE NA URASIMUNA SULEIMAN PANDU

UPO mwamko hivi sasa kwa wanawake kuhusu umuhimu wa kumiliki ardhi na majengo.


Hatua hiyo inatokana na taasisi mbalimbali za serikali na asasi za kiraia kutoa elimu kwa wanawake.


Zeyana Seif Ali (38), mkazi wa Jumbi, Wilaya ya Kati, Unguja, ameonyesha mfano kwa wanawake baada ya kuhakikisha anafanikiwa kupata hati miliki ya shamba.Zeyana Seif   mwanamke aliyeteeska zaidi ya mwaka mmoja akitafuta hati miliki ya shamba lakeHati miliki hiyo anaipata kwa kuihangaikia kwa zaidi ya miaka miwili bila kukata tamaa, akifuatilia katika ofisi mbali mbali za serikali na za halmashauri ya wilaya na mkoa.

“Inahitaji ujasiri kutafuta hadi kufananikiwa kupata hatimiliki ya ardhi ambayo kwa sasa ni sehemu ya kukuza uchumi na kujiletea maendeleo kwa sababu ni raslimali muhimu,” anasema.


Kama zilivyo nchi zingine duniani, Zeyana anasema pia kwa Zanzibar ardhi ni chanzo kikuu cha uzalishaji mali na uingizaji mapato kupitia sekta mbali mbali ikiwemo kilimo, utalii, uwekezaji na biashara.


Anasema idadi ya wanawake Zanzibar ni asilimia 51% ya watu wote visiwani humo, ambapo asilimia 20 tu ndiyo wanamiliki ardhi. 


“Sisi wanawake wanaharakati ikiwemo  vikundi vya mtandao wa ardhi Zanzibar,  tunaitaka serikali kuondoa urasimu ambao ni kikwazo  kwa wanawake kumiliki ardhi.

Wanawake wanao uwezo wa kutumia vema ardhi kwa kilimo, uwekezaji na biashara mbalimbali ili kuwawezesha kuondokana na umaskini,” anasema.

Anaeleza kwamba urasimu wa upatikanaji hatimiliki za ardhi kwa wanawake visiwani humo, huwavunja moyo wananchi wenye nia ya kumiliki raslimali hiyo.

Kwa mfano, anasema urasimu huo huwavunja zaidi moyo wanawake  wanaoishi vijijini, ambao kimsingi hawana uelewa wa namna ya kupata hatimiliki hizo.


‘Taasisi zinazoshughulikia hatimiliki zinatakiwa kuweka utaratibu mzuri na rahisi utakaotoa fursa zaidi kwa watu waliopo vijijini kupata hatimiliki hizo kwa urahisi,” anasema.


Anatoa mfano kwamba ilimgharimu takriban mwaka mmoja na miezi mitatu kupata hatimiliki kupitia idara mbali mbali za serikali, hatimaye alifanikiwa.


Hata hivyo, anasema tangu kupata hatimiliki hiyo, shamba lake lenye ukubwa wa hekta tatu kwa sasa lipo salama, waliovamia awali na kujenga nyumba hivi sasa wamehama baada ya ya kuthibitishiwa kwamba eneo hilo siyo mali yao halali.

Amina Iddi, mkazi wa Bambi, Wilaya ya Kati Unguja anasema ameanza mchakato wa kutafuta hatimiliki katika shamba la familia yao, lakini anakiri kuwepo kwa mlolongo wa utaratibu husika.

“Tunaiomba serikali iweke utaratibu utakaotoa nafuu kwa wananchi hususan sisi wanawake tunaotoka kvijijini, kwani  tumehamasika kuwa na hatimiliki ya ardhi kwa mashamba yetu”, anasema.

Mwanasheria aliyewahi kuwa mjumbe wa bodi ya ardhi, Miza Haji, akieleza kuhusu tatizo la wanawake kushindwa kumiliki ardhi kwa matumizi ya kilimo, makazi na uwekezaji, anaiomba serikali kuweka utaratibu mzuri namna wanawake wanavyoweza kufanikiwa katika suala hilo.


Anasema katiba ya Zanzibar inatoa nafasi sawa kwa wananchi wote ikiwemo wanawake na wanaume kumiliki ardhi kwa shughuli mbali mbali, licha ya kukabiliwa na vikwazo vya gharama za juu zinazotozwa kupata hatimiliki.


Wanaharakati na wanawake kwa jumla wameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupunguza urasimu katika upatikanaji wa hatimiliki kwa wanaohitaji  kumiliki ardhi.


Katibu wa Mtandao wa Ardhi Wilaya ya Kati, Unguja, Bahati Suleiman, amekiri kuwepo kwa urasimu mkubwa kuanzia ngazi za shehia hadi Wilaya ambapo wanawake hushindwa kumudu gharama husika.


Anasema bado jamii haina uelewa wa kutosha kujua kiwango cha fedha kinachotozwa kwa ajili ya usajili wa ardhi katika ngazi ya shehia, hali inayosababisha baadhi ya masheha kutoza fedha nyingi.


“Baadhi ya masheha wamekuwa kikwazo katika kupata hatimiliki za ardhi kwa sababu wamekuwa wakitoza fedha nyingi kinyume na utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria,” anasema.Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Zanzibar, kwa  ufadhili wa Foundation Civil Society (FCS), Shirika la Maendeleo la Canada (CFLI) linalosaidia wanawake, wanatekeleza mradi wa kuwahamasisha wanawake kumiliki ardhi kwa ajili ya shughuli za uchumi.


Ofisa Mwandamizi wa TAMWA, Asha Abdi,  anawataka wanawake kujitokeza kutafuta hatimiliki bila ya kujali kiasi cha fedha kilichowekwa, kwani thamani ya ardhi kwa maisha ya binaadamu hivi sasa ni kubwa.


Kwa mfano, anasema wanawake katika mwaka mmoja huchangia zaidi ya sh. 300,000 harusini na katika shughuli zingine zisizo na tija, tofauti na kumiliki ardhi kwa ajili ya maisha yako.


“Wanawake tusibabaishwe na kiwango cha sh. 280,000 kilichowekwa kwa ajili ya kupata hatimiliki, ambayo haina tija tofauti na kupata hatimiliki ya ardhi,” anasema.


Imebainika kuwepo kwa jumla ya sheria sita zinazohusiana na mambo ya ardhi lakini hazizungumzii masuala ya umiliki wa ardhi kwa wanawake.


Mwaka 2015 Wilaya ya Kati pekee iliripoti jumla ya kesi za migogoro ya ardhi 132 na  mwaka 2016 kesi 88 zilifikishwa katika ngazi ya wilaya hiyo.


“Wanawake bado wanadhalilika katika masuala ya ardhi, hivyo serikali inatakiwa kutoa elimu zaidi na kuweka mfumo wa upatikanaji hatimiliki,” anasema Asha.


Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud, anazitaka taasizi zinazosimamia na kushughulikia masuala ya ardhi ikiwemo kamisheni ya ardhi, kuweka utaratibu unaoeleweka ili jamii iepukane na usumbufu wa kumiliki ardhi.


Kwa mfano, anasema wakati umefika kuweka kifungu cha sheria kitakachozingatia umuhimu wa mwanamke katika ugawaji wa ardhi, kwa mgao wa asilimia 20 kama ilivyo nchi zingine ikiwemo Zimbabwe.


Anasema katika marekebisho ya sera ya ardhi, ipo haja ya kuweka kifungu  kitakachozingatia masuala ya uhaulishaji wa ardhi ambao umefanywa na mwanamme basi mkewe naye anatakiwa kwanza kuridhia ili kutoa baraka hizo.


“Tunataka sheria ya ardhi itakayozingatia usawa wa jinsia ili wanawamke wawe na fursa na uwezo wa kumiliki mali na nguvu ya uamuzi katika suala hilo ndani ya  ndoa”, anasema.  


Sheria za ardhi zilizopo zinao mlolongo  mrefu na urasimu ambao huwafanya wanawake kushindwa kupata hatimiliki na uhaulishaji wa ardhi,” anasema.


Hivi karibuni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, alizungumza na watendaji wa Wizara ya Ardhi na kuwataka kuongeza kasi ya upimaji ardhi, ikiwa ni miongoni mwa hatua za kupambana na migogoro ya ardhi nchini. 


No comments