Breaking News

USIYOYAJUA KUHUSU MINYOO WANAWEZA KUISHI MIAKA 30

NA MWANDISHI WETU

WANASAYANSI wa Marekani wamegundua kuwa minyoo wenye umbo la neli, wanaoishi kwenye bahari yenye kina kirefu katika ghuba ya Mexico, wanaweza kufikia umri wa miaka 300.Pia, wamesema minyoo hao wakipata chakula cha kutosha, wanaweza kuishi kwa miaka mingi zaidi.

Minyoo hao, ambao hujificha kwenye neli zao, wanaonekana kama mimea yenye vichaka vingi,  inayokua juu ya miamba au mchanga.

Mazingira ya bahari yenye kina kirefu ni salama kwa minyoo hao kwani hakuna maadui wengi. 

Kabla ya hapo, wanasayansi waligundua kuwa, minyoo wenye umri wa miaka 250, huishi katika kina chenye mita 300 hadi mita 950, katika ghuba ya Mexico. 

Hivi karibuni, wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Temple cha Marekani, wametafiti minyoo wa aina nyingine, wanaoishi katika kina chenye urefu wa kilomita moja hadi tatu na kugundua kuwa, wana maisha marefu zaidi, ambao baadhi wana umri wa zaidi ya miaka 300. 

Hadi sasa rekodi ya mnyama mwenye uti wa mgongo kwenye nchi kavu, aliyeishi maisha marefu zaidi ni kobe mkubwa, aliyeishi katika visiwa vya Galapagos, mwenye umri wa miaka 177 na mamalia, aliyeishi maisha marefu zaidi ni nyangumi mwenye kichwa kinachofanana na pinde, mwenye umri wa miaka 211.

Mnyama mwenye umri mkubwa zaidi ni chaza wa Actic, mwenye umri wa miaka 507.

mwisho


Damu ya bui bahari inasukumwa

na utumbo badala ya moyo


KWA wanyama wengi duniani, damu inasukumwa na moyo, lakini bui bahari  ni tofauti kabisa. Kazi hiyo kimsingi inafanywa na utumbo badala ya moyo. 

 Bui bahari ni mdudu anayefanana na bui. Ana mwili mdogo na mwembamba, miguu mirefu na myembamba, anaishi pwani na kuvuta hewa ya oxygen kutoka maji ya bahari kupitia ngozi yake. 


Wanasayansi wa tawi la Missoula la Chuo Kikuu cha Montana, wametoa ripoti kwenye gazeti la Current Biology, wakisema tofauti na binadamu, utumbo wa bui bahari uko mwilini kote, hadi kwenye kila mguu na unafanana zaidi na mfumo wa mzunguko wa damu. 


Viumbe vinavyoishi katika ncha za dunia huwa vikubwa zaidi kuliko vile vinavyoishi katika ukanda wenye halijoto ya wastani au ukanda wa tropiki. Hivyo wanasayansi walipofanya uchunguzi katika Bara la Antarctic, wamechunguza bui bahari wakubwa wa huko, ili kujua jinsi wanavyovuta hewa ya oxygen. 


Uchunguzi na majaribio, unaonyesha kuwa moyo wa bui bahari ni dhaifu, hauna uwezo wa kusukuma damu hadi miguuni, lakini utumbo wake una uwezo kubwa ya kumeng'enya chakula na kupeleka damu na hewa ya oxygen mwilini kote. 


Watafiti wanasema utumbo wa kipekee wa bui bahari unaonyesha kuwa, mabadiliko tofauti yametokea kwenye wanyama mbalimbali ili kutatua matatizo yao.

mwisho

Mafuta meupe huhifadhi nishati

 ya kahawia kuzalisha  joto

MAFUTA meupe ndani ya miili wa binadamu yanatumiwa kuhifadhi nishati na mafuta ya kahawia yanatumiwa kuzalisha joto. 

 Kwa watu wanene, kuyafanya mafuta ya kahawia yazalishe joto jingi zaidi kunasaidia kupunguza uzito.  Watafiti wa Chuo Kikuu cha Leipzig cha Ujerumani,  wamegundua njia mpya ya kupunguza uzito kwa kupunguza mafuta kahawia. 

Katika miaka mingi iliyopita, wanasayansi waliona mafuta ya kahawia yanafanya kazi nyingi zaidi katika miili ya watoto, lakini utafiti uliofanywa katika miaka ya hivi karibuni, unaonyesha kuwa, mafuta ya kahawia ndani ya miili ya watu wazima pia yanaweza kuamshwa, na baadhi ya mafuta meupe yanaweza kubadilishwa kuwa kahawia.

Watafiti walipofanya majaribio kwa kutumia panya, wamegundua kuna kemikali iitwayo Phosphodiesterase 10A ndani ya mafuta ya mwilini.

 Kazi ya kemikali hiyo ikizuiliwa, mafuta ya kahawia yataamshwa, baadhi ya mafuta meupe yanabadilika kuwa kahawia, uzito wa panya utapungua kwa kiasi kikubwa na uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari utapungua.

mwisho


Zifahamu njia zitazokuepusha kukoroma 

WATU wengi wana tabia ya kukoroma wanapolala, lakini kukoroma siyo kuzuri sana kwani familia yako pengine inaweza kushindwa kupata usingizi vizuri, kutokana na makelele unayoyatengeneza. Kwa upande mwingine, kukoroma kunamaanisha kuwa pumzi zako haziko sawa. Baadhi ya wakati kukoroma kunaweza kusababisha kukosa pumzi na kifo.

Hizi ndizo njia zinazoweza kubadilisha hali hiyo:
Kwanza ni kuchagua mito laini na inayoweza kufanya shingo yako iwe vizuri, ambayo itasaidia kupumua.

Pili ni kutumia mashine ya (humidifier) ili hewa ndani ya chumba iwe ya unyevu na kuepuka koo lako kuwa kavu; 

Tatu, kunywa asali kidogo kulainisha koo lako na usinywe pombe kwani inapandisha shinikizo lako la damu na kubana koo lako pamoja na kuzuia pumzi. 

Nne, ni kufanya mazoezi mara kwa mara.

mwisho


Hali ya hewa  haitakuwa na unyevu

kwa kipindi cha miaka 10,000 ijayo


WATAFITI wa Chuo Kikuu cha Miami cha Marekani, wamegundua mabadiliko ya hali ya hewa katika miaka mingi iliyopita, huko Mashariki ya Kati kwa kuchambua mawe ya chokaa pangoni nchini Iran na kukadiria kuwa, hali ya hewa ya ukanda huo  haitakuwa na unyevu ndani ya miaka 10,000.

Kutokana na utafiti huo, inadaiwa kuwa hata mvua zinaweza kuendelea kupungua katika kanda hiyo, kutokana na athari ya mzingo wa dunia kutokana na kiasi cha mwanga wa jua unaopatikana katika sehemu ya kaskazini ya dunia. 
 Mawe ya chokaa mapangoni yanaundwa na Calcium Carbonate ya majini. Kama mazingira yanafaa, kemikali kwenye mawe hayo zinaweza kuonyesha mabadiliko ya hali ya hewa katika kanda fulani. 

Pia, watafiti wamegundua kuwa, kiasi cha tufani kwenye Bahari ya Mediterranean kinahusiana na kiasi cha mwanga wa jua unaopatikana kwenye kanda hiyo.

Wakati kiasi cha mwanga wa jua kinapoongezeka, tufani zitaleta mvua nyingi zaidi katika mashariki ya kati. 

Jambo linaloathiri kiasi cha mwanga wa jua ni mabadiliko ya mzingo wa dunia na kwamba, mzingo wa dunia umeamua hali ya hewa ya kanda hiyo iwe ya unyevu katika miaka 10,000 ijayo.
Mafuriko makubwa kutokea baada ya miaka 50


WANASAYANSI nchini Marekani wanasema kuongezeka kwa joto duniani kutasababisha kuinuka kwa usawa wa bahari, na ifikapo mwaka 2050, upo uwezekano wa kutokea kwa mafuriko makubwa, ambayo hivi sasa kwa wastani, yanatokea kila baada ya miaka 50. 


 Kikundi cha utafiti cha tawi la Chicago la Chuo Kikuu cha Linois cha Marekani, kimetoa makadirio hayo kwenye gazeti la Scientific Reports la Uingereza, baada ya kuchambua athari ya mambo mbalimbali, yakiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, mawimbi, dhoruba na shinikizo dogo la hewa. 

Wanasayansi wengi wanaona kuwa, kuongezeka kwa joto duniani kutasababisha barafu kuyeyuka na usawa wa bahari duniani utainuka kwa sentimita 10 hadi 20, katika makumi ya miaka ijayo. 

Kiongozi wa kikundi hicho cha utafiti, Profesa Sean Vitousek, anasema usawa wa bahari ukiinuka kwa sentimita tano, miji ya Mumbai na Gorge nchini India na Abidjan nchini Cote d'Ivoire, itakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya mafuriko na ukiinuka kwa sentimita 10, miji ya Shanghai, London na New York pia itaathiriwa na mafuriko. 

Profesa Vitousek anasema, hatua za kukabiliana na mafuriko ni pamoja na kuhamisha miji ya pwani na kutenga fedha nyingi katika ujenzi wa miradi ya kukinga mafuriko pwani.

No comments