Breaking News

UVIMBE TUMBONI HUSABABISHA MIMBA KUHARIBIKA


Uvimbe tumboni husababisha mimba kuharibika, mtoto kuzaliwa njiti

NA MWANDISHI WETU.

TUNANDELEA na mfululizo wa tatizo la ugumba kwa wanawake, kama inavyoelezewa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Dk. James Chapa wa Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam.

vyakula vinavyoshauriwa na wataalamu dhidi ya kinga ya maradhi mwilini
Anataja sababu zinazochangia tatizo hilo kuwa ni pamoja na ugonjwa unaoathiri mfumo wa upevushaji mayai na kusababisha ugumba unaoitwa ‘Polycystic Ovarian Syndrome’  (PCOS).

Athari hii hutokea baada ya mifuko ya mayai kuwa na vivimbe vidogo ambavyo huzalisha kiasi kikubwa cha vichocheo vya kiume, hivyo kusababisha mzunguko wa hedhi pamoja na uenguaji wa mayai kuathirika na kupelekea tatizo la ugumba.

Dk. Chapa anataja dalili kwa wanawake wenye tatizo hili kuwa ni kutokuwa na mpangilio mzuri wa hedhi, kuongezeka uzito kusiko kwa kawaida na kuota nywele nyingi mwilini.

Dalili zingine ni kutokwa na chunusi, kukosa hamu ya tendo la ndoa, kutopata usingizi wa kutosha, uchovu, mabaka meusi mwilini, kushuka moyo na wasiwasi mwingi.

“Nawashauri wenye dalili hizo, kuwaona wataalamu wa afya hususan mabingwa wa magonjwa ya kina mama mapema, kwani wakiwahi wanaweza kushika mimba.

Anataja uvimbe katika tumbo la uzazi la mwanamke kuwa huota na  kukandamiza mirija ya uzazi, jambo linalosababisha kushindwa kupitisha mayai na kutobeba mimba.

Anasema uvimbe huo pia unaweza kusababisha mimba iliyotungwa kuharibika au mama kuzaa mtoto njiti.
Matibabu yake ni upasuaji na kuondolewa kwa uvimbe.

Makovu katika mji wa mimba ni tatizo ambalo daktari huyo anabainisha kwamba linaweza kusababishwa na kusafishwa kizazi na  upasuaji wowote unaohusisha kizazi ikiwemo kutoa uvimbe kwenye kizazi.

Sababu zingine ni magonjwa ikiwemo Kifua Kikuu (TB) na kichocho cha mji wa mimba ikiwemo utoaji mimba kwa njia ya kukwanguliwa kizazi.

“Mwanamke mwenye shida hiyo, hawezi kupata siku zake au akipata zitakuwa kidogo na anao uwezekano mdogo wa kushika mimba.
Hata hivyo, iwapo atashika mimba uwezekano wa kuharibika ni mkubwa kwa kuwa haiwezi kujishikiza vizuri kutokana na makovu katika kizazi,” anasema.

Anashauri kwamba, kwa mwanamke yoyote ambaye amewahi kusafishwa kizazi na ana dalili zilizotajwa, anaweza kumuona daktari kwa ajili ya vipimo na msaada, ili kujikwamua na tatizo hilo.

Kipimo ambacho mgonjwa hufanyiwa na ndicho kinatumika kugundua tatizo hilo kinaitwa ‘hysteroscopy’.

Anasema matibabu yake ni upasuaji kuondoa makovu, hata hivyo upasuaji huu huwa na mafanikio madogo katika maana ya kurudisha ufanyaji kazi wa kawaida wa mji wa mimba.

Matatizo mengine yanayosababisha ugumba
Dk. Chapa anaeleza kwamba ute mzito unaotoka katika shingo ya kizazi huweza kuzuia mbegu kupenya na ikiwemo kuzuia urutubishwaji wa  yai, hivyo kusababisha mimba kushindwa kutungwa.

Vile vile, hali ya mwili wa mwanamke kutengeneza kingamwili (antibodies) ambazo huweza kunashambulia mbegu za kiume.

Sababu ingine ya ugumba inaweza kutokana na matatizo ya kuzaliwa ya viungo vya uzazi.

 Anatoa mfano wa mwanamke kuzaliwa bila kuwa na baadhi ya viungo vya uzazi ikiwemo tumbo la uzazi, ama tumbo la kizazi lililogawanyika au lenye ukuta katikati.
Lakini pia baadhi ya wanawake huweza kuzaliwa na ukuta kwenye uke unaosababisha mbegu za mwanaume zisipenye kirahisi kwenda kwenye tumbo la uzazi.

“Msongo wa mawazo, kushuka moyo au wasiwasi uliopitiliza pia vyaweza kuathiri upevushaji wa mayai na hivyo kuathiri mfumo wa hedhi na uzazi kwa jumla,” anasema.
Uzito uliopitiliza kwa wanawake, daktari huyo anabainishwa kwamba ni miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha ugumba , ikiwemo magonjwa ya muda mrefu ambayo huathiri upevushaji wa mayai.

Namna ya kujikinga na ugumba
Mgonjwa mwenye maambukizi katika nyonga, anapaswa kuhakikisha anatibiwa mapema hususan magonjwa ya zinaa.

Kufanya ngono salama ili kuzuia maambukizi ya zinaa yanayoathiri mirija ya uzazi.

Daktari huyo anawaasa wanawake hususan walio katika umri au wanaokusudia kupata watoto kuhakikisha wanaepuka matumizi ya kupitiliza ya vilevi ikiwemo pombe na dawa za kulevya.

Hata hivyo, anasema kufanya mazoezi kupitiliza, pia huathiri uzazi, licha ya kutakiwa kuwa na uzito wa wastani, mazoezi yafanyike kwa kiasi.

Dk. Chapa anataja namna zingine za kujikinga na ugumba kuwa ni kuhakikisha mwanamke anapata lishe bora, usingizi wa kutosha na kuondoa msongo unaosababisha kushuka moyo.

Ili kukabiliana na hali ya msongo wa mawazo, anasema mgonjwa anapaswa kupata tiba ya dawa na kisaikolojia.

Hata hivyo, anasema mgonjwa anapaswa kuepuka mambo yanayoweza kumletea msongo wa mawazo ama kushuka moyo na wasiwasi uliopitiliza.

Dk. Chapa anawashauri wanawake hususan wanaotarajia ama kujiandaa kupata mimba, kuhakikisha wanafanya utaratibu wa kupima afya inayohusiana na uzazi.

Vile vile anawatakwa kuepuka matumizi holela ya dawa, vinginevyo kwa ushauri wa wataalamu wa afya.

Tahadhari
Ugumba unaweza kumpata hata mwanamke ambaye alishazaa, hivyo  upo ugumba kwa mwanamke hajawahi kushika mimba toka azaliwe na ule unaowapata kina mama waliowahi kushika mimba.

Dk. Chapa anasema kushika mimba au kwa wanawake wanaozaa, haimaanishi kwamba mtu anaweza kutopata ugumba baadaye.

Faith Julius, ni mama wa watoto watatu, anasema alipata changamoto wakati wa uzazi wa pili ambapo alichelewa kushika mimba na alipopata alijifungua mtoto mwenye tatizo la kichwa kujaa maji.

“Tatizo hilo lilinitesa, niliwasiliana na wataalamu mbalimbali wakati namtibia mwanangu, hata hivyo  walinishauri nitakapohitaji mtoto mwingine, kuhakikisha nakula chakula bora ikiwemo matunda na mboga kwa wingi, maziwa, samaki na dagaa ili kupata viinilishe muhimu mwilini,” anasema.

Anasema baadaye mtoto huyo alifariki. Alikaa muda wa miaka miwili akiwa na malengo ya kupata mtoto mwingine, hivyo alizingatia ushauri wa wataalamu wa afya wa kufanya maandalizi kabla ya kushika mimba.

Faith anasema alifanikiwa kupata ujauzito na kuzingatia ushauri wa afya wa kitaalamu na baadaye alijifungua mtoto mwenye afya njema.

Hivyo ni muhimu kuzingatia ushauri wa daktari huyu wa kuchunguza afya kila mara hususan kwa wanawake wanaotarajia kupata watoto sasa au baadaye na iwapo kuna tatizo, kushughulikia mapema.

Wiki ijayo tutaendelea na mada hii tika sehemu ya tano ambapo tutaangalia ugumba kwa upande wa wanaume.

No comments