Breaking News

WATALII WANAVYOSTAABISHWA NA MVUTO NA MAAJABU YA ZIWA NGOSI WILAYA YA RUNGWE-MBEYA KUTOKANA NA MUONEKANO WA KIPEKEE


 NA MWANDISHI WETU

TANZANIA ni moja ya nchi ambayo imebalikiwa kuwa na vivutio mbalimbali ambavyo hufanya wageni wa ndani na nje ya nchi kutembelea katika makala haya mwandishi Innocent   Ng’oko anaangazia maajabu ya ziwa Ngosi lililopo wilayani Rungwe-Mbeya.

ZIWA Ngosi ni moja ya maziwa yenye Mvuto wa aina  yake duniani ambayo yametokana na kulipuka kwa Volikano(maziwa ya kreta),ziwa hilo Lililopo Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya nchini Tanzania karibu na  kijiji cha Mbeye- one au mchangani umbali wa km 38 kutoka Mbeya Mjini na ni ziwa la pili kwa ukubwa Afrika baada ya ziwa lililopo Nchini  Ethiopia.


ziwa Ngosi ikiwa na muonekano kama ramani ya bara la afrika

Asili ya jina Ngosi linatokana na jina la kabila la Wasafwa linalomaanisha kitu kikubwa ‘’LIGOSI’’ na ziwa hilo tangu zamani linatajwa kuwa lilikuwa chini ya himaya ya kabila la wasafwa katika koo mbili za machifu akiwemo ya Chifu Mrotwa Mwalingo (akitawala upande wa magharibi) na chifu Mlotwa Mwalupindi(aliyekuwa akitawala upande wa Mashariki).

Mbali na Ziwa Ngosi kuwa na simulizi za aina mbalimbali ziwa hilo  lipo usawa wa mita 2620 kutoka usawa wa bahari na limezungukwa na misitu minene ya asili katika safu za milima ya Uporoto yenye hekari 9,332 ambayo zimetengwa kwajili ya uhifadhi wa eneo hilo.
Ndani ya ziwa Ngozi kuna visiwa viwili vinavyovutia sana kwa muonekano na inatajwa visiwa hivyo vimekuwa vikitumiwa kwajili ya mazalia yandege wa aina mbalimbali wakiwemo  bata pori.

Ziwa hilo lina kina cha mita 74 na urefu wa kilometa 2.5 pamoja na upana wa kilometa 1.5 na eneo lake ni km za eneo 3, na pembezoni mwa ziwa hilo kuna mabonde makubwa yenye misitu mikubwa ya miti ya asili na baadhi ya mimea hiyo ni migomba ya asili, mianzi ya asili pamoja na miti mirefu na miti yenye maua ya aina mbalimbali.


Wakati wa kwenda kulifikia ziwa hilo kuna njia nyembamba iliyotengenezwa kwa umahili mkubwa wakati wa kupandisha mwinuko huo kuelekea ziwa Ngosi,na ukiwa njiani ni kawaida kusikia milio ya ndege wa aina mbalimali pamoja na ngedere ingawa si rahisi sana kuwaona kutokana na misitu minene ya asili yenye miti mirefu na mabonde yenye muonekano wa aina yake.

Unapofika eneo la Ziwa Ngosi utastajabu kuona  umbo la ziwa hilo lenye muonekano unaofanana na ramani ya Afrika na ndani yake likiwa na visiwa viwili , na katika msitu unaolizunguka ziwa hilo kuna  viumbe wanaoweza kuonekana ambao ni nyani aina ya Mbega, ndege wa aina mbalimbali, Vinyonga wa pembe tatu na wanyama wengine wadogo wadogo.
Muonekano wa ziwa Ngozi unavutia sana bila kukuchosha wakati wa kulitazama ,ingawa ni kawaida kwa ukungu kutawala sehemu kubwa ya eneo la ziwa hilo kwa siku na kiwango cha joto katika eneo hilo ni kati 18 °C.
Maajabu mengine ni kuwa maji ya Ziwa Ngosi huonekana kama yakibadilika rangi kutokana na hali ya hewa wakati wa jua,mawingu na ukungu  na  maji huonekana kama yenye  rangi zikiwemo za  za Bluu,nyeupe na nyeusi kiasi , na ikumbukwe kuwa ziwa hilo lipo juu ya mwinuko unaofanana na kilima  na baada ya kufika katika kilima hicho ziwa hilo huonekana kwa upande wa chini sana  kutoka sehemu uliyosimama.
Ni mwendo wa takribani saa moja kuyafikia maji ya ziwa hilo na ikumbukwe  kuna awamu tatu za mitelemko ndani ya gema la ziwa hilo ,ambapo mtelemko wa kwanza ni mkali sana kutoka juu ya usawa wa ziwa hilo,mtelemko wa pili kuna tambalale kiasi yenye vichaka miti mirefu sana na mianzi ya asili,na mtelemko wa tatu na wa mwisho ni mkali na wenye misitu mikubwa mabonde ya aina yake.

Na unapofika chini na kulifikia ziwa hilo utastaajabishwa njisi ziwa hilo lilivyo kutokana na maji yake kuwa na radha ya chimvichumvi,ndege wanao ogelea na kuruka ndani ya ziwa hilo na muonekano wa karibu kabisa wa visiwa viwili ndani ya ziwa hilo,ni ziwa linaloonekana kuwa na kina kirefu sana kwa muonekano.

Kwa karibu  maji  hayo  huonekana kuwa na rangi ya kijani na rangi ya bluu kwa mbali na ukiyachota maji hayo ni maji meupe sana na yenye uvuguvugu wenyeji wengi wanaoishi karibu na ziwa hilo huyatumia maji hayo kwajili ya imani za kimila.

Na umbali wa kupandisha kutoka chini ya ziwa hilo hadi juu ya usawa wa ziwa hilo ni zaidi ya saa 1:45 kwa miguu na ni ziwa la kipekee sana lenye mvuto wa aina yake na wakati wa kushusha na kupadisha ni jambo la kawaida kutawaliwa na ukungu wa mara kwa mara unaoambatana na kijibaridi.

Tafiti za kitaalamu zinaonyesha kuwa ziwa hilo lina uwezo wa kuzalisha nguvu ya umeme kutokana na maji ya ziwa hilo kuwa na joto kubwa la kati ya nyuzi 230-250 °C  na muonekano wa ziwa Ngosi unavutia sana bila kukuchosha kwa mtu yeyote anayefika na kulitazama.

Katika eneo la ziwa ngosi ni kawaida kwa ukungu kutawala sehemu kubwa ya eneo la  ziwa na muda mzuri wa kuweza kuliona ziwa hilo ni kati ya saa 5 asubuhi na kuna wakati ziwa hilo ni vigumu kuliona ukiwa upande wa juu kutokana na hali ya ukungu  ambao hutawala katika eneo hilo na wastani cha joto katika eneo hilo ni kati 18 °C

Mbali na ziwa Ngosi kuna maziwa mengine madogo sana yenye asili ya volkano yaliyopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya ambayo ni Kisiba, Chungululu,Ikapu, Itamba, Masoko, Ilamba,Ndwati, Katubwi Itende,Lusanje na Kingili.na mzaiwa mengine ni ziwa a Chala( Dschalla) ambalo lipo nje kidogo ya mjini Moshi.

Afisa Utalii halmashauri ya wilaya ya Rungwe,Numwagile Bugali anakili kuwa  wilaya ya Rungwe imebalikiwa kuwa na vivutio vingi sana na hivyo kufanya wilaya hiyo kutembelewa mara kwa mara na wageni wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujionea vivutio hivyo vyenye mvuto wa kipekee na wa aina yake.

Numwagile anabainisha kuwa miongoni mwa vivutio hivyo  vilivyopo ndani ya halmashauri ya wilaya Rungwe  ni Hifadhi Asilia ya Mlima Rungwe, Maporomoko ya Maji (kapologwe,Malasusa,Malamba n.k), Daraja la Mungu, Kijungu, Maziwa ya Volkano (Ngosi,Kisiba,Ndwatin.k), Majengo ya kale, Nyumba ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere pamoja na maeneo mengine mengi yenye fursa za uwekezaji na yanayovutia hisia za watu ukiwemo  Mti wa Maajabu wa Katembo.

Anasema uwepo wa fursa hizo za  uwekezaji ni fursa za kipekee katika mambo ya uchumi ikiwemo kufua umeme kwa kutumia  maporomoko ya Maji,meme wa Joto Ardhi katika maeneo yenye volcano zikiwemo  Ziwa Ngosi,Uwepo wa Madini, gesi na Makaa ya Mawe,huduma za utalii (Hoteli, Migawaha ya Kitalii,kambi za utalii nk ) katika maeneo ya vivutio vya utalii.

Mbali na  umarufu wa ziwa Ngosi na ziwa challa nchini Tanzania pia kuna Maziwa makubwa mengine duniani yenye muundo wa ziwa Ngosi ambayo ni ziwa Toba linalopatikana eneo la Sumatra nchini , Indonesia ndiyo ziwa pekee duniani linaloongoza kwa ukubwa lina urefu wa Kilometa 100 na upana wa kilometa 30 na eneo ni km za eneo 1,130 na kina ni mita 500.

Maziwa mengine ni Pinatubo linalopatikana nchini Ufilipino lina kina cha mita 600 na upana wa km 2.5 na ziwa Heaven linalopatikana Korea ya Kaskazini lina Urefu wa mita 213 na eneo la Km 9.82,maziwa mengine ni IRAZÚ nchini Costa Rica,Cuicocha, nchini Ecuador na mengineyo.

picha 1,muonekano wa ziwa Ngosi kwa upande wa juu.

picha 2,mwandishi wa makala haya baada ya kufika katika ziwa hilo na picha namba tatu ni ndani ya ziwa Ngosi.  

No comments