Breaking News

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AWATAKA WABUNIFU MAJENGO NA WAKADILIAJI MAJENZI KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa aipokea ngao ya shukurani kutoka  kwa Mwenyekiti  wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, Dk. Ludigija Bulamile baada ya kufungua semina endelevu ya 29 ya Bodi hiyo  kwenye ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo


NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi wajiepushe na vitendo vya rushwa ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inalingana na thamani ya fedha inayotumika.
’’Epukeni vitendo vya rushwa ambavyo huisababishia Serikali hasara kubwa na kuleta usumbufu kwa wananchi. Ni matumaini yangu kuwa mtafanya kazi kwa weledi na kufuata maadili ya taaluma zenu’’, alisema. 
 Alitoa onyo hilo leo wakati akifungua semina endelevu ya 29 ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, iliyofanyika Jijini hapa.
Alisema wataalamu hao ni vema wakahakikisha majengo wanayobuni yanakuwa  bora katika muonekano na mandhari yake iwe yenye kuvutia na yenye kuzingatia utunzaji wa mazingira na matumizi bora na endelevu ya nishati.
 Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kwa kuchagua mada inayohusu jukumu la wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi katika kuendeleza viwanda hapa nchini.
 Alisema anatambua kuwa ujenzi wa viwanda unaendana na ujenzi wa miundombinu kama majengo, barabara, madaraja, miundombinu ya nishati na viwanja vya ndege, ambayo ni muhimu katika kuimarisha uchumi wa viwanda. 
 ’’Hivyo, wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi mna mchango mkubwa sana katika kufikia uchumi wa viwanda. Nitoe rai kwa Bodi ihakikishe kuwa miradi yote ya majengo pamoja na miundombinu mingine inashirikisha wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi katika ubunifu na usimamizi wa ujenzi wake,’’ alisema Majaliwa.
 Katika hatua nyingine, Majaliwa alizitaka taasisi za Serikali na waendelezaji binafsi wahakikishe wanatunza majengo ya kale, kama Sheria ya Mambo ya Kale inavyoelekeza.
 Alisema nchi nyingi duniani zinaenzi majengo ya kale, ambayo yanatoa taswira ya nchi husika, ambapo kasi ya ukuaji wa sekta ya ujenzi hapa nchini haiwezi kuondoa dhana hiyo. 
 ’’Kwa msingi huo, napenda kusisitiza kuwa taasisi za Serikali na waendelezaji binafsi, wote wanapaswa kutunza majengo ya kale, kama Sheria ya Mambo ya Kale inavyoelekeza’’. 
 Alisema,  jambo la muhimu ni kutoa elimu  ili wananchi waelewe umuhimu wa kutunza historia ya nchi yao kwa kupitia majengo ya kale ambayo pia yanaweza kuwa chanzo cha mapato kwa Serikali kupitia sekta ya utalii.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akioneshwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa, Makame Mbarawa mashine 10 za kufyatua matofali alizokabidhiwa na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kabla ya kufungua semina ya Bodi hiyo kwenye ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo. Mashine hizo zitagawiwa bure kwa vikundi vinavyojishugulisha na ufyatuaji matofali. Watatu kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge na wannel ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Joseph Nyamhanga.
  WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza  kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufungua semina endelevu  ya 29 ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu  Majengo na Wakadiriaji Majenzi.
BAADHI ya washiriki wa   semina endelevu  ya 29 ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu  Majengo na Wakadiriaji Majenzi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua semina hiyo.
MAJALIWA akipata maelezo kutoka kwa Ofisa Mauzo wa Kampuni ya  Locks and Systems Limited ya Dar es salaam, Linda Mwamukonda kuhusu vitasa, bawaba na milango ya kielektroniki wakati alipotembelea banda la kampuni hiyo katika maonyesho yaliyoandaliwa na Bodi hiyoi kwenye viwanja vya Hazina jijini Dodoma,
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa akifungua semina hiyo.
WAZIRI  Mkuu, Kassim Majaliwa  akiagana na viongozi walioshiriki katika semina endelevu ya 29 ya Bodi hiyo. Kutoka kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano, Profesa, Makame Mbarawa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi, Joseph Nyamhanga na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi Dk. Ludigija  Butamile.(Picha zote na ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments