Breaking News

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA MAABARA YA KUPIMA MADINI. Ni ya kwanza Afrika, inauwezo wa kutambua aina za madini na yalikotoka.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amezindua maabara ya kisasa ya na ya kwanza barani Afrika yenye uwezo wa kupima na kutambua aina mbalimbali za madini.

Akizindua maabara hiyo, Majaliwa, alisema itasaidia kupunguza migogoro ya umiliki wa madini na kudhibiti utoroshwaji wa madini mbalimbali kati ya nchi moja na nyingine.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa 38 wa Mawaziri wa Madini  kutoka nchi wananchama wa Ukanda wa  Maziwa Makuu kwenye   Kituo cha Utafiti  na Uendelezaji wa Sekta ya Madini, Kundichi Jijini Dar es salaam, juzi.

Maabara hiyo ilifunguliwa katika Kituo cha Madini na Jiosayansi  cha Afrika  (AMGC) kilichopo Kunduchi Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu alisema uzinduzi wa maabara hiyo utawezesha wataalamu kutambua aina za madini na nchi yanakotoka, hivyo kuondoa migogoro ya umiliki wake. 

“Maabara hii litatuweza kulinda madini yetu na kufanya biashara ya madini vizuri. Pia hii ni fursa nzuri kwa nchi za Afrika kutumia maabara hii kupima madini yao na kubaini yalikotoka,” alisema.
 
MAJALIWA, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi  kutoka nchi wanachama wa Ukanda wa   Maziwa Makuu baada ya kufungua Mkutano 38 wa  Mawaziri wa Madini kutoka nchi hizo kwenye Kituo cha utafiti na uendelezaji wa sekta ya Madini, Kunduchi Jijini Dar es salam, juzi. Watatu kulia ni Waziri wa Madini, Angela Kairuki. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Hata hivyo, aliwataka viongozi wa kituo hicho kuhakikisha wanaziwesha nchi wanachama kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya madini pindi zinapohitaji.

Aidha, Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia katika ununuzi wa vifaa vya maabara hiyo pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu watakaoiendesha.

Pia, aliiomba Serikali hiyo kutoa mafunzo hayo kwa Watanzania wengi zaidi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa kuendesha maabara hiyo.
 

MENEJA Maabara ya Kemia na Mazingira wa Kituo cha Utafiti na Uendelezaji wa Sekta  ya Madini, Charles Butete, akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Majaliwa,  baada ya kuzindua maabara hiyo. Wapili kushoto ni Waziri wa Madini, Angela Kairuki.


Wakati huo huo, Waziri Mkuu alipata fursa ya kufungua Mkutano 38 wa Mawaziri wa Madini kutoka nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika katika kituo cha AMGC.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ikiwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama zilizosheheni wanyama wa aina mbalimbali pamoja na fukwe za bahari.
 
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua Mkutano wa 38 wa  Mawaziri wa Madini kutoka nchi wanachama wa Ukanda wa  Maziwa Makuu kwenye Kituo cha Utafiti na Uendelezaji wa Sekta ya Madini, Kunduchi Jijini Dar es salam, juzi.

No comments