Breaking News

CHUO CHA AFYA CHA ZSH CHATOA PONGEZI KWA SERIKALI YA MAPINDUZI.
Na Mwandishi Wetu.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea  pongezi kutoka kwa Uongozi wa Chuo cha Afya kwa Mchina Mwanzo {Zanzibar School of Healthy –ZSH}  kwa kitendo cha Kihistoria kilicho kamilika hivi karibu pale ambapo Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia {PSA} ulisainiwa rasmi  baina  yake na Kampuni ya Kimataifa ya RAKGAS ya Nchini Ras Al – Khaimah.
Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar School of Healthy Bibi Aziza Hemed alitoa pongezi hizo kwa niaba ya Uongozi wa Chuo chake wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuelezea malengo ya Chuo kicho ya kutaka kutanua wigo wa mafunzo mengine Chuoni hapo.
Bi Aziza Hemed alisema Wananchi waliowengi Nchini wamejenga matumaini makubwa yakionyesha mwanzo mwema wa Taifa kuendelea kufungua zaidi fursa za Kiuchumi na ustawiwa Jamii.
Alisema wakati dalili za matarajio ya kuongezeka kwa ajira kupitia Sekta hiyo Mpya Nchini inaanza kutoa mwanga, Wananchi hasa Wanafunzi wanapaswa kuendelea kushirikiana na Serikali katika mtazamo wa kujikita zaidi katika Masomo ya Sayansi kwa nia ya kujiweka sambamba na Mradi huo Mpya Nchini.
Akizungumzia maendeleo ya chuo chake Mkurugenzi huyo wa Zanzibar School of Healthy alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2013 baada ya kupata baraka na kibali kutoka Nacte mwaka 2012 kufuatia kukamilisha taratibu zote za Chuo.
Alisema ushirikiano mkubwa uliyopata Uongozi wa Chuo hicho kutoka Serikalini umewezesha kuzalisha wahitimu zaidi ya 960 ambapo kwa mwaka hukadiria kuzalisha wahitimu 200 wenye vigezo na sifa zinazowawezesha kutoa huduma katika Hospitali na Vituo vya Afya Zanzibar na baadhi yao Tanzania Bara.
“ Najisikia raha na faraja ninapokwenda kutaka huduma za Afya ama iwe Hospitali kubwa au Vituo vya Afya nimekuwa nikikutana na Wanafunzi wangu wakija kunihudumia jambo ambalo napaswa kujivunia”. Alisema Bibi Aziza.


Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Chuo hicho kupitia Mkurugenzi wake huyo Mtendaji kutokana na uamuzi wake wa kuanzisha chuo hicho ikiwa ni jambo la msingi litaloendelea kuungwa mkono ya Serikali Kuu.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inahitaji kuimarisha Sekta ya Afya kwa kuongeza Hospitali na Vituo vya Afya Nchini  vitakavyohitaji Watendaji zaidi ili kutoa huduma bora kwa Wananchi wake.

No comments