BALOZI SEIF AIOMBA TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI TANZANIA {TAEC} KUANDAA MAFUNZO KWA WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI WANAOWAKILISHA WANANCHI KATIKA MAJIMBO YAO.
WATANZANIA lazima waendelee kubaki salama na afya
chini ya matumizi sahihi ya mionzi inayotokana na Teknolijia ya Nyuklia Duniani
ambapo kwa hapa nchini, yanaratibiwa na
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC}.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki
Tanzania, Profesa Lazaro Busagala, alisema hayo leo wakati akizungumza na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi, Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar
alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kuiongoza Taasisi hiyo ya
Teknolojia.
Profesa Busagala alisema, Tume hiyo
iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge Nambari 7 ya Mwaka 2003 kulingana na kifungu
nambari 6{1} cha sheria ya Atomiki imepewa jukumu la kudhibiti matumizi salama
ya mionzi, kuhamasisha na kupanua matumizi salama ya Teknolojia ya Nyuklia
pamoja na kutoa ushauri na taarifa tofauti za Kisayansi na Teknolojia ya
Nyuklia.
Alisema, udhibiti huo una lengo la kulinda
umma, wafanyakazi pamoja na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi, jukumu linalowapa mamlaka ya kufanya ukaguzi
wa vituo vitoavyo huduma ya mionzi nchini ili kujiridhisha na hali ya usalama.
Profesa Busagala, alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
kwamba zipo Hospitali 72 Nchini Tanzania zilizofungiwa kutoa huduma za mionzi
baada ya kubainika matatizo yanayosababisha kuathiri kwa wagonjwa wasiopungua
Laki 262,000 kwa mwaka.
Alisfafanua kuwa, ugonjwa wa Saratani
unaoibuka kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo zile za mionzi umeongezeka
kwa asilimia 30 hadi 40 katika kipindi
cha miaka mitatu iliyopita hali inayowafanya Wataalamu wa Tume hiyo kuwa makini
katika utekelezaji wa majukumu yao katika kusimamia udhitibi mzuri wa matumizi
ya mionzi.
Profesa Busagala, alisema matumizi ya Teknolojia ya Mionzi
Nchini, hivi sasa tayari yameibua
vianzio zaidi ya 700 vinavyotokana na huduma za hospitali, viwanda pamoja na
vifaa ya utengenezaji wa bara bara.
Akizungumzia masuala ya ufundi wa vifaa
vinavyotokana na mionzi, Busagala alisema tume ina maabala maalumu inayofanya
kazi ya kuratibu, kutoa huduma ya kudhibiti ubora wa vifaa vya nyuklia pamoja
na mafunzo ya ufundi.
Alisema wakati Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar tayari imesharidhia kuipatia Tume hiyo eneo la ujenzi wa maabara kwa
upande wa Zanzibar ili iendelee kutekeleza majukumu yake ya ufanisi mzuri zaidi
lengo la maabara hizo ni kuimarisha uwezo wa Taifa katika ufundi wa vifaa
vya nyuklia.
Kwa mujibu wa Busagala, baadhi ya huduma
zinazotolewa na maabara kufuatia maombi ya wadau mbali mbali ni pamoja na
matengenezo ya mashine za hospitali za X – Ray, vifaa vya kisayansi vinavyotumika
katika utafiti, Viwanda na Hospitali.
Kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika sekta
ya kilimo kwa matumizi bora ya mionzi, Busagala alisema lipo ongezeko kubwa la
uzalishaji katika kilimo cha Mpunga, Migomba, Mahindi na Shairi hatua iliyowapa
matumaini makubwa wakulima hasa upande wa Zanzibar.
Profesa Busagala alisema mafanikio hayo
yalikwenda sambamba na udhibiti wa maradhi mbali mbali kwenye mimea na matunda
yaliyokuwa yakisababishwa na wadudu Mbuno ambapo Zanzbar ilifanikiwa kupiga
vita maradhi hayo mnamo Mwaka 1998 baada ya upandishaji mbegu za kuzuia
ongezeko la wadudu hao chini ya utaalamu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani
{IAEA}.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe wa Viongozi wa Tume hiyo ya Nguvu
za Atomiki Tanzania kwamba jamii bado ina uelewa mdogo juu ya tafrisi sahihi ya
masuala ya nguvu za Atomiki.
Balozi Seif alisema watu wengi wana ufahamu wa
Atomiki na masuala yanayotokana na nguvu za Kijeshi wanazofikiria zinaweza
kuleta athari ya maangamizi wakati wowote iwapo wasimamizi wake watatumia
visivyo stahiki.
Alisema ipo haja ya wataalamu wa tume hiyo
kuendelea kutoa taaluma kwa jamii ili iondoe shaka sambamba na kujilinda na
masuala ya mionzi katika misingi halali inayokubalika kitaaluma.
Akielezea furaha yake kutokana na uelewa na
majukumu ya tume hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba uongozi wa
juu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC} kuandaa mafunzo kwa Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi wanaowakilisha Wananchi katika majimbo yao ili kwa hatua
za awali Taaluma ya Teknolojia ya Nuklia isambae kwa jamii nzima.
BALOZI Seif (kulia), akimkaribisha Busagala
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania yenye Makao
Makuu yake mjini Arusha iliyoanzishwa kwa sheria ya bunge namba 7 ya mwaka
2003, awali ilikuwa ikijuilikana kama Tume ya Taifa ya Mionzi iliyoanzishwa kwa
sheria ya bunge namba 5 ya mwaka 1983.
No comments