MAJALIWA ‘NIMERIDHISHWA NA MAENDELEO YA VIWADA’.
Na Mwandishi wetu.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema
amefarijika na maendeleo ya ujenzi wa viwanda kwenye mkoa wa Tanga kwa sababu
vitasaidia katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.
Aliyasema hayo jana jioni (Alhamisi,
Novemba 1, 2018) alipotembelea kiwanda cha saruji cha Rhino na kiwanda cha
maziwa cha Tanga Fresh, vyote vya jijini Tanga.
Waziri Mkuu ambaye jana alihitimisha
ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga, aliwapongeza wawekezaji wa
viwanda hivyo kwa kuunga mkono mkakati wa Serikali.
Alisema Serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kukuza uchumi kutoka wa
chini hadi wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda.
Akizungumzia kuhusu kiwanda cha Rhino,
Waziri Mkuu alisema kiwanda hicho na vingine vya saruji nchini vitasadia
kupunguza gharama ya saruji nchini na kurahisisha ujenzi.
“Serikali inaamini kwamba uwepo wa
viwanda mbalimbali nchini si tu utawezesha ukuaji wa uchumi wa Taifa, pia
utasaidia katika kumaliza changamoto ya ajira hususani kwa vijana.”
Akiwa katika kiwanda cha Tanga Fresh,
Waziri Mkuu aliwataka wafugaji mkoani Tanga wabadili mfumo wa ufugaji na wafuge
kwa kutumia njia za kisasa ili waongeze uzalishaji.
“Wafugaji lazima wakubali kubadilika
watumie fursa ya uwepo wa kiwanda hiki kwa kufuga kisasa ili wapate maziwa
mengi kwa sababu wana uhakika wa kuyauza kiwandani hapa”.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka
wananchi walioajiriwa kiwandani hapo wafanye kazi kwa bidii, uaminifu na wawe
waadilifu na wasijihusishe na vitendo vya wizi kwa kuwa havina tija.
No comments