MIAKA MITATU YA JPM TARURA YALETA FURAHA KWA WANANCHI WA BUKOBA.
Na Mwandishi Wetu, Bukoba
MIAKA mitatu ya Rais John Magufuli, madarakani inatajwa kuondoa
adha ya wananchi waliokuwa wanatembea umbali mrefu na kutozwa gharama kubwa ya
usafiri kutokana na uwepo wa miundombinu mibovu ya barabara katika Manispaa ya
Bukoba mkoani Kagera.
Hilo, limefanikiwa chini ya Wakala wa Barabara
za Mijini na Vijijini (TARURA), ambao imetengeneza barabara tatu kwa kiwango
cha lami ambazo ni barabara ya shirika la nyumba hadi kilimahewa, Kahororo hadi
Mugeza na barabara ya Kashura.
Akizungumza na Blog
hii, wilayani hapa, mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Savera Kamugisha,
alisema walikuwa wanapata shida kutumia barabara hizo hasa nyakati za mvua.
“Barabara hizi
mwanzoni licha na kuwa mbaya na kutopitika nyakati zote, ilikuwa inasababisha
ajali kutokana na kuwa nyembamba na hivyo, magari mawili kushindwa kupita kwa wakati
mmoja, lakini kwa sasa tuna furaha barabara hizi tunazitumia wakati wote na
kupunguza gharama za usafiri,” alisema mkazi huyo.
Diwani wa Kata ya
Bakoba Jimmy Mwakyoma, amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele
kulinda barabara zinazojengwa ili ziwe na manufaa kwao kwa muda mrefu.
“Mimi kama diwani nitahakikisha kupitia vikao vyetu tunaweka
mikakati ya kusimamia mapambano didi ya waharibifu
wa barabara hizi, tabu waliyokuwa
wanapata wananchi ni kubwa, hivyo ni wajibu wetu sasa kulinda na kutunza barabara
hizi ambazo zimetumia fehda nyingi hadi kukamilika kwake,”alisema diwani
Mwakyoma.
Nae diwani wa Kata ya Kashai, Kabaju Muruhuda Kabaju,
amewasisitiza madiwani kushirikiana na TARURA katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao ikiwemo miradi ya barabara ili
kuharakisha ukamilikaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wake meneja wa TARURA Manisoaa ya Bukoba mhandisi
Andondile Mwakitalu amesema katika manispaa hiyo TARURA ina jumla ya
km 165.8 ambapo kati ya hizo kilomita 24.6 zimejengwa kwa kiwango cha lami.
“Katika
mwaka huu wa fedha wa 2018/2019 serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni
1.53 ili kutekeleza miradi sita,kati ya miradi hiyo mitano tayari utekelezaji
wake umeanza kasoro mradi mmoja mchakato wake umechelewa kutokana na kutopatikana
kwa mkandarasi mwenye sifa,”alisema Mwakitalu.
TARURA imeanzishwa mwaka julai 2017 ikiwa na lengo la kufanya matengenezo endelevu ya gharama nafuu
na kusimamia maendeleo ya Mtandao wa Barabara Vijijini na Mijini ili kusaidia
maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.
No comments