Breaking News

MKUTANO WA 20 WA WAKUU WA NCHI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI UMEAHIRISHWA.RAIS Dk. John Magufuli (kulia), akizungumza katika kikao chao na Wakuu wa

nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kushotoni Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika kikao kilichofanyika Ikulu Ndogo, Jijini Arusha (Picha zote na Ikulu).


                                  Na Mwandishi Wetu

MKUTANO wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliyokuwa ufanyike leo mjini Arusha, umeahirishwa.

Akizungumza mara baada ya chakula cha mchana, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema umeahirishwa hadi Desemba 27, 2018 utakapo fanyika tena.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari ilisema kuwa, Rais Museveni, alisema, mkutano huo umeahirishwa kutokana na mmoja wa wanachama wa jumuiya hiyo amba ye ni nchi ya Burundi, kutohudhuria ilihali mkataba wa jumuiya hiyo unataka maamuzi yafanywe na wanachama wote kwa pamoja.

“Tuliamua kuahirisha mkutano kwa leo kwa sababu mmoja wetu ambayeni Burundi hakuja, tumeahirisha mkutano mpaka tarehe 27 Desemba, 2018 wakati sisi wote tutakapokuwepo, kwasababu mkataba wa Afrika Mashariki unasema mambo mawili, moja lazima tuwe na mkutano mmoja wakawaida kila mwaka na ndio huu wa leo.

“Lakini vile vile uamuzi wowote utakaofanyika lazima wanachama wote wawepo, kwahiyo kama mmoja hayupo sio vizuri kuendelea, inakuwa inakwenda kinyume na mkataba” alisema Rais Museveni.

Wakati huo huo, akiwa mkoani hapa Arusha,  kesho  Desemba 01, 2018, Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, wanatarajia kufungua kituo cha huduma za pamoja mpakani (One Stop Border Post) katika eneo la Namanga, mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Mapema leo Novemba 30, 2018, Rais, Dk.  Magufuli, alikutana na Marais,  Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta kando ya Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya wa Kenya kabla ya Mkutano huo uliyekuwa umepangwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Mara baada ya kikao cha ndani kilichofanyika katika moja ya kumbi za watu mashuhuri ndani ya kituo cha AICC, Marais wote watatu walisafiri kwa gari moja hadi Ikulu ndogo ya Arusha Mjini ambako Magufuli, aliwaalika wageni wake kwa chakula cha mchana.
No comments