Breaking News

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YASAINI MKATABA NA WAKALA WA MAJENGO TANZANIA KUANZA UJENZI WA OFISI KATIKA MJI WA SERIKALI JIJINI DODOMA.

KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro (kushoto), na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania, Arch. Elius Mwakalinga, wakitiliana Mkataba wa kuanza rasmi ujenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Mji wa Serikali, Ihumwa Jijini Dodoma, leo.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imesaini Mkataba na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wa kuanza rasmi ujenzi wa ofisi katika mji wa Serikali, Ihumwa Jijini Dodoma.

Mkataba huo umesainiwa ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ya kuhamisha shughuli za Serikali Makao Makuu ya Nchi.

Kabla ya kutiwa saini kwa mkataba huo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema ujenzi wa ofisi hiyo ni hatua muhimu ya kutimiza mpango wa serikali na maelekezo ya  Dk. Magufuli, ya kuhamia Dodoma kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi.

Dk. Ndumbaro, aliitaka TBA kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa ofisi hiyo kwa wakati na kwa kiwango bora ili kuwawezesha watumishi wa ofisi yake kutoa huduma kwa wananchi katika mazingira mazuri.


Dk.  Ndumbaro (kushoto), na Arch. Mwakalinga, wakibadilishana mikataba baada ya kutiliana saini. 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania,  Arch. Elius Mwakalinga, aliishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuiamini ofisi yake na kuwapa kazi ya ujenzi wa ofisi hiyo.

Arch. Mwakalinga, aliahidi kufanya kazi ya ujenzi huo kwa weledi mkubwa kwani wana vitendea kazi vya kisasa vinavyojitosheleza ikiwa ni pamoja na wataalam wa kutosha watakaowezesha kukamilisha jengo hilo kwa kiwango bora na kwa wakati.

'KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania, Arch. Elius Mwakalinga wakionyesha mikataba wa kuanza rasmi ujenzi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika mji wa serikali, Ihumwa jijini Dodoma. 

Aidha, Arch. Mwakalinga, alitoa wito kwa wakuu wa taasisi nyingine kuitumia Wakala wa Majengo Tanzania katika ujenzi wa majengo mbalimbali kwani wako tayari muda wote kutoa huduma kwa kiwango bora.

Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika mji wa serikali, Ihumwa ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dk. John Magufuli, ya kuhamishia shughuli za Serikali Jijini Dodoma aliyoutoa  Julai 25, 2016,  wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa

No comments