RAIS MAGUFULI AKUTANA NA TIMU YA MADAKTARI WA MOYO KUTOKA ISRAEL, MAREKANI NA CANADA
Ikulu,Dar
es salaam
UAMUZI
wa Serikali ya Awamu ya Tano kufungua Ubalozi wa Tanzania nchini Israel umeanza
kuzaa matunda baada ya timu ya madaktari na wataalamu wa matibabu ya moyo 30
kutoka nchini Israel kuja hapa nchini kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto 51
wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es
Salaam.
Timu
ya Madaktari na wataalamu hao wakiwemo wawili kutoka Marekani na Canada
wanatoka shirika la Save
a Child’s Heart la Israel wamekutana na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar
es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi amesema kati
ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika kampeni hii 10 watafanyiwa upasuaji wa
kufungua kifua na 20 watafanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo.
Prof.
Janabi amebainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita Taasisi ya Moyo
ya Jakaya Kikwete imetoa matibabu ya moyo kwa wagonjwa 254,881 ambapo kati yake
wagonjwa 799 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua, 2,056 wamefanyiwa upasuaji
kwa kutumia tundu dogo na wengine wamepatiwa matibabu mengine ya moyo.
Ameongeza
kuwa ushirikiano wa taasisi hiyo na wataalamu kutoka nje ya nchi umesaidia
kuwawezesha wataalamu wa Tanzania kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
na pia kuokoa gharama kubwa zilizokuwa zikitumika kupeleka wagonjwa nje ya
nchi, ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu Tanzania imetumia shilingi Bilioni 22
ikilinganishwa na shilingi Bilioni 87.8 ambazo zingetumika kutoa matibabu hayo
nje ya nchi.
Kiongozi
wa timu ya Madaktari hao kutoka nchini Israel na Mkurugenzi Mtendaji wa Save a
Child’s Heart Bw. Simon Fisher na Mkuu wa Kitengo cha upasuaji wa moyo wa
shirika hilo Prof. Sasson Lior wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano
mkubwa ambao timu hiyo inapata kutoka Serikali ya Tanzania na wameahidi kuwa
taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania kuokoa maisha ya watoto.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amewashukuru madaktari na wataalamu hao kwa kuja
Tanzania kuokoa maisha ya watoto na pia amemshukuru Waziri Mkuu wa Israel Mhe.
Benjamin Netanyahu kwa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri
uliopo kati ya Tanzania na Israel.
Mhe.
Rais Magufuli amemuandikia barua ya shukrani Mhe. Netanyahu na kuikabidhi kwa
Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal Gendler ambapo pamoja na kushukuru
kwa msaada wa matibabu pia amemshukuru kwa ushirikiano katika sekta nyingine.
“Israel ni
marafiki zetu wa siku nyingi, tunasaidiana na kushirikiana kwa mengi, ndio
maana niliona tufungue Ubalozi wetu kule Israel ili kurahisha masuala haya
muhimu ya ushirikiano na yenye manufaa kwa watu wetu”
amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa wito kwa Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Noah Gal
Gendler na wataalamu hao kuwahamasisha wawekezaji wanaoweza kuja kujenga
viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Serikali
itanunua dawa na vifaa hivyo, na pia watakuwa na uhakika wa soko la Afrika
Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mhe.
Rais Magufuli pia amewapongeza Madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuokoa maisha ya watu na amewahakikishia kuwa
Serikali inatambua juhudi hizo na itaendelea kuwajengea mazingira bora ya kazi.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Balozi wa Israel hapa nchini Mhe.
Noah Gal Gendler na baada ya mazungumzo hayo Mhe. Gendler amesema Israel imetoa
nafasi za masomo kwa watanzania 150 watakaogharamiwa na Serikali ya Israel kwa
ajili ya kujifunza utaalamu wa kilimo cha kisasa kwa miezi 11.
Halikadharika
Mhe. Rais Magufuli amekutana na Daktari Bingwa wa upasuaji wa ubongo na uti wa
mgongo Prof. Roger Hartl kutoka nchini Marekani ambaye amepongeza juhudi za
Tanzania kuendeleza huduma za matibabu ya kibingwa na ameahidi kuendeleza
ushirikiano kati ya taasisi yake ya Weill Cornell Medicine iliyopo nchini
Marekani na Tanzania.
No comments