Breaking News

SERIKALI IMETANGAZA UAMUZI WA KUNUNUA KOROSHO ZOTE ZA WAKULIMA MSIMU HUU KWA BEI YA 3,300


Na Mwandishi Wetu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 12 Novemba, 2018 ametangaza uamuzi wa Serikali kununua korosho zote za wakulima msimu huu kwa bei ya shilingi 3,300 kwa kilo baada ya wanunuzi binafsi kushindwa kutimiza maagizo ya Serikali kwa kuanza kununua kwa kusuasua na kwa bei isiyoridhisha.
Mhe. Rais Magufuli ametangaza uamuzi huo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuwaapisha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Joseph George Kakunda, Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Constantine John Kanyasu, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Lugha Bashungwa, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Mhe. Jaji Mstaafu January Henry Msoffe.
Pamoja na kutangaza uamuzi huo Mhe. Rais Magufuli ameagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutoa fedha za kununulia korosho hizo na ameliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupeleka askari katika maghala yote yenye korosho na kuanza ununuzi wa korosho mara moja kwa kushirikiana na Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
Mhe. Rais Magufuli pia ameagiza wakulima waanze kulipwa fedha zao mara moja na bila kukatwa fedha yoyote.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameagiza kiwanda cha kubangua korosho cha BUCCO Investment Holding kilichopo Mkoani Lindi ambacho hivi karibuni kimechukuliwa na Serikali baada ya aliyeuziwa kiwanda hicho kushindwa kukiendesha, kikabidhiwe kwa JWTZ ili jeshi hilo lianze kukitumia kubangua korosho zitakazonunuliwa katika msimu huu.
Kiwanda hicho kina uwezo wa kubangua tani 20,000 za korosho kwa mwaka na Mhe. Rais ameagiza Bodi ya Mazao Mchanganyiko ianze kutafuta soko la ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuuza korosho zikiwemo zitakazobanguliwa kiwandani hapo.
“Mwaka huu huenda tutazalisha kati ya tani 210,000 na 220,000 za korosho, korosho hizi zinaweza kuzalisha tani takribani 70,000 za korosho zilizobanguliwa, kwa hiyo tutanunua korosho zote, tutatafuta soko tutaziuza na tusipopata soko tutakula sisi wenyewe” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli ameagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilichokuwa chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuongeza ufanisi katika kupata wawekezaji wazuri hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli ameionya Bodi ya Pamba na bodi nyingine za mazao kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao kwa maslahi ya wakulima badala ya kuwaacha wakikandamizwa na wanunuzi binafsi na amesisitiza kuwa “kilichotokea kwa Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba ijiandae”.
Kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya aliowateua, Mhe. Rais Magufuli amewataka kurekebisha dosari zote zilizojitokeza katika usimamizi wa Kilimo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, na ameelezea kutoridhishwa kwake na mwenendo wa wizara hizo mbili hali iliyosababisha afanye mabadiliko ya Mawaziri.
“Wizara ya Kilimo mambo mengi imebidi niwe namtuma Waziri Mkuu kwa sababu kwenye wizara hakuna hatua zinazochukuliwa na hakuna maamuzi, nataka Mawaziri muwe mnafanya maamuzi, haiwezekani wakulima wanapata shida Mawaziri mpo, Makatibu Wakuu wenu wapo na wataalamu wapo. Kule Dodoma wakulima wa zabibu wanapata shida mpaka leo hakuna utatuzi wa shida zao” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Tukio hilo limehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambao wamewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kufanya kazi kwa kutambua umuhimu wa wizara hizo na uwekezaji mkubwa ambao nchi imeufanya katika kilimo.
Viongozi wengine waliohudhuria tukio hilo ni Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Siasa, Majenerali wa JWTZ na viongozi wa Taasisi za Serikali.

No comments