Breaking News

SERIKALI INAFANYA MAPITIO YA LESENI ZA UCHIMBAJI-MAJALIWA * ASEMA ZITAKAZOBAINIKA KUTOFANYA KAZI KWA MUDA MREFU ZITAFUTWA.


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi wa Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita, leo Novemba 30, 2018. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Na Mwandishi Wetu, Geita
SERIKALI imesema, inafanya mapitio ya leseni zote za uchimbaji madini na zile ambazo zitabainika kuwa hazijafanya kazi kwa muda mrefu zitachukuliwa na kisha maeneo hayo hayo yatagawiwa kwa wachimbaji wadogo.
Ilisema, Wizara ya Madini imeimarishwa  na sasa inatengeneza fursa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu inayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mji Mdogo wa Katoro.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, leo Novemba 30, 2018, wakati akizungumza na wananchi katika Mji Mdogo wa Katoro uliopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Geita, akiwa kwenye siku ya mwisho mwa ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Geita.
Waziri Mkuu aliwaambia wananchi hao ambao wengi wao ni wachimbaji wadogo kuwa waendelee kuwa na imani na Serikali yao ambayo imedhamiria kuhakikisha wachimbaji hao wanafanya shughuli zao bila ya kubugudhiwa.
“Jipangeni kwa kufanya kazi maeneo yapo na Serikali itawapa. Nawashauri mjiunge katika vikundi vitakavyosajiriwa na kutambilika kisheria ili muende kwenye benki mbalimbali na kukopa fedha za kununulia mitambo ya kisasa itakayowawezesha kuchimba kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” alisema.
Kadhalika, Waziri Mkuu aliiagiza Halmashauri ya wilaya ya Geita ihakikishe kila kijiji kinakuwa na kisima cha maji ili kuwapunguzia wananchi kutumia muda mwingi kwa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji katika maeneo yasiyojulikana.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama inayowakabili wanachi kwenye Mji Mdogo wa Katoro, Waziri Mkuu aliwataka waendelee kuwa na subira kwani Serikali imepanga kuwafikishia maji kutoka ziwa Victoria. 
Majaliwa alisema, Serikali kupitia kampeni ya Rais, Dk. John Magufuli, ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, mbali na kuimarisha huduma za maji  kwenye Mji Mdogo wa Katoro, pia Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya na kikuwezesha Kituo cha Afya cha Katoro kiweze kuwa na maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, chumba cha kujifungulia, wodi za wanawake na wanaume.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema Serikali imeendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo na wa Mji Mdogo wa Katoro ili waendelee kufanya shughuli zao bila ya usumbufu wa aina yoyote.

Alisema katika kuhakikisha wachimbaji hao wafanya shughuli za uchimbaji kwa weledi, Serikali imeamua kujenga vituo vya mfano vyenye lengo la kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu namba bora ya uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa

                                          MAJALIWA akipungia wananchi mikono

Biteko aliongeza kuwa, Mji Mdogo wa Katoro ni miongoni mwa maeneo ambayo Serikali imejenga kituo hicho katika eneo la Lwamgasa. Pia amesema wachimbaji wadogo kwa sasa wanaendelea na shughuli zao katika maeneo mbalimbali kwa uhuru na Amani yakiwemo ya Bingwa, Musasa, Nyamalimbe, Nyarugusu, Lwamgasa.

Naibu Waziri huyo alitaja maeneo mengine nchini ambayo Serikali inaendelea na miradi ya ujenzi wa vituo hivyo kuwa ni pamoja na Lindi, Chunya, Mpanda, Tanga na   Buhemba mkoani Mara.
Naye, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani aliwahakikishia wakazi wa Mji Mdogo wa Katoro na Buselesele kuwa maeneo yao yote ambayo hajaunganishiwa umeme wasiwe na wasiwasi umeme utawaka kabla ya sikukuu ya X-Mas na kuongeza kuwa, tayari mkandarasi ameshafika kwenye maeneo hayo na kuanza  kazi.
Dk. Kalemani alifafanua kuwa, maeneo hayo yatasambaziwa umeme kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi hawatowajibika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

                                                      WAZIRI Mkuu Majaliwa

“Rais wetu Dk. John Magufuli, anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Awali, Mbunge wa Busanda, Lolencia Bukwimba, alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za huduma za afya kwa kuwa kituo chilichopo hakitoshelezi mahitaji kwani watu wengi. Ameomba Serikali iwajengee hospitali na kuimarisha huduma za mama na mtoto kwa kuwa kwa mwezi wanazaliwa watoto 700.

No comments