TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA NCHI ZA MAZIWA MAKUU- MAJALIWA.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Nchi za Bonde la Mto Nile za Ukanda wa Maziwa Makuu kwenye hoteli ya Serena Jijini Dar es salam, leo Novemba 22, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
Muu Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na
nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu katika kusimamia matumizi endelevu ya maji ya
Mto Nile kwa ustawi wa kiuchumi wa nchi zote.
Aliyasema
hayo leo Novemba 22, 2018 wakati akifungua mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri
la Nchi za Bonde la Mto Nile zilizopo Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika Jijini
Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli.
Alisema
nchi wanachama hazina budi kuimarisha ushirikiano ili ziweze kusimamia vizuri
matumizi endelevu ya maji ya Mto Nile pamoja na kushughulikia changamoto
zinazolikabili Bonde la Mto Nile.
Waziri
Mkuu alitaja baadhi ya changamoto zinazolikabili Bonde la Mto Nile kuwa ni
pamoja na kushindwa kufikia makubaliano ya kuanzisha Kamisheni ya Kudumu ya
Bonde la Mto Nile. “Kwa takribani miaka 10 sasa tumeshindwa kufikia
makubaliano.”
MAJALIWA akisalimiana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, wakati alipowasili kwenye Hoteli ya Serena Jijini Dar Es Salaam kufungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Nchi za Bonde la Mto Nile za Ukanda wa Maziwa Makuu kwenye hoteli hiyo.
Alisema, sambamba na changamoto hiyo nchi wanachama zimekuwa
zikichelewa sana kutoa michango yao ili kuziwezesha taasisi zao kutekeleza
ipasavyo majukumu yao, jambo ambalo si tu linachelewesha maendeleo bali
linatishia usalama wa maji katika Bonde la Mto Nile.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu alitoa mapendekezo mbalimbali ili
kuhakikisha kunakuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwenye Bonde la
Mto Nile pamoja na kusaidia nchi wanachama kupata maendeleo.
Moja ya mapendekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni pamoja na nchi
wanachama kutoa elimu kwa wananchi wake kuhusu matumizi sahihi ya maji na
umuhimu wa kutunza vyanzo vyake ili kuhakikisha kunakuwepo na matumizi endelevu
ya maji.
“Suala jingine ni ulipaji wa michango. taasisi zetu haziwezi
kutekeleza majukumu yake kama hatulipi michango tena kwa wakati maana miradi ya
maendeleo haiwezi kutekelezwa kwa haraka kwa kutegemea wafadhili. Ni vema nchi
zikalipa michango,” alisema.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema maji ni rasilimali muhimu duniani
kwa ajili ya uhai wa binadamu, maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususani katika
kuendesha shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji, utalii na ujenzi, hivyo lazima
vyanzo vitunzwe.
KASSIM Majaliwa (kushoto), akipata maelezo kutoka kwa George Lugomela, kuhusu mashine ya kutambua uwepo wa maji ardhini kabla ya kufungua mkutano huo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu huyo, Bara la Afrika ni miongoni mwa
maeneo yanayokabiliwa na matatizo makubwa ya maji duniani, ambapo takwimu zinaonesha
kuwa takribani nchi 14 hivi sasa zinakabiliwa na uhaba ama upungufu wa maji
huku zingine 11 zinatarajiwa kuingia katika kundi hilo ifikapo 2025.
Alisema, kutokana na hali hiyo mikakati ya makusudi inahitajika
ili kuhakikisha chanzo hiko cha maji kinalindwa na rasilimali ya maji katika
Bonde la Mto Nile inatumika vizuri.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, akitazama burudani ya ngoma wakati alipowasili kwenye Hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam kufungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Nchi za Bonde la Mto Nile za Ukanda wa Maziwa Makuu, leo Novemba 22, 2018. Wapili kulia ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mbarawa Makame na watatu kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Balozi Dk. Augustine Mahiga.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa,
ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Bonde la Mto Nile
zilizopo kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Nishati Dk. Medard
Kalemani.
Wengine ni Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Awesu, Mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao nchini, watendaji wa Sekretarieti ya Bonde la Mto
Nile kutoka Ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na Ukanda wa Mashariki na maofisa
wengine wa serikali.
No comments