Breaking News

TANZANIA YAWEKA HISTORIA MPYA YAFUNGUA MAKTABA KUBWA YA KWANZA AFRIKA MASHARIKI NA KATI. * JPM ATOA NENO ASEMA NI MATUNDA YA URAFIKI WA TANZANIA NA CHINA.


                       
                     
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli akihutubia katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.Na Mwandishi Wetu


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.  John Magufuli, leo Novema  27, 2018 amefungua maktaba mpya, kubwa na ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyojengwa katika Kampasi Mlimani (Mwl. Julius K. Nyerere) Jijini Dar es Salaam.

Maktaba hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati, imejengwa kwa gharama ya sh. Bilioni 93.6 ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya China na inakuwa maktaba kubwa kuliko maktaba zote ambazo China imezijenga barani Afrika.

MAGUFULI akirudisha kitabu hicho kwenye shelfu la vitabu mara baada ya kukisoma huku Balozi wa China hapa nchini Wang Ke akiangalia

Katika taarifa yake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye, alisema majengo ya maktaba hiyo yenye ghorofa mbili, yamechukua eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 20,000 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi vitabu 800,000, kukalisha watumiaji 2,100 kwa wakati mmoja.

Pia, ina kompyuta 160 zilizounganishwa na mtandao kwa ajili ya kusoma vitabu kwa njia ya kielektroniki, ofisi za wafanyakazi, eneo la wanafunzi wenye mahitaji maalum na ukumbi wa kisasa wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua watu 600.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli akizungumza jambo na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke wakati wakiagana mara baada ya hafla ya ufunguzi wa Maktaba hiyo ya Kisasa.Prof. Anangisye ameishukuru serikali kwa mchango mkubwa uliosaidia kufanikisha ujenzi wa maktaba hiyo, ameishukuru Serikali ya China kwa kutoa msaada wa fedha za ujenzi huo na kampuni ya ujenzi ya Jiangsu Jiangdu ya China kwa kujenga majengo yenye ubora na hadhi ya hali ya juu.

Aliahidi kuwa, Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itahakikisha majengo ya maktaba hiyo yanatunzwa vizuri na maktaba inatumika kuwanufaisha wanafunzi wa chuo hicho pamoja na wanafunzi wa taasisi zingine za vyuo na wananchi wa kawaida.

BAADHI ya Mabalozi  wanaoziwakilisha nchi zao wakifatilia kwa makini hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli kabla ya kuifungua rasmi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, alimshukuru Rais Magufuli, kwa namna anavyotoa kipaumbele kwa sekta ya elimu na aliahidi kuwa wizara yake itaendelea kuhakikisha taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo zinaendeshwa kwa kuzingatia maadili na matumizi bora ya rasilimali.

Pia, waziri huyo alimshukuru Balozi wa China hapa nchini,  Wang Ke, kwa kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu ujenzi wa maktaba hiyo na kwa Serikali ya China kutoa sh. Bilioni 50.8 kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha elimu ya mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Mkoani Kagera.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu Msataafu Edward Lowassa mara baada ya kuwasili katika eneo la Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.Akizungumza katika sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli amemshukuru Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke na kumuomba apeleke shukrani za Tanzania kwa Rais wa China Mhe. Xi Jinping kwa misaada ambayo China imekuwa ikiitoa kwa Tanzania, ikiwemo ujenzi wa Maktaba hiyo na Chuo cha VETA kitakachojengwa Mkoani Kagera.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema, urafiki wa China na Tanzania ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Nyerere, na Mwenyekiti Mao Zedong, umeendelea kuleta manufaa makubwa na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano na itauendeleza na kuukuza uhusiano na ushirikiano huu mzuri.

                   Mandhari ya nje ya Maktaba hiyo kama inavyoonekana. 

“Jambo la kufurahisha ni kwamba misaada yao haiambatani na masharti. Wenyewe wakiamua kukupa wanakupa, walitujengea TAZARA, URAFIKI na pia wametusaidia katika maeneo mengine ya maendeleo,” alisema Magufuli na kumhakikishia Balozi Wang Ke, kuwa Serikali itahakikisha kila msaada unaotolewa unatumiwa vizuri.

Aidha, Rais Magufuli alimpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya
 Nne, Jakaya Kikwete, na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mstaafu, Prof. Rwekaza Mukandala kwa kuandaa mpango wa ujenzi wa maktaba hiyo na pia aliwapongeza Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kwa kupata maktaba ambayo itawasaidia kuongeza kiwango cha ubora wa elimu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipata maelezo mbalimbali ya  maktaba hiyo mpya itakavyokuwa ikihudimia wanafunzi na wadau mbalimbali wa elimu watakapoanza kuitumia.Aliwataka wana Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kuhakikisha maktaba hiyo inatunzwa vizuri na ametoa wito kwa Watanzania kujifunza lugha ya Kichina katika jengo mojawapo la maktaba hiyo litakalokuwa likifundisha lugha hiyo kwa kuwa kuna manufaa makubwa kwa Watanzania kujifunza lugha hiyo.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa China hapa nchini,  Wang Ke, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Jaji mstaafu Joseph Warioba na Edward Lowassa, mawaziri, mabalozi wa nchi mbalimbali na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Paul Makonda.

No comments