Breaking News

WADAU WA SEKTA YA AFYA KUENDELEA KUBORESHA UTOAJI WA HUDUMA NCHINI.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mpoki Ulisubisya (Katikati), akisaini makubaliano ya malengo na vipaumbele vya kisera vya mwaka 2019/2020. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia  Afya TAMISEMI Dk. Zainab Chaula. Kulia ni Mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo.


NA WAJMW-DODOMA

SERIKALI  kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kuboresha huduma afya nchini kwa kukarabati vituo vya afya vipatavyo 350 ili  utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto hususani  huduma za dharura wakati wa kujifungua.

Hayo yalisemwa jana Novemba 26, 2018 na  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu, wakati wa mkutano wa mwaka wa wadau wa sekta ya afya wa kujadilia njia zitakazowezesha kufikia malengo na vipaumbele vya kisera vya mwaka 2019/2020 uliofanyika mapema  jijini Dodoma.

“Sekta ya afya tunaona inaendelea kupiga hatua kubwa sana katika maeneo mbalimbali ikiwemo suala la kuimarisha miundombinu ambapo vituo vya Afya takribani 350 vimekarabatiwa kwa  kuongeza miundombinu kwa ajili ya kutoa huduma za afya za dharura ikiwemo huduma za kumtoa mtoto tumboni,”alisema.

        WAZIRI Ummy akihutubia kwenye mkutano huo jana

Waziri Ummy alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo duniani inahakikisha sekta ya afya inapata mafanikio kwa kuboresha huduma nchini ikiwemo na kufikia asilimia zaidi ya 90 ya dawa zinapatikana katika sehemu zote za kutoa huduma.

Aidha, Waziri Ummy alisema mkutano huo ulikua na lengo la kukubaliana kutekeleza vipaumbele nane (8) ambavyo serikali pamoja na wadau wa maendeleo itahakikisha vinatekelezwa ipasavyo katika mwaka 2019/2020.

Maeneo hayo ni pamoja na kuimarisha huduma za afya ya uzazi,  mama na mtoto ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi,  kwa kuweka miundombinu ya huduma za uzazi wa dharura na watoto wachanga kwani kwa takribani hivi sasa watoto wachanga wapatao elfu 90 hufariki ndani ya siku 28 za mwanzo.

WADAU mabalimbali wa maendeleo wakifuatilia kwa makini majadiliano yaliyokua yanaendelea katika mkutano huo Jijini Dodoma jana.

Eneo la pili linahusu afya za wasichana na wavulana walio katika umri wa kubalehe ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kuepuka ngono katika umri mdogo na mimba zisizotarajiwa.

Alitaja eneo jingine  ni kuongeza nguvu kazi katika sekata ya afya ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi wa afya katika ngazi zote, kuongeza ujuzi kwa kutoa nafasi za kusomesha watumishi ili kukidhi vigezo vilivyoweka na shirika la afya duniani (WHO).

Kipaumbele cha Nne, ni kuimarisha ubora wa huduma za afya utakaoenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya sehemu za kutolea huduma za afya za serikali pamoja na kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za afya kwa kuongeza  ya bajeti ya afya   kutoka kutoka Bilioni 31 hadi Bilioni 270 mwaka 2018/2019.

WKUGENZI mabalimbali wa maendeleo wakifuatilia kwa makini majadiliano yaliyokua yanaendelea katika mkutano huo.

Naye Naibu katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia afya Dk. Zainabu Chaula, alisema kwamba wao kama sehemu ya utekelezaji wamejipanga kutekeleza maboresho ya afya ngazi ya msingi kuanzia vijijini hadi Taifa kupitia sera ya afya.

Alisema wamejipanga kuongeza kutoa elimu ya afya kwa umma kuanzia zahanati  kwa kupanga mipango endelevu ili iende sambamba kuanzia ngazi husika kwa kutumia kamati za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.  

No comments