Breaking News

WANANCHI SHIRIKIANENI KUJENGA MABWENI YA SHULE: MAJALIWA.


WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA


Na Mwandishi Maalumu, Lindi

WANANCHI wa Kata ya Mnacho wilayani Ruangwa, wametakiwa kushirikiana  kujenga mabweni katika shule ya Sekondari Mnacho ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembelea umbali mrefu kwenda shuleni hapo.
Agizo hilo limetolewa leo Novemba 19, 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni, ambalo ujenzi wake unagharimu sh. milioni 92.4 ikiwa ni mchango uliotolewa na wadau mbalimbali wa elimu.
“Bweni hili likikamilika litawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kuja shuleni hususani wanaoishi vijiji vya mbali kwa sababu wataishi hapa, jambo ambalo litachangia kuongeza ufaulu wa watoto wetu,” alisema Majaliwa.
Pia, Majaliwa, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waishio katika kata hiyo na za jirani washirikiane na kuanzisha mradi wa ujenzi wa mabweni mengine kwa kuwa hilo moja lililojengwa na wadau halitoshi kulingana na idadi ya wanafunzi.
Alisema yeye (Majaliwa), yuko tayari kuendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye mipango yao yote ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata yao, lengo likiwa ni kuhakikisha mikakati ya serikali ya kuboresha huduma za jamii inatimia.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka wananchi hao washirikiane na walimu kufuatilia maendeleo ya taaluma kwa watoto wao shuleni na kujiridhisha kama wanafanya vizuri darasani na iwapo watabaini changamoto waweze kuzitatua kwa pamoja.  
Akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni hilo, Mkuu wa Sekondari hiyo Mnacho, Mwalimu David Mwakalobo, alisema ujenzi wa bweni hilo lenye uwezo kulaza wanafunzi 80 ulianza Septemba 19, mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Januari mwakani.
Alisema, kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo shuleni, bweni hilo litakidhi mahitaji ya kuwalaza wanafunzi wa kike tu, hivyo aliwaomba wahisani waendelee kuwasaidia ili wapate bweni lingine kwa ajili ya kuwalaza wanafunzi wa kiume.
Kwa mujibu wa Mwakalobo, iwapo watafanikiwa kuwa na mabweni ya kuwalaza wanafunzi wote 334 shuleni hapo, yatawasaidia katika kutatua changamoto ya utoro na mdondoko wa kitaaluma kwa wanafunzi kwa sababu wengi wanatoka mbali.
Alisema pia, mradi wa ujenzi wa mabweni utasaidia walimu kuwa karibu na wanafunzi wakati wote, hivyo kupata muda mwingi wa kuwasaidia wanafunzi kimasomo kwa sababu watakuwa wanaishi shuleni na kwamba mradi huo pia, utapunguza idadi ya wanafunzi wengi wa kike kupata mimba.
Mwakalobo, aliongeza kuwa, uwepo wa mabweni shuleni hapo utaongeza ari ya wanafunzi kupenda masomo tofauti na ilivyo sasa kwa sababu wengi wanalazimika kutokana na kutembea muda mrefu kwakuwa wanatoka vijiji vya mbali jambo linalowafanya wasipende kusoma.

No comments