Breaking News

WAZIRI MKUU AAGIZA MRADI WA MAJI CHATO UKAMILIKE KWA WAKATI * NI WA IMALABUPINA/ICHWANKIMA WENYE THAMANI YA SH. BIL. 8.28.


WAZIRI  Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua ujenzi wa mradi wa Maji wa Imalabupina - Ichwankima wilayani Chato leo Novemba 27, 2018. Kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mwita Waitara na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandishi Robert Gabriel. (Picha zote na  Ofisi ya Naziri Mkuu).


Na Mwandishi Wetu, Geita
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameweka jiwe la msingi mradi wa maji wa Imalabupina/ Ichwankima wilayani Chato ambao una thamani ya sh. bilioni 8.28 na amewaagiza viongozi wa wilaya hiyo wahakikishe unakamilika kwa wakati.
Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia kampeni ya Rais Dk. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (wa pili kulia), akiwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki wakati alipowasili kwenye Kiwanja cha Ndege cha Chato kuanza ziara ya kikazi mkoani Geita, leo Novemba 27, 2018.  Kutoka ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI,  George Waitara, Waziri wa Nishati na Mbunge wa Chato Dk. Medard Kalemani na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gbriel.


Aliyasema hayo leo Novemba 27, 2018, alipozungumza na wananchi kwenye kijiji cha Nyamirembe baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi huo wa maji wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Geita.

Alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha wananchi wote nchini wakiwemo na wa wilaya ya Chato mkoani Geita, wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao, hivyo amewataka waendelee kuwa na imaji na serikali yao.

MAJALIWA, akisalimiana na viongozi wa dini wakati alipowasili kwenye  eneo la mradi wa Maji wa Imalabupina - Ichwankima kuweka jiwe la msingi la mradi huo wilayani Chato,

Alisema, Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo mbalimbali nchini vikiwemo na vijiji vya wilaya ya Chato ili kuwawezesha wananchi kupata maji,” aliseama.

Waziri Mkuu aliagiza mradi huo ukamilike kwa wakati kwa kuwa serikali inahitaji kuona wananchi wakinufaika na huduma hiyo. Mradi huo ulianza kujengwa Mei, 2017 na ulitakiwa ukamilike Mei, 2018, lakini kutokana na changamoto mbalimbali unatarajiwa kukamilika Februari 2019.

WAZIRI Majaliwa, akisalimiana na mtoto, Naomi Nkingwa, ambaye alishirkiana na wanakwaya wa Kikundi cha Mwagazege cha Chato kuimba nyimbo za kumkaribisha alipowasili kwenye Kiwanja cha ndege cha Chato.

Awali, Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi, Mtemi Simeon, alisema mradi huo unatarajiwa kuhudumia watu takribani 59,609 katika vijiji 11 vilivyopo kwenye kata nne za Nyamirembe, Ichwankima, Kachwamba na Kasenga.

MAJALIWA, akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Geita, Alhaj  Said Kalidushi, wakati alipowasili kwenye Kiwanja cha Ndege cha Chato. Katikati ni Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel.

Alivitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huu ni Nyamirembe, Kalebezo, Nyambiti, Busalala, Imalabupina, Ichwankima, Kachwamba, Ipandikilo, Idoselo, Igagula na Mwangaza. Tayari vituo 240 vya kuchotea maji vimeshakamilika na matenki nane kati ya tisa yamekamilika pamoja na mabirika 10 ya kunyweshea mifugo.

No comments