Breaking News

WIZARA YA NISHATI NA JICA WAJADILI MPANGO WA UENDELEZAJI WA MATUMIZI YA GESI ASILIA.


KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati Dk. Hamis Mwinyimvua akiongoza kikao cha kujadili mpango wa uendelezaji wa matumizi ya Gesi asilia nchini akiwa na ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), kilichofanyika Jijini Dodoma jana.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati,  Dk.  Hamisi Mwinyimvua,  ameongoza kikao kati ya Wizara ya Nishati na ujumbe  kutoka Shirika la Maendeleo la Japan  (JICA),  kilicholenga  kujadili Mpango wa uendelezaji wa matumizi ya Gesi asilia nchini (Domestic Natural Gas Promotion Plan - DNGPP).

Kikao hicho kimefanyika jana  katika ukumbi wa Wizara ya Nishati Jijini Dodoma  na kuhudhuriwa na Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya,  Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango,  Fortunatus  Mlwanda  na maofisa kutoka  Idara ya Petroli na  Gesi na Sera na Mipango. Ujumbe wa JICA uliongozwa na Kensuke Kenekiyo.

Ujumbe huo wa JICA, uliwasilisha matokeo ya utafiti wa mahitaji ya Gesi asilia uliofanywa katika Miji ya Arusha, Moshi, Morogoro, Dodoma na Tanga  chini ya ufadhili wa Shirika hilo na kuhusisha wataalam kutoka kutoka Wizara  ya Nishati na Shirika la  Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC).

JICA wameeleza kuwa zipo njia mbadala za kufikisha  Gesi asilia katika  miji hiyo  tofauti na njia  iliyozoeleka  ya  kujenga  bomba  ambapo  njia  zilizoainishwa  ni  pamoja  na kutumia mitungi  yenye  gesi  iliyokandamizwa  (Compressed Natural Gas - CNG),  kujenga mitambo midogo ya kubadili gesi kuwa kimiminika  ( mini - LNGs) kisha kuisafirisha kwenda miji husika au kwa njia ya mitungi ya petroli iliyogeuzwa kimiminika ( Liquefied Petroleum Gas - LPG) .

Aidha, JICA imewasilisha uchambuzi wa kiuchumi unaoonesha gharama za kufikisha gesi asilia katika miji tajwa kwa kutumia bomba ukilinganisha na njia nyingine kama vile CNG, mini - LNG na LPG.

Kazi hiyo ya utafiti wa mahitaji ya gesi asilia katika miji tajwa inatarajiwa kukamilika rasmi mwishoni mwa mwezi Desemba 2018 ambapo taarifa kamili itawasilishwa serikalini.

 Katibu Mkuu aliipongeza JICA kwa utafiti huo na kuwashauri kuhusisha utafiti wao na namna ambavyo ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda utasaidia katika usambazaji na matumizi ya gesi katika mikoa itakayopitiwa na Bomba hilo.

No comments