Breaking News

BALOZI IDDI: ZANZIBAR HAIKO TAYARI KUPOKEA MISAADA YENYE MASHARTI KUTOKA KWA WASHISANI.


MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (kulia), leo Desemba 29, 2018 akisalimiana na Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Modesti Jonatan Mero, alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushisha wadhifa huo wa Kidiplomasia.
                        Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAMAKU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar haitakuwa tayari kupokea msaada wowote wa Wahisani ambao utatanguliwa na masharti yenye nia ya kwenda kinyume na utamaduni, mila, silka na utaratibu wa Taifa.
Alisema Zanzibar ina nia njema ya kushirikiana na Taasisi zozote za Kitaifa na Kimataifa kwa lengo la kustawisha maslahi ya wananchi wake kama inavyofanya kwa Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi zake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo leo Desemba 29, 2018 wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Modesti Jonatan Mero, alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushisha wadhifa huo wa Kidiplomasia.
Alisema, Zanzibar na watu wake ina  utamaduni na silka zake zinazopaswa kuheshimiwa na wageni wanaoitembelea na kamwe haitakuwa tayari kuruhusu tabia za kigeni zilizo kinyume na imani za wananchi kuendelezwa visiwani humo.
Balozi Iddi, alisema Zanzibar ina uhusiano wa karibu na Umoja wa Mataifa pamoja na Taasisi zake na kupongeza Balozi huyo wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vyema msimamo wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa.
Alisema katika kusimamia uhusiano huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuzipatia viwanja Taasisi za Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi zao ili ile dhana ya uwepo wao Visiwani Zanzibar ifanikiwe vyema.
Balozi Iddi, alimuelezea Mwakilishi huyo wa Tanzania Umoja wa Mataifa kwamba umoja huo bado una kazi kubwa ya kutanzua changamoto zilizopo katika Mataifa Wanachama hasa suala la amani, mazingira pamoja na maradhi yanayowasumbuwa wananchi wa mataifa hayo.
Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Modesti Jonatan Mero, alisema Tanzania inatarajiwa kuwasilisha taarifa yake katika vikao vya Umoja wa Mataifa  Julai, 2019, ikiwa miongoni mwa Nchini 92 wanachama za mwanzo zilizoteuliwa na umoja huo.
Balozi Iddi (kulia), akizungumza na Balozi Mero, (Picha zote na OMPR – ZNZ).
Balozi Modesti alimueleza Balozi Iddi, kwamba hiyo ni nafasi ya Tanzania kujenga heshima kwenye umoja huo ambapo aliwashauri wadau watakaohusika na taarifa hiyo kushirikiana na Hazina ya Jamuhuri ya Muungano waTanzania na ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kukamilisha ripoti ya taarifa hiyo.
Alisema jihihada zilizopo hivi sasa kwa Wanadiplomasia wa Tanzania ndani na nje ya Nchi ni kuielezea Tanzania mpya ndani ya vikao vya Umoja huo na Taasisi za Kimataifa iliyojielekeza zaidi kiuchumi ili ieleweke vyema malengo yake ya kuingia katika nchi ya viwanda.
Alifahamisha kwamba Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa na ushiriki mzuri katika vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jambo ambalo huleta faraja kwa Taifa na Jamii kwa ujumla.
Alisema yapo mambo yanayozungumza kupitia Uwakilishi wa Mawaziri wa Wizara husika kwenye vikao hivyo akitolea mfano masuala ya afya, mazingira, hali ya amani na usalama pamoja na mafungamano ya Mataifa Wanachama.
Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Modesti Jonatan Mero aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wananchi wake chini ya Rais wake Dk. Ali Mohamed Shein kutokana na Maendeleo makubwa yaliyopamba moto kila kukicha.
Balozi Modesti alisema Maendeleo hayo ya Miaka Miwili  hasa katika Sekta ya Uwekezaji kupitia Utalii yamekuwa yakishuhudiwa na Mabalozi wa Kigeni waliopo Tanzania wakiwa ni Wawakilishi wa kuyatangaza maendeleo hayo katika Mataifa yao.
Akigusia ushiriki wa Watanzania katika fursa za ajira za Umoja wa Mataifa, Mwakilishi huyo wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa alisema nafasi hizo zipo lakini kilichopo ni ukosefu wa uelewa wa mfumo kwa Watanzania hao.
Balozi Modesti alisema kitengo cha Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kilichotoa muelekeo tayari kimewajengea uwezo baadhi ya Watanzania kuchangamkia fursa zinazotolewa za ajira za Umoja huo.

No comments